NI NINI KINATOKA KINYWANI MWA MTOTO WAKO?

by Admin | 26 July 2022 08:46 pm07

Nakusalimu tena katika jina la Bwana Yesu mwokozi  wetu, karibu katika kutafakari Maneno ya uzima..huu ni mwendelezo wa Makala  zinazohusu malezo ya Watoto kwa mzazi.

 Ikiwa wewe ni mzazi au mlezi na unao Watoto wadogo chini yako wa kuwalea, au unatarajia kuwa na Watoto.. Basi Makala hii ni muhimu sana kwako,

Zipo Makala nyingine tulishazitazama huko nyuma ikiwa hukuzipitia, basi waweza waweza wasiliana nasi inbox kwa namba hizi +255693036618 tuweze kukutumia.

Leo tutaona umuhimu wa kuwafundisha, Watoto nyimbo za kumsifu Mungu au kumwimbia..Awali ya yote ni lazima ufahamu kuwa, kila mtoto amewekewa ibada ya sifa ndani yake, haijalishi utalipenda hilo au hautalipenda..Na ibada hiyo huwa inakamilika pale anapokutana na Watoto wenzake kwenye michezo sehemu za wazi..Hapo ndipo utajua hicho kitu kipo ndani yake.

Kaa chunguza kwa makini, mahali palipo na Watoto wengi wamekusanyika, utasikia wakiimba vi-nyimbo Fulani mbalimbali, kulingana na kile ambacho walifundishwa, au wanachokisikia watu wengine wakiimba..

Na ndio maana Bwana Yesu alitumia mfano wa Watoto wanaocheza, masokoni, kwa kuimba, kukifananisha kizazi hiki jinsi mienendo yao ilivyokuwa na mwitikio mdogo wa injili..

Luka 7:31 “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?

32 Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia”.

Sasa wewe ukiwaona wanaimba unaweza kuchukulia kirahisi rahisi sana ukasema wanacheza tu, wanajifurahisha..lakini rohoni wanaonekana wanasifu katika ukamilifu wote, na hivyo wanasababisha madhara makubwa sana, hata kwa upande wa pili.

Ili tuelewe vizuri embu tujifunze kisa kimoja, kilichotokea Yerusalemu kipindi kile Bwana Yesu, anaingia akiwa amepanda punda na mwanapunda..Biblia inasema, watu walimtandikia nguo zao chini, na wengine majani ya mitende, wakaanza kumsifu kwa nguvu, wakisema Hosana hosana, Mwana wa Daudi..

Lakini wakati huo huo kulikuwa na kundi la Watoto linaongozana nao pembeni likiwasikiliza.. linajifunza hizo nyimbo..ndipo tunaona mwishoni kabisa wale watu walipomaliza sifa zao, Bwana Yesu aliingia Hekaluni, Lakini kule hekaluni, Watoto, hawakukaa kimya, wakaanza kutoa walivyovisikia,..wakawa wanakiimba kile wachokisikia kule nje! Hosana hosana, mwana wa Daudi..

Tendo lile likawa bughza kwa maadui wa Kristo, walipokuwa wanawasikia Watoto wakipiga kelele kama nyuki hekaluni, wakiimba walichokuwa wanakisikia, ndipo wakamfuata Kristo, kumuonya.. Lakini tunaona, Bwana hakuwaambia sawa nitawanyamazisha kinyume chake akawapa siri nyingine ambayo walikuwa hawaijui..akawaambia maneno haya.. “HAMKUPATA KUSOMA, KWA VINYWA VYA WATOTO WACHANGA NA WANYONYAO UMEKAMILISHA SIFA”

Mathayo 21:9-10,15-16

 “9 Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.

10 Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?

11 Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya…..

15 Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika,

16 wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?”

Umeona? Kumbe sifa za kweli zimekamilika katika vinywa vya Watoto wachanga, sio ajabu kuona mapepo yale yakilipuka ndani ya wale waandishi na wakuu wa makuhani, na kutaka kumshambulia Yesu kwasababu yao..

Mapepo yaliyokuwa yameigeuza nyumba ya Mungu kuwa pango la wanyang’anyi, sasa yanakutana na waaabuduo halisi wanaomwabudu Mungu katika Roho na kweli wamefika..(watoto)..Ni lazima yataabikie tu..

Lakini Habari hii inatufundisha nini sisi wazazi na walezi?

Kama sifa za kweli zimekamilika katika vinywa vya Watoto wachanga, basi tunapaswa tutumie nguvu nyingi sana kuwafundisha Watoto kumwimbia na kumsifu Mungu,  Ni muhimu sana, kwasababu hizo tu zinatosha kumtikisa shetani na ufalme wake..

Lakini kinyume chake ni kweli, kama mtoto hatoimba nyimbo za Mungu, badala yake amekaririshwa, bongofleva, na manyimbo ya kidunia, tufahamu kuwa sifa hizo pia zinakuwa zimekamilika kwa shetani. Hivyo, shetani anatukuzwa, na ufalme wa Mungu unadidimia.

Inasikitisha leo hii, kuona makundi ya Watoto wengi barabarani wanaimba nyimbo za wasanii wa kidunia, ambazo hata wewe mtu mzima kusikiliza unaziba masikio, mpaka unajiuliza hivi wazazi au walezi wao wapo wapi?

Wazazi wapo buzy na kazi, wapo buzy na biashara, wanachozingatia kwao tu ni elimu za duniani basi..Hayo mengine hawahangahiki nayo, hawajui kuwa mapepo yanapata nafasi katika mahekalu yao( yaani Nyumba zao), kwasababu ya sifa za Watoto wao za kipepo, zinamtukuza Ibilisi mwenyewe..

Ndugu, ukitaka furaha katika nyumba yako, embu wafundishe Watoto wako kuimba mapambio, vichwa vyao vijae sifa na nyimbo, waimbe hizo wakati wote, wachezecheze wakiimba hizo sio bongofleva.. kataa mtoto wako kujifunza, hizo nyimbo, wala usimvumilie unapomwona anaziimba bali mkemee.. sio kila mahali umpeleke mtoto au uende naye, huko atajifunza manyimbo ya ibilisi..

Wakati huu ambao bado ni wachanga, vichwa vyao huwa vinakamata sana upesi, hivyo tumia fursa hiyo, kuwapeleka Watoto, Sunday school, na kwenye mafundisho yao, ili wafunze huko kuimba na kumtukuza Mungu..Amani ije nyumbani kwako.

Bwana atusaidie sana, kuliona hilo.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU WATOTO.

MALEZI YA MTOTO MCHANGA.

KAMA “MAMA” UMEBEBA HATIMA YA MTOTO WAKO WA KIUME.

Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa?

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

UMEITIMIZA HAKI YOTE?

MWANAMKE ULIYEKOMAA KI-UMRI, ITAMBUE HUDUMA YAKO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/07/26/ni-nini-kinatoka-kinywani-mwa-mtoto-wako/