by Admin | 1 November 2022 08:46 pm11
Mtu yeyote aliyeokoka (Kwa kumaanisha kabisa), ni lazima Bwana ataweka huduma ndani yake, anaweza akawa mchungaji, au mwinjilisti, au mwalimu, au mwimbaji, shemasi, lakini pia anaweza akawa mwandishi, mtunza bustani, mratibu wa vipindi, mwasibu wa kanisa, n.k. maadamu tu zinafanya kazi ya kulihudumia kanisa la Mungu, na si vinginevyo.
Licha ya kuwa utaifurahia kazi yako na kupata thawabu, lakini uhalisia wake ni kwamba, huduma yoyote Mungu anayokupa haitakuwa nyepesi kama wewe unavyoweza kudhani, yaliyowakuta mitume wakati fulani, yatakukuta na wewe, lakini yatamkuta hata na Yule ambaye atakuja kutumika baadaye.
Haya ni baadhi ya maumivu utakayokutana nayo;
2Timotheo 4:10 “Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia”
Tengeneza picha, Wakati ambapo mtume Paulo yupo katika kilele cha utumishi, halafu mtendakazi mwenzake mpendwa, anageuka ghafla, na kumwachwa alijisikiaje. Ni heri angemwacha na kwenda kutumika mahali pengine, lakini anamwacha na kuurudia ulimwengu. Ni maumivu makali kiasi gani? Ni kuvunjwa moyo kiasi gani?
Mwaka 2016-2018, tulikuwa na rafiki yetu mmoja, hatukudhani kama siku moja tungekaa tutengane, kwasababu tulikuwa tumeshajiwekea malengo mengi makubwa ya kumtumikia Mungu, tuliishi kama Daudi na Yonathani, lakini tulipoanza kupiga hatua tu ya kutekeleza malengo yetu, ghafla alikatisha mawasiliano na sisi, akawa hapokei simu zetu, na baadaye kutu-block kabisa, akaurudia ulimwengu, hadi leo.
Tuyahifadhi haya ili yatakapotokea tusivunjike moyo tukaacha utumishi. Wakina Dema unaweza kupishana nao katika huduma Mungu aliyoweka ndani yako, ila usivunjike moyo.
Pale pale Mtume Paulo anamsihi Timotheo asikawie kumfuata, kwasababu Kreske, amekwenda Galatia, Tito, Dalmatia..
2Timotheo 4:9 “Jitahidi kuja kwangu upesi. 10 Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia. 11 Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi. 12 Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso.
Kundi hili halikuondoka, kwasababu ya kuupenda ulimwengu kama Dema, hapana bali kwasababu ya huduma, hivyo mtume Paulo akabaki peke yake. Kuna wakati alikuwa na kundi kubwa la watenda kazi pamoja naye, lakini upo wakati alibaki peke na Luka tu.. Anamhizi Timotheo afike pamoja na Marko, ili afarijike katika huduma, hali ya upweke imwache.
Kama mhudumu wa Kristo, zipo nyakati utakuwa peke yako, Hivyo usife moyo, ni vipindi tu vya Muda.
Moja ya ziara za mtume Paulo iliyokuwa na mafanikio makubwa sana, basi ni ile ziara ya kwanza. Ni kwasababu gani? Ni kwasababu alikuwa na Barnaba. Wote wawili walikuwa na nia ya Kristo, hawakuwa na fikra za kiulimwengu au kimaisha. Lakini cha kusikitisha hilo halikuendelea sana.. Walipishana kauli, kutokana na kwamba kila mmoja aliona uchaguzi wake ni bora kuliko wa mwingine.. Paulo alitaka kwenda Sila, lakini Barnaba kwenda na Marko. Lakini kama wangetoa tofauti zao, na kuwachukua wote, naamini huduma ingekuwa na mafanikio makubwa zaidi, lakini hilo lilikuwa halina budi kutokea.
Matendo 15:36 “ Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.
37 Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.
38 Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.
39 Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro”.
Nyakati za kupoteza kiungo chako muhimu katika huduma utapishana nacho.
2Timotheo 4:13 “Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi. 14 Iskanda, mfua shaba, alionyesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake. 15 Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu”.
