by Admin | 6 September 2022 08:46 pm09
Bwana Yesu asifiwe, karibu tena tujifunze maneno ya uzima. Leo nataka tuone jambo ambalo, wengi wetu tuliookoka hatulifahamu kuhusiana na tabia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
Ili tuelewe vema kiini cha somo, naomba tusome hivi vifungu vitatu, kwa umakini sana;
Marko 2:1
Akaingia Kapernaumu tena, baada ya siku kadha wa kadha, ikasikiwa ya kwamba yumo nyumbani.
Mathayo 13:1 “Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.
2 Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani”.
Mathayo 14:13 “Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao.
14 Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao”.
Kama tunavyosoma hapo, kuna wakati Bwana Yesu alikaa nyumbani kwake, mahali ambapo panajulikana, kwamfano kama mtu angemuulizia angeambiwa anakaa pale kwenye kaya ile namba Fulani..Utamkuta ameketi kwenye kochi lake, sebuleni kwake, au yupo jikoni kwake anajipikia chai, atakukaribisha na mtazungumza mengi tu.
Soma,
Yohan1:37 “Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.
38 Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?
39 Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi”.
Lakini upo wakati aliondoka hapo, akaenda katika mazingira ambayo yana watu, lakini hayana nyumba ndio hapo unamwona anatoka nyumbani kwake anakwenda kuketi kando ya bahari.. Sasa kumpata hapa, si kurahisi kama ilivyokuwa nyumbani, Leo hii ni rahisi mtu kukwambia tuonane hoteli Fulani, au nyumba Fulani, kuliko kukwambia tuonane fukweni, wavuvi walipo. Ni ngumu kwasababu hakuna ofisi au makazi pale.
Lakini kama hiyo haitoshi, aliondoka tena huko fukweni ambapo alikuwa anakwenda mara kwa mara kuwafundisha watu, akakaa sehemu isiyokuwa na watu kabisa, maana yake nyikani/ jangwani. Huku ndiko kubaya kabisa, kwasababu hakuna upatikanaji wa mahitaji yoyote ya kijamii. Hakuna maji wala chakula, wala kivuli, ni jua tu, na vumbi..
Lakini katika sehemu zote hizi, watu waliokuwa na shida kwelikweli walimfuata, isipokuwa ni kwa ugumu sana, kwasababu iliwabidi watembee kwa miguu umbali mrefu, kama tunavyosoma hapo juu, waende mahali ambapo hawajui kama watarudi salama, au mizoga.
Na ndio maana kule nyikani, ilifikia hatua wanawafunzi wake wakamwambia Bwana awaage makutano, waende kujitafutia chakula kwasababu wamekaa naye siku tatu, usiku na mchana, bila chochote, watazimia,…Lakini Yesu alijua ni nini anakitengeneza ndani yao.
Mathayo 14:15 “Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula”.
Ndugu yangu, pindi unapookoka, ni sawa na ile hatua ya kwanza ya Yesu kukaa nyumbani kwake. Wakati huu Kristo anakuwa karibu sana na wewe, mda wowote utampata, itakuwa ni rahisi yeye kuchukuliana na wewe kwa hali zako zote.. Lakini jambo hilo halitaendelea sana..
Ataondoka nyumbani kwake na kwenda ufukweni.. Hapo ndipo itabidi umfuate. Ukikaa katika mazingira yale yale, miezi inaenda miezi inarudi, huonyeshi bidii yoyote kwa Kristo, wewe mwenyewe utashuhudia tu ukame utakaouna moyoni mwako. Utadhani kwamba Kristo amekuacha, kwasababu ile raha uliyokuwa mwanzo, au vile vitu alivyokuwa anakuonyesha mwanzo vimekata. Ukishaona hivyo, hapo ndipo unapaswa ujiongeze, zidisha bidii yako, kufanya ibada, kuomba, kusoma Neno na kujitenga na uovu. Ukizingatia hayo, utaanza kumwona tena akikufundisha..
Lakini hapo napo hatadumu kwa muda mrefu sana kama unavyodhani.. Atapiga hatua nyingine na kwenda nyikani, pasipokuwa na kitu/watu. Na huko nako huna budi kumfuata.. Hapo ndipo inapokugharimu, kuuaga ulimwengu, inapokugharimu, kupoteza nafsi yako kwa ajili yake,. Unamfuata Yesu hujui kesho yako utakula nini, hujui hatma ya maisha yako itakuwaje, unakubali kupukutika naye pale nyikani, huku ukimsikiliza tu,
Wakati huu usijijali sana, ikiwa unahaja kweli na Yesu.. Kwasababu hatua hii ya kujikana nafsi, inafikiwa na wachache, lakini huku ndipo Kristo anajifunua kwa mtu kwa viwango vingine kabisa. Utaona wale makutano walioweza kustahimili naye, siku tatu kule nyikani, bila kitu chochote, walipata faida mbili, ya kwanza ni kupokea uzima wa milele, na ya pili, ni kugawanyiwa mikate, ambayo waliila na kusaza. Sasa mikate pale inafunua, [rizki zao], maana yake ni kuwa Kristo aliwabariki, rizki zao, kule waliporudi, walipata vingi, kupita kiasi mpaka wakasaza, Kama kulikuwa na muuza genge alipata wateja mara mbili zaidi n.k..yaani kwa ufupi uchumi wao ulirekebishwa na Bwana.(Mathayo 14:19-21)
Lakini hiyo yote ilitokana na nini?
Ni kuwa radhi, kujitwika msalaba wako na kumfata Yesu. Hili haliepukiki kwa mtu yeyote anayemaanisha kumfuata Bwana Yesu. Ikiwa hauwi tayari binti kutupa vimini na suruali, na maurembo ya kidunia, kuukana ulimwengu kweli kweli, huwezi kumwona Bwana katika viwango vingine, ikiwa kijana, upo nusu nusu, vuguvugu, mizaha, na matusi, miziki ya kidunia, kubeti, mipira, punyeto, pamoja na udunia vimekutawala, hapo usiseme nimemwona Bwana.
Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.
35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.
36 Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?”
Tukizijua tabia hizi za Bwana Yesu, basi tutajifunza kuwa watu wa kupiga hatua kila siku, kumfikia yeye. Kwasababu Bwana hayupo sehemu moja. Tukatae ukristo mgando.
Bwana atusaidie.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KUNA WAKATI YESU ATAPITA NA WATU HAWATAJUA.
JE UPANGA UMEINGIA MOYONI MWAKO?.
LEO WOKOVU UMEFIKA NYUMBANI HUMU
Je! ni sahihi kuning’iniza picha nyumbani mwako kama ya Yesu?
“Bonde la vilio” ni nini katika biblia?(Zaburi 84:6)
Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/09/06/yesu-hayupo-katika-mazingira-yaleyale-tu-sikuzote-usijisahau/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.