Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

by Admin | 26 August 2022 08:46 pm08

JIBU: ‘Bila kazi ya mikono’ maana yake ni kuwa pasipo kisaidizi chochote cha kibinadamu, kwamfano neno hilo utalisoma katika vifungu hivi;

Danieli 2:34 “Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande”.

Huu ni utabiri unaomwelezea Yesu Kristo, jinsi atakavyokuja kuangusha ngome zote za ufalme wa huu ulimwengu, yeye ndio hilo jiwe dogo linalozungumziwa hapo, Na biblia inasema, lilichongwa bila kazi ya mikono maana yake ni kuwa lilijichonga lenyewe kutoka mwambani, lilijimegua lenyewe, likaenda na kuipigia ile sanamu, kufunua kuwa Kristo, hakuletwa na mwanadamu hapa duniani, alizaliwa pasipo baba, halikadhalika atakapokuja kuangusha hizi falme sugu za ulimwengu, hatosaidiwa na mtu, wala hata tegemea msaada wa mtu yeyote yeye mwenyewe ataupiga kwa uweza wake, na wote utaanguka kisha atauweka utawala wake usio na mwisho, ambao utaifunika dunia nzima,

Kufahamu jinsi atakavyojua kuzipiga hizi falme za dunia Soma Ufunuo 19:11-16

“11 Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

15 NA UPANGA MKALI HUTOKA KINYWANI MWAKE ILI AWAPIGE MATAIFA KWA HUO. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA”.

Lakini pia Neno hili, utalisoma katika vifungu vingine, ambavyo vinamwelezea mtawala katili aliyetokea zamani katika ufalme wa Uyunani, aliyeitwa Antiokia Epifane, mtawala huyu alikuwa ni kivuli cha mpinga-Kristo anayekuja, kwani, alikuwa na nguvu nyingi, na kwasababu hiyo akawaua wayahudi wengi, na kama hiyo haitoshi akalitia unajisi hekalu la Mungu, ambalo hata wafalme wengine walikuwa wanaogopa kufanya matendo kama hayo, yeye hakujali hiyo alikuwa anamtukana Mungu wa Israeli hadharani, na kuchukua nguruwe na kuwaingiza hekaluni, lakini biblia inasema alivunjika, bila kazi ya mikono.

Danieli 8:25 “Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono”.

Maana yake ni kuwa, Mungu hatotumia jeshi, au wanadamu, au kitu chochote kijulikanacho kumuua, bali yeye mwenyewe atampiga na kufa ghafla, na ndivyo ilivyokuwa katika historia alipatwa na ugonjwa wa ajabu na ghafla, akafa. Kama alivyokuwa Herode wakati ule alivyoliwa na chango, baada ya kujitukuza kama Mungu. (Matendo 12:23).

Hii ni kufunua nini?

Kazi zote za huu ulimwengu ni mbovu, kama Yesu mwenyewe alivyosema katika Yohana 7:7, na ndio maana atakuja kuziondosha zote.  Falme zote zitaanguka, ustaarabu wote utaondolewa, Yesu atakuja kuweka ustaarabu wake mpya wa amani hapa duniani.

Sasa jiulize, mambo unayoyasumbukia leo hii, kana kwamba ndio uzima wako yatakufaidia nini huko mbeleni? Ishi ndani ya Kristo kama mpitaji na msafiri, ukijua kuwa huna makazi ya kudumu hapa, tumia nguvu zako, kuwekeza katika ufalme ujao udumuo, hata kwa hicho unachokisumbukia.

Kumbuka mambo haya yapo karibuni kutokea, huwenda hata ndani ya kizazi chetu, tukayashuhudia haya yote.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

DANIELI: Mlango wa 8

Je Elisha alimdanganya Ben-hadadi kuwa hatakufa kwa ugonjwa wake?

Wakati wakina Shadraka wanatupwa katika tanuru la moto, Danieli alikuwa wapi?

DANIELI: Mlango wa 2

Je mama mjamzito anaruhusiwa kufunga?

UTAKAPOKUWA MZEE, UTAINYOSHA MIKONO YAKO. NA MWINGINE ATAKUFUNGA

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

YOTE NAMTOLEA YESU_Tenzi za Rohoni.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/26/bila-kazi-ya-mikono/