by Admin | 5 March 2022 08:46 pm03
Ipo kanuni moja ya kuuvuta uwepo wa Mungu na miujiza ya kiMungu karibu nasi. Na kanuni yenyewe ni KUKAA KATIKA UTARATIBU. Mungu siku zote ni Mungu wa utaratibu!, mahali pasipo na utaratibu basi pia Mungu hayupo hapo!.. Hiyo ndio kanuni yake, na hawezi kubadilika!, yeye siku zote atabaki kuwa wa utaratibu…
1Wakorintho 14:40 “Lakini mambo yote na yatendeke kwa UZURI NA KWA UTARATIBU”.
Upo utaratibu katika Nyumba ya Mungu. Ambao huo tukiufuata basi tutaona baraka za Mungu zikijizidisha kwa kasi sana… Na utaratibu wenyewe ni kukaa katika mipaka.
Kanisa likikosa mipaka ya Jinsia, Umri, na Marika.. Ni ngumu Mungu kutembea hapo, kadhalika likikosa utaratibu wa utendaji wa karama, pia kuna shida!. Katika kanisa Wanawake hawana budi kujitofautisha na wanaume, kimwonekano na kiutendaji.. Kadhalika kanisa ni lazima kuwe na utaratibu bora na mpangilio bora..
Hebu tujifunze mfano mmoja kwenye biblia, ambao utatusaidia kuelewa Zaidi..
Marko 6:38 “Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili.
39 AKAWAAGIZA WAWAKETISHE WOTE, VIKAO VIKAO, PENYE MAJANI MABICHI.
40 WAKAKETI SAFU SAFU, HAPA MIA HAPA HAMSINI.
41 Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.
42 Wakala wote wakashiba.
43 Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia.
44 Na walioila ile mikate WAPATA ELFU TANO WANAUME”.
Umeona hapo?..Bwana asingeweza kuigawa ile mikate mahali ambapo hapakuwa na utaratibu!, watu wamekaa shaghala bhagala, watu wamechanganyikana wanaume na wanawake Pamoja.. Lakini walipokaa katika safu, na katika vikao vikao, ndipo ilipojulikana idadi ya Wanaume na wanawake na Watoto.. Na ndipo Bwana akaongeza baraka zake.
Na sisi pia hatuna budi kukaa katika safu, tuwapo katika nyumba ya Mungu, hatuna budi kujipanga na kujitofautisha kwasababu Mungu anafanya kazi zake katika utaratibu.. Hali kadhalika karama hazina budi kufanya kazi katika utaratibu.. Mmoja akiongea sharti wengine wote watulie wasikilize..
1Wakorintho 14:29 “Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.
30 Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.
31 Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.
32 Na roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu”.
Vile vile wanawake katika kanisa wanapaswa wawe watulivu..Maandiko yanasema wanawake wajifunze katika utulivu.. Huo ni utaratibu Mungu aliouweka!.. tukiuvunja huo Basi hata Bwana hatatuvunjia mikate ya baraka..Tutabaki na vurugu zetu, na hatutaambulia chochote!.
Je upo katika Safu?..upo katika utaratibu wa Bwana?..Upo katika utulivu?
Je unaingia nyumbani kwa Bwana kama unavyoingia disko?..fahamu kuwa unajipunguzia baraka zako mwenyewe..Nyumbani kwa Bwana sio kijiwe cha kupiga stori wala jukwaa la matamasha, kwamba unaweza kukaa tu utakavyo na kufanya utakalo.
Bwana atusaidie tukae katika utaratibu wake.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/03/05/tuyatende-mambo-yote-kwa-uzuri-na-utaratibu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.