Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana?

by Admin | 22 April 2022 08:46 am04

SWALI: Yohana alimaanisha nini aliposema..10]Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana?

Je hiyo siku ya Bwana ni ipi? Na kwanini  itajwe pale?

Ufunuo wa Yohana 1:10

[10]Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,


JIBU: Mtume Yohana alikuwa katika kisiwa cha Patmo, kwa ajili ushuhuda wa Kristo, Na kwa mara ya kwanza alipotokewa na Bwana Yesu  na kuonyeshwa mambo yanayohusiana na siri za siku za mwisho na kanisa, anasema siku hiyo aliyotokewa iliangukia  siku ya Bwana.

Swali je siku hiyo ni siku ipi?

Ikumbukwe kuwa tangu awali wakristo wa kwanza, waliifanya siku ya kwanza ya juma( Yaani jumapili) kuwa ni siku ya Bwana, kufuatana na tukio la kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Na ni siku ambayo Bwana alikuwa akiwatokea wanafunzi wake (Soma Marko 16:9, Yohana 20:19 ).

Vilevile Siku hii hii ndio siku ambayo kanisa lilipokea ahadi ya Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza..Kwahiyo watakatifu wote, tangu enzi za mitume, hadi wakati wetu huu wa sasa waliifanya siku hii kuwa ni siku ya Bwana.

Soma vifungu hivi;

Matendo ya Mitume 20:7

[7]Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.

1 Wakorintho 16:2

[2]Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;

Na ndio hapa sasa  tunaona mtume Yohana anaeleza Kwamba alipokuwa katika Roho, siku ya Bwana (yaani jumapili) ndio alitokewa na maono hayo..

Zingatia:  Mtazamo ambao siku hiyo ilikuwa ni jumamosi, si sahihi. Jumamosi, haikuwahi kuadhimishwa na wakristo wa kwanza kwa shughuli rasmi za kibada, kwa mujibu wa maandiko.

Lakini kulikuwa na umuhimu gani habari ya siku hiyo kuandikwa?

Sio kwamba Bwana anaithamini jumapili, zaidi ya siku nyingine zote, hapana au siku hiyo ni takatifu zaidi ya nyingine zote, Hapana bali anachotaka kutuonyesha ni umuhimu wa siku tunazoziweka wakfu kwa ajili yake kwamba anaziheshimu na kwamba kwa kupitia hizo, ni rahisi yeye kujifunua kwetu.

Ikiwa siku yetu kwa Bwana ni jumamosi, basi tuithamini kwa kuwa katika Roho kama vile Yohana alivyokuwa mpaka Kristo akamtembelea siku hiyo..

Kama ni jumapili, tuifanye vivyo hivyo, kama ni jumatano tuipe heshima yake. Hizi siku tusizichukulie juu juu tu,

Lakini leo hii tunapuuzia ibada kuu za kila wiki (Jumapili), tunakosa mafundisho ya biblia kanisani, au hata tukienda siku hiyo hatuwi katika roho, tunaenda ili kutimiza tu wajibu . Halafu tunataka Bwana ajidhihirishe kwetu tunapokuwa nyumbani tunaangalia tv.

Kamwe Usiruhusu, siku yako ya ibada  iliwe na uvivu au mambo ya ulimwengu huu, kama vile anasa, na mihangaiko ya dunia, hata kama upo katika mazingira ambayo hayana watakatifu..Nenda milimani huko, au maporini ukasome biblia na kuomba kama Yohana..kuliko kumwachia shetani akupangie ratiba zake kwenye siku takatifu ya Bwana..

Ithamini siku ya ibada. Na kwa hakika atajidhihirisha kwako.

Ubarikiwe.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?

Dini ni nini, na Imani ya kweli ni ipi?

UFUNUO: Mlango wa 1

Nini maana ya kumwabudu Mungu katika Roho na kweli?

JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?

JIWE LILILO HAI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/04/22/nalikuwa-katika-roho-siku-ya-bwana/