KAZI YA MALAIKA MIKAELI KWA WATU WA MUNGU.

by Admin | 1 November 2022 08:46 pm11

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe, karibu tuongeze maarifa ya Neno la Mungu.

Leo tutajifunza juu ya Malaika Mikaeli.

Mbinguni kuna aina kuu tatu za Malaika. Wapo malaika wa sifa ambao ndio wale Maserafi na Makerubi, pia wapo malaika wa Ujumbe ambaye ndio kundi la Gabrieli (aliyemletea Mariamu taarifa za kumzaa Bwana Yesu na pia aliyemletea ujumbe Danieli)

Pia wapo malaika wa Vita, ambao kazi yao ni kupambana na nguvu zote za adui zinazoshindana na watu wa Mungu, na hapa ndipo kundi la Mikaeli na wenzake linapotokea.

Sasa inaaminika na baadhi ya watu kuwa Mikaeli ni jina lingine linalomwakilisha Bwana Yesu..lakini kulingana na maandiko hilo jambo si kweli..

Sasa ni kwa namna gani Mikaeli sio Bwana Yesu kulingana na maandiko unaweza kufungua hapa na kusoma >>>Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?

Sasa maswali mawili ya kujiuliza ni je Mikaeli anampigania nani, na anapiganaje?

1. Anampigania nani?

Mikaeli ni malaika wa vita aliyewekwa na Mungu kulipigania Taifa la Israeli na kanisa la Mungu.

Tunalithibitisha hilo kipindi kile ambacho Danieli analetewa ujumbe na Malaika Gabrieli, na kumtaja Mikaeli kuwa amewekwa kusimama upande watu wa Danieli (yaani waisraeli)”.

Danieli12:1 “Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako…”

Pia unaweza kusoma Danieli 10:21,utaona Mikaeli anatajwa kama Mkuu wa watu wa Danieli

Hivyo Mikaeli ni malaika wa vita kwa ajili ya Taifa la Israeli kwa jinsi ya mwili, na Israeli ya roho ambayo ni kanisa (yaani sisi tuliompokea Yesu).

2. Mikaeli anapiganaje?

Vita vya Mikaeli dhidi ya roho zitufuatiliazo si za kurusha mikuki au mapanga..bali ni za hoja.

Maandiko yanasema shetani anatushitaki usiku na mchana mbele za Mungu (Ufunuo 12:10)..na zaidi sana tafsiri ya jina shetani ni “mshitaki / mchongezi”..hiyo ndio tafsiri ya jina shetani.

Kwahiyo shetani anachokifanya usiku na mchana na kuchukua taarifa zetu mbaya na kuzifikisha mbele za Mungu kama mashitaka, hata kama hataona dosari katika maisha yetu bado tu atafika Kwa Mungu kutuchongea kama alivyofanya kwa Ayubu.

Lakini sasa Mikaeli pamoja na wenzake wanachokifanya ni kupeleka hoja zetu nzuri mbele za Mungu, kamwe hawapeleki mashitaka..Na hoja za Mikaeli zikishinda dhidi ya hoja za shetani juu yetu ndipo hapo tunapata yale yote tuliyomwomba Mungu.

Lakini hoja za shetani zikishinda dhidi ya zile za Mikaeli bali tunakabidhiwa shetani, na hivyo tunawekwa katika mikono ya shetani na kupata madhara…kwasababu Mungu ni Mungu wa haki na hana upendeleo!…Ndio maana Adamu alipoasi Mungu hakumpendelea Adamu na bali aliruhusu shetani ayachukue mamlaka yake, kwasababu ni kweli kayapata kihalali kutoka kwa Adamu.

Kwahiyo vita kati ya shetani na malaika watakatifu si vingine zaidi ya hivyo vya hoja, kila upande unapamba kuvuna watu.

Tunaweza kupata picha zaidi tunaposoma ufunuo alioonyeshwa Yuda ambao alioonyesha kuhusu mwili wa Musa.

Yuda (sio yule aliyemsaliti Bwana) alifunuliwa katika roho jambo ambalo shetani alikuwa analifanya baada tu ya Musa kufa.

Alionyeshwa baada ya Musa kufa kumbe shetani alimfuata Mungu na kuutaka mwili wake, na lengo la kuutaka mwili wake ni wazi kuwa si lingine zaidi ya kutaka kuuweka uabudiwe na watu.

Na alipofika mbele za Mungu, alikuwa na hoja kwanini anautaka ule mwili, na pengine hoja ambayo alikuwa nayo ni lile kosa Musa alilolifanya lililompelekea yeye kufa (la kutompa Mungu utukufu).

Hivyo shetani alikuwa na kila sababu za yeye kuumiliki mwili wa Musa, lakini tunaona kitu cha kipekee ni kwamba wakati anapeleka hayo mashitaka Mikaeli aliyewekwa kwaajili ya kuwatetea Israeli alisimama kumpinga hoja zake hizo, na Mikaeli akatoa hoja zenye nguvu juu ya Musa, na hivyo Mikaeli akashinda na shetani hakukabidhiwa mwili wa Musa, ndio maana mpaka leo hakuna mtu anajua mifupa ya Musa ilipo.(Ni Mungu mwenyewe ndiye  aliyemzika).

Lakini endapo shetani angeshinda hoja mbele ya Mikaeli basi huenda Musa angekufa hemani na watu wangeikusanya mifupa yake na kuiabudu na ufalme wa giza ungestawi zaidi.

Yuda 1:9 “Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee”.

Ndugu mpendwa Ikiwa unasema umeshampokea Yesu halafu bado unafanya uzinzi, basi fahamu kuwa shetani anapeleka mashaka hayo mbele za Mungu mchana na usiku…akidai haki ya kukumiliki wewe.

Lakini matendo yako yakiwa sawasawa na biblia, basi shetani anakosa alama za kukushitaki mbele za Mungu, na kinyume chake Malaika wa Bwana, Mikaeli na kundi lake wanasimama kuyataja mambo yako mazuri mbele za Mungu, wanautazama uso wa Baba na kutaja mema yako kama maandiko yasemavyo..

Mathayo 18:10 “Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni”

Na kamwe malaika hawapeleki mashtaka mabaya mbele za Mungu kwaajili yetu.

2 Petro 2:11 “Wenye ushupavu, wenye kujikinai, hawatetemeki wakiyatukana matukufu; ijapokuwa malaika ambao ni wakuu zaidi kwa uwezo na nguvu, hawaleti mashitaka mabaya juu yao mbele za Bwana”.

Je umetubu kwa kumaanisha kuacha dhambi?..umeacha wizi?, umeacha usengenyaji?, umeacha ulevi, umeacha uasherati?, umeacha uuaji na hasira?.

Kama bado hujaacha hivyo vyote basi fahamu kuwa ndivyo vinavyokushitaki mbele za Mungu.

Marana tha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?

AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!

Je Musa yupo anawashitaki watu..kulingana na Yohana 5:45?

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

UFUNUO: Mlango wa 14

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/01/kazi-ya-malaika-mikaeli-kwa-watu-wa-mungu/