KUWA MWOMBOLEZAJI.

by Admin | 30 August 2022 08:46 am08

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WANAWAKE.

Kuwa mwombolezaji:

Yeremia 9:20 “Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia”.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu, mkuu wa uzima, karibu katika kujifunza maneno ya uzima. Huu ni mwendelezo wa mafundisho maalumu yawahusuyo wanawake.

Leo nataka tuone jambo ya kitofauti lililokuwa linawatokea wanawake wengi wa-Kimungu katika biblia. Na kwa kupitia hilo naamini lipo la kujifunza wewe kama mwanamke, uliyeokoka.

Na jambo yenyewe ni “kufungwa Tumbo la uzazi”. Ukisoma kuanzia mwanzo, wanawake wengi hodari walioitwa wacha Mungu, walifungwa matumbo yao wasiweze kuzaa, tukianzia kwa Sara, mpaka Rebeka, tukiendelea hadi kwa Raheli, na Ana-Mama yake Samweli, na  Mke wa Manoa aliyemzaa Samsoni, na  Elizabeti mama yake Yohana. Wote hawa walikuwa ni matasa. Unajua ni kwanini?

Wengi wanachukulia katika jicho la laana na mikosi, lakini ukitafakari vizuri, hakukuwa na laana yoyote juu ya watu hawa, kwasababu maandiko yanatuambia ni Mungu mwenyewe ndio aliyewafunga matumbo yao, Tengeneza picha Sara ambaye wafalme waliojaribu kumuiba wamfanye mke wao, Bwana aliwaadhibu vikali, mtu kama huyo iweje awe amebeba laana?

Hivyo lipo funzo kubwa sana nyuma yake, linalowahusu wanawake wote. Na funzo lenyewe ni kwamba Mungu anataka mwanamke yeyote, awe mwombolezaji, ili kusudi lake litimie, aulekeze moyo wake kwake kwa machozi mengi na dua, maombi, kwasababu kwa kupitia yeye, Mungu atalifanikisha kusudi  lake kubwa duniani.  Na ndio maana ilimgharimu Mungu awafunge matumbo wale wanawake wote, ambao alijua kabisa kwa kupitia wazao wao, Mungu atatukuzwa.

Ndio hapo utamwona mwanamke kama Ana, mke wa Elkana analia kama mlevi kule hekaluni, juu ya uzazi wake, yeye akidhani kwamba Mungu anasikiliza dua za tumbo lake, kumbe Mungu alikuwa anasikiliza maombi ya kuletwa mwamuzi  Samweli duniani… Kwasababu ili shujaa aje ilihitaji maombolezo mengi sana.

 Lakini kama moyo wake ungelitambua hilo tangu mwanzo, kuomba kwa bidii juu ya mwamuzi Israeli, kulikuwa hakuna sababu ya yeye kufungwa tumbo. Yanini?

Ndivyo ilivyokuwa kwa Raheli na Elizabeti, na wanawake wengine.

Binti, dada, Mama, bibi.. Tambua kuwa wewe umewekwa, kama  mzalisha Nuru ulimwenguni. Maombi yako, machozi yako, sala zako, maombolezo yako, ni changizo kubwa sana la Mungu kuleta mapinduzi katika kanisa, familia, na hata taifa kwa ujumla.

Usisubiri Mungu akufunge tumbo lako, ndipo uanze kulia, na kuomboleza,. Bali jitambue sasa, Kumbuka Tumbo, linaweza kuwa pia kazi yako, au  afya yako n.k ukiona hicho ndicho kinachokukosesha raha sasa, na umekiombea kwa muda mrefu bila mafanikio, basi tambua umefungwa hivyo na Mungu makusudi, ili uuelekeze moyo wako kwake.

Sasa hapo usiombe Mungu akupe mtoto au akupe kazi au akuponye huo ugonjwa, au akukombe kiuchumi, hapana omba Mungu, alete geuko kwa kanisa, kwa familia yako, kwa taifa, kwa kupitia wewe, ombea sana rehema na toba. Na hayo yaliyosalia Mungu alishakujibu siku nyingi yeye mwenyewe alishayatimiza. Kutokukujibu kwake haraka sio kwamba akutese hapana, machozi yako kwake hayajatosha, na umeyaelekeza pasipostahili.

Mwanamke usipokuwa mwombolezaji, fahamu kuwa unalididimiza kanisa, usipokuwa mwombaji, unalidhoofisha kanisa la Kristo kwelikweli. Tambua huduma hii, ili Kanisa liweze kusimama vema, wachungaji waweze kuhubiri, vipawa na karama vinyanyuke kwenye kanisa hadi kwenye familia, wewe ndio unayeweza kufungua milango hiyo.

Bwana atusaidie kujua hilo;

Yeremia 9:17 “Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje; 18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.

19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.

20 Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia.

21 Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO KWA WANAWAKE.

NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO.

Katika (Mathayo 25:8 na Marko 16:8) Wale wanawake walitangaza kufufuka kwa Bwana au walikaa kimya?

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 3)

Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.

Shetri ni nini kama tunavyosoma katika Marko 3:38?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/08/30/kuwa-mwombolezaji/