USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU UKAE NANYI NYOTE.

by Admin | 5 December 2022 08:46 pm12

Je! Unataka Roho Mtakatifu afanye kazi vizuri ndani yako?

Fuatilia somo hili.

Maandiko yanasema..

2Wakorintho 13:14  “Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote”

Unaweza kujiuliza ni kwanini, ofisi hizo kuu tatu za Mungu, zitajwe na sifa zao? Na si zenyewe tu kama zilivyo, (yaana Mungu, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu).. Bali kila mmoja inaelezewa na sifa yake pembeni, yaani ‘Pendo’ la Mungu, na ‘Neema’ya Yesu Kristo, na ‘Ushirika’ wa Roho Mtakatifu? Kwanini iwe hivyo?

Ni kwasababu Mungu anataka tujue kwa ukaribu tabia kuu iliyotenda kazi katika kila ofisi,

Kwamfano Anaposema Pendo la Mungu…Maana yake ni kuwa Palipo na upendo, Mungu yupo, hivyo kazi zote za Mungu(Baba), zinadhihirika kwa upesi sana pale ambapo pana upendo kwasababu maandiko yanasema kuwa yeye ni upendo..

Ukitaka umuone Mungu kama baba yako, basi hauna budi kuwapenda watu kwa moyo.

1Yohana 4:16  “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake”.

Usipopenda maana yake ni kuwa Mungu(kama Baba), kamwe hatakaa ajidhihirishe kwako.

1Yohana 4:20  “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona”

Halidhalika, maandiko yanasema.. “Neema ya Bwana Yesu Kristo, ikae nanyi nyote”. Ikiwa na maana kuwa Kristo yupo katika neema. Neema ni ile hali ya kutoa kitu ambacho mtu hajastahili kukipata. Kwamfano mtu anayefaulishwa, kwa kuhurumiwa na wakati hakusoma..Hiyo inatafsirika kama neema, ndicho Yesu alichokifanya sana akiwa duniani..

Kwanza aliacha enzi na mamlaka na uweza kule mbinguni, akaja duniani, ili kutupa sisi wokovu bure, bila kuusumbukia, akamwaga damu yake ili sisi tupate ondoleo la dhambi. Tukahesabiwa kuwa tumestahili uzima wa milele bure bila matendo. Kwaufupi Maisha yake yote yalikuwa yamejaa neema! neema! tu

Hivyo Kristo naye ili atembee na sisi, ni lazima nasi tuwe watu waliojaa neema kwa wengine.. Ndio maana akasema, ndugu yako akikukosa hata 7 mara 70, huna budi kumsamehe. Vilevile tujifunze kuachilia, na kutokuhukumu. Hivyo tukitaka tutembee kama Kristo duniani, basi tabia hii ni lazima tuwe nayo kwa wingi.

Lakini Pia maandiko yanasema..

‘Ushirika’ wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote” ..

Maana yake ni kuwa utendaji kazi mkuu wa  Roho Mtakatifu, upo katika ushirika.. Neno ushirika, limetokana na neno ushirikiano.  Anachotaka kwanza ni ushirikiano wetu sisi na Mungu, lakini zaidi sana ushirikiano wetu sisi kwa sisi (tuliokoka).

Kanisa la sasa tunakosa kuona nguvu za Roho Mtakatifu kwasasababu hatuna ushirikiano. Kila mmoja anatembea kivyake, kila mmoja ana nia yake, na matazamio yake binafsi. Hivyo basi Roho Mtakatifu anashindwa kufanya kazi kama anavyotaka. Tunamwita Roho Mtakatifu lakini haji kwasababu hatujui kuwa yeye yupo katika ushirikiano.

Siku ile ya Pentekoste, maandiko yanasema, kabla Roho Mtakatifu hajashuka, walikuwa kwanza mahali pamoja wote, wakidumu katika kusali.

Matendo 2:1  “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste WALIKUWAKO WOTE MAHALI PAMOJA. 2  Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.

3  Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4  Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Hata baada ya pale, bado waliendelea kuwa wamoja, na kudumu katika nia moja.(Matendo 5:12)

Hivyo Roho Mtakatifu akatenda kazi sana miongoni mwa watu.

Hata sasa, ukitaka Roho Mtakatifu ajae kwa haraka sana ndani yako usiepuke, kuwepo katika ibada na wenzako, katika mikesha, katika maombi, katika ushirikia wowote mwema, hapo Roho Mtakatifu yupo sana, kwasababu yeye kiini chake ni ushirika. Ukitaka aitumie vizuri karama yako, hakikisha unakuwepo miongoni mwa kanisa, ili idhihirike, kwasababu haiwezi kudhihirika mahali ambapo upo peke yako.

Kwasababu vipawa hivyo yeye