KAMA MHUBIRI USIWE MFANO WA DIOTREFE.

KAMA MHUBIRI USIWE MFANO WA DIOTREFE.

Je! Unamjua Diotrefe katika biblia?

Diotrefe alikuwa ni kiongozi katika kanisa moja ambalo mtu wa Mungu ,Gayo alikuwa akishiriki. Kiongozi huyu alianza vizuri na Bwana lakini mwisho wake ulikuwa mbaya.. mpaka Mtume Yohana anamwandikia Gayo waraka juu yake,  ili asiziige tabia zake..

Hebu tumsome huyu Diotrefe jinsi alivyokuwa na tabia zake..

3Yohana 1:8 “Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.

9  Naliliandikia kanisa neno, lakini Diotrefe, apendaye kuwa wa kwanza kati yao, hatukubali.

10  Kwa hiyo, nikija, nitayakumbuka matendo yake atendayo, atoavyo upuzi juu yetu kwa maneno maovu; wala hatoshwi na hayo, ila yeye mwenyewe hawakaribishi hao ndugu, na wale watakao kuwakaribisha, huwazuia, na kuwatoa katika kanisa”.

Sasa hebu tuzitazame hizi tabia 4 Diotrefe alizokuwa nazo.

1: ANAPENDA KUWA WA KWANZA:

 Hii ni tabia ya kwanza Diotrefe aliyokuwa nayo;  Sasa Kupenda kuwa wa kwanza si jambo baya, lakini mtu anapotaka kuwa wa kwanza kwa lengo la kutukuzwa na watu, au kwa lengo la kuwatawala wa wengine, au kwa lengo la kutumikiwa.. hususani ndani ya kanisa, basi hiyo ni mbaya sana na ni kinyume na Neno la Mungu..

Kwasababu Bwana Yesu alisema..

Mathayo 20:25  “Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.

26  LAKINI HAITAKUWA HIVYO KWENU; BALI MTU YE YOTE ANAYETAKA KUWA MKUBWA KWENU, NA AWE MTUMISHI WENU;

27  NA MTU YE YOTE ANAYETAKA KUWA WA KWANZA KWENU NA AWE MTUMWA WENU;

28  kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi”.

Kwahiyo kama Mhubiri wa Injili: Katika nafasi yoyote uliyopo aidha ni Mchungaji, au Mwalimu, au Nabii, au Mtume au Mwimbaji kumbuka kuwa unapaswa uwe Mtumwa wa wote!, kama unataka kuwa wa Kwanza, lakini kamwe usijiinue wala usitafute utukufu wa wanadamu kama huyu Diotrefe. Ni hatari kubwa!

2. ANANENA MANENO YA UPUUZI  JUU YA MITUME

Hii ni tabia ya pili Diotrefe aliyokuwa nayo.. Alikuwa anawachafua Mitume wa Bwana Yesu (Ikiwemo Yohana, Mtume wa Yesu ambaye alipendwa sana na Bwana Yesu). Ijapokuwa aliwajua kuwa wamechaguliwa na Bwana lakini yeye aliwachafua kwa maneno mabaya na kuwafanya waonekane si kitu mbele ya kanisa la Mungu…Na hiyo yote ni kutokana na wivu.

Roho hii pia ipo kwa baadhi ya watu, ambao kutokana na Wivu, basi wapo radhi hata kuwachafua watumishi wa kweli wa Mungu, na huku mioyoni wakishuhudiwa kuwa wanawachafua ni watumishi wa kweli wa Mungu, lakini kutokana na wivu wanaendelea tu kuwachafua!,.. Hili ni jambo la kuzingatia sana  wewe kama Mwimbaji, au Mchungaji, au Mtume au Nabii au Mwinjilisti.

3. HAWAKARIBISHI NDUGU

Hii ni tabia ya tatu ambayo Diotrefe alikuwa anaionyesha katika kanisa… Yeye alikuwa ni kiongozi lakini kamwe hakutaka kupokea Watumishi wengine waliokuja kuhubiri katika mitaa yake, au mji wake, au waliokuwa wakipita njia yake kuelekea sehemu nyingine kuhubiri. Na sababu ya kufanya hivyo ni ile ile ya wivu na kutaka kuwa wa kwanza..

 Aliona kama mtu mwingine akija kuhubiri katika mji wake basi yeye hadhi yake, au heshima yake itashuka, na Yule alitakayekuja atatukuzwa zaidi..Hivyo hiyo roho ikampelekea mpaka kukataa kupokea wahubiri walio wageni.

Vile vile na sisi hatuna budi kuikataa hiyo roho kwasababu ni roho kutoka kwa Yule adui, siku zote hatuna budi kuwakubali na kuwakaribisha Watumishi wengine wanaotaka kuja kuhubiri maeneo tuliyopo, maadamu tumewahakiki kuwa kweli ni watumishi wa Mungu kwa Neno la Mungu, na wamekuja kwa nia ya kuhubiri injili.

4. ALIWAZUIA WATU WENGINE WASIWAKARIBISHE NDUGU

Hii ni tabia ya mwisho aliyoionyesha huyu Diotrefe.. Hakuridhika tu kuwakataa Mitume waliokuja kuhubiri pande zake, bali pia aliwakataza washirika wa kanisa lile wasimpokee mtumishi mwingine yoyote atakayekuja kuomba hifadhi kwao, kwaajili ya kuhubiri injili.. Na hakuishia hapo, bali aliendelea na kuwafukuza katika kanisa wale wote waliodhubutu kuwakaribisha Mitume. (Uone jinsi hii roho ilivyoenda mbali).

Lakini huyu Diotrefe hakuanza hivi.. Alianza vizuri tu!, ndio maana hata akafikia hatua ya kuwa kiongozi wa Makanisa (Huenda alikuwa Askofu).  Lakini roho nyingine ya kujiinua ilimwingia na ya kupenda kutukuzwa na watu na kuinuliwa, na akaipalilia mwishowe ikawa ni roho ya uadui mbaya sana na iliyoiharibu kanisa.

Na sisi hatuna budi kujifunza katika haya, ili tusijikute tunaangukia katika makosa hayo hayo ya Diotrefe (Ndio maana Mungu karuhusu kisa cha Diotrefe kiwepo katika biblia hata kama kwa ufupi sana). Ili tujifunze na tujihadhari na roho ya kujiinua, na kupenda utukufu wa wanadamu zaidi ya utukufu wa Mungu, na tama nyingine zote za kiulimwengu.

Bwana atusaidie tuwe kama Mzee Gayo aliyekubali kupokea mashauri hayo.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.

Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments