Tufanyaje ili tuonekane tunampenda Mungu?

by Admin | 19 August 2022 08:46 pm08

SWALI: Naomba kufahamu kumpenda Mungu kukoje, Je tufanyeje ili tuonekane tunampenda?


JIBU: Tofauti na sisi tunavyotafsiri upendo, kwamba ni kuonyesha hisia zilizo nzuri kwa mwingine, Kwamfano kuhurumia, kujali, kuthamini, kuhudumia, kusifia, kujitoa n.k.

Lakini kwa Mungu ili tuonekane tunampenda yeye, ni zaidi ya kuonyesha hisia.. Kwani waweza kuwa na hisia nzuri kwa Mungu, mpaka ukatoa machozi, unapotafakari matendo yake makuu, Unapotazama wema wake na fadhili zake, na uumbaji wake wote, vikakufanya ujihisi kumpenda sana Mungu.

Lakini hili mbele za Mungu linaweza lisihesabike, kwasababu si kile Mungu anachotaka kukiona kwetu..

Hivyo ni vizuri kufahamu mambo haya makuu matatu (3), ambayo  ukifanya bidii kuyatenda, bila hata kuonyesha hisia Fulani kubwa,  Mungu atakuona unampenda sana, na matokeo yake atajidhihirisha kwako. Mambo yenyewe ni haya;

1). Zishike amri zake:

Amri zake ni pamoja na kukaa mbali na dhambi, halikadhalika, kupendana sisi kwa sisi.

Biblia inasema..

1Yohana 5:3 “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.

4 Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu”.

Umeona, Bado Bwana Yesu analirudia tena hilo hilo neno katika

Yohana 14:15 Mkinipenda, mtazishika amri zangu.

16 Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;

Na amri yake iliyo kuu aliyotupa, ni kupendana sisi kwa sisi, kama nafsi zetu (Yohana 13:34), na zaidi kuwapenda mpaka wale wanaotuchukia. Tukizingatia hayo mambo mawili, huku tukijilinda na dhambi, kwa maisha ya utakatifu, hiyo ni dalili ya kwanza inayofunua upendo wetu wa kweli kwa Mungu.

2) Uchukie ulimwengu:

Kuupenda ulimwengu kunakwenda kinyume na kumpenda Mungu, biblia inasema hivyo katika;

1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.

Ukisema unampenda Mungu, halafu, bado unapenda fashion, unapenda anasa, unapenda party party, na tafrija tafrija, mipira, muvi muvi kila wakati, miziki ya kidunia, kampani za wenye dhambi, vijiwe vijiwe visivyo na maana.

Basi ufahamu upendo kwa Mungu hautakaa uwepo ndani yako, Biblia inasema hivyo. Jitenge na mambo ya kiulimwengu kwa jinsi uwezavyo, tafuta ndugu katika Bwana ndio wawe watu wako wa karibu, biblia ndio iwe novel yako, nyimbo za sifa ndio ziwe mziki wako, kanisani ndio pawe kijiweni pako. Ukizingatia hayo kwa bidii, basi kidogo kidogo, upendo kwa Mungu usio wa kinafki utaingia ndani yako. Na Mungu atauona.

3) Husisha kila kitu chako chote kwa ajili ya Mungu:

Biblia inasema..

Marko 12:29 “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote”.

Hapo hajasema, “mpende tu Bwana Mungu wako”, halafu basi, bali anasema utampenda kwa mambo yote manne, yaani roho, moyo, mwili na akili.

Mungu hataki kupendwa kwenye roho tu, bali hata kwenye akili zako, na nguvu zako. Ikiwa unafikiria Mungu anataka umtafute tu siku za ibada, umwabudu halafu basi, bado hujakamilisha kumpenda, bali anataka nguvu zako unazokwenda kuzisumbukia huko katika kutanga tanga kwako ziishie kwake, Mali zako, kujitoa kwako katika kuujenga ufalme wa Mungu, na kusambaza habari zake.

Vilevile akili yako yote uitumie kwake, ubuni utafiti ni kwa jinsi gani, unaweza kuifanya kazi ya Mungu iwe bora zaidi, kama vile unavyofikiri kila siku ni jinsi gani unavyoweza kuyafanya maisha yako kuwa bora kwake, sio tu kumwachia mtumishi Fulani,au mchungaji Fulani afanye yeye kila kitu, angali vingine vipo ndani ya uwezo wako wewe.

Kwa kuzingatia mambo hayo matatu, basi utakuwa umempenda Mungu, na yeye atalijua hilo, na matokeo yake ni kujidhihirisha kwako, na kukuhudumia. Huko ndio kumpenda Mungu.

Zaburi 91:14 “Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.

15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;

16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA YOANA NA MANAENI?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/19/tufanyaje-ili-tuonekane-tunampenda-mungu/