Haijalishi, utampendeza mtu kiasi gani, utafanya wema mwingi namna gani, bado wapo watakaokupinga tu utumishi wako, na zaidi watakuwa ni kama maadui zako. Ni jambo ambalo mtume Paulo hakulitarajia lakini alikumbana nalo baadaye, kutoka kwa Iskanda.. Yaliyomkuta Kristo Bwana wetu kutoka kwa mafarisayo yakamakuta na yeye. Na huwenda yatakukuta na wewe wakati Fulani mbele. Usirudi nyuma.
Watu wengi wanaweza kuchukizwa na wewe kwasababu matarajio yao kwako ni tofauti na walivyokutegemea, hili lilianza tangu wakati wa Bwana alipokuwa duniani. Watu wengi waliosikia habari zake, ikiwemo Yohana mbatizaji, walimtazamia Bwana angekuja kama mfalme Daudi, akipambana na utawala sugu wa kirumi, akivaa nguo za kifalme, akiogopwa na kila mtu. Lakini aliposikia analala kwenye milima ya mizeituni, anaongozana na wavuvi, anakaa na wenye dhambi..Imani ya Yohana ikatetereka kidogo na kutuma watu ili kuulizia kama yeye kweli ndiye, au wamtazamie mwingine..Lakini maneno ya Bwana Yesu yalikuwa ni haya;
“Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami” (Mathayo 11:6).
Vivyo hivyo na mtume Paulo, alitarajiwa na wengi kuwa atakuwa ni mtu mkuu kimwonekano, mwenye mavazi ya kikuhani kama waandishi, kutoka na sifa zake, na nyaraka zake, kuvuma duniani kote..lakini walipokutana naye walimwona kama kituko Fulani hivi;
2Wakorintho 10:10 “Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu.
11 Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo”
Hivyo si kila mtu atapendezwa na jinsi atakavyokukuta, wengine watakuacha au hawatakuamini kwasababu umekuja nje ya matarajio yao.
Japokuwa vipo vipindi vyingi vya mafanikio, lakini pia vipo vipindi vya kupungukiwa kabisa. Paulo anamwagiza Timotheo pindi amfuatapo makedonia ambebe joho(Koti) lake, kwa ajili ya ule wakati wa baridi. Kama angekuwa na fedha ya kutosha wakati huo, kulikuwa hakuna haja ya kumwagiza, angenunua lingine tu alipokuwepo.
Mungu hawezi kukuacha, wala kukupungukia kabisa, atakupa, na kukufanikisha, lakini pia vipindi kama hivi utapishana navyo mara kwa mara na ni Mungu mwenyewe anaruhusu. Hivyo usitetereke.
Wafilipi 4:11 “Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.
12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa. 13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”
Ukiwa mtumishi, haimaanishi wewe ni malaika, umejitenga na mateso ya hii dunia, Kazi hii itakufanya uumwe wakati mwingine, Timotheo alikuwa anaumwa mara kwa mara tumbo, kwasababu ya mifungo, kuhubiri sana, hivyo akashauriwa na Paulo atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya kuweka tumbo lake sawa. Alikuwepo Epafrodito mtume, naye kwasababu ya injili, aliumwa sana, karibu na kufa lakini baadaye Bwana akamponya( Wafilipi 2:25). Elisha alikufa na ugonjwa wake.
Upitiapo vipindi vya magonjwa, usitetereke ukaacha utumishi bali jifariji kwa kupitia mashujaa hawa.
Hivyo, tukiyahifadhi haya moyoni, basi utumishi wetu hautakuwa wa manung’uniko au wa kuvunjika moyo, mara kwa mara. Kwasababu ndio njia ya wote. Hivyo tukaze mwendo katika kumtumikia Bwana, kwasababu malipo yake ni makubwa kuliko mateso tunayopishana nayo. Thawabu za utumishi ni nyingi sana,
Ufunuo 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.
Je Musa yupo anawashitaki watu..kulingana na Yohana 5:45?
Tofauti kati ya mtume na mwanafunzi ni ipi kibiblia?
Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma.
Je mbinguni itakuwa ni kuimba tu wakati wote?
MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.
KAMA MHUBIRI USIWE MFANO WA DIOTREFE.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/11/01/maumivu-nyuma-ya-huduma/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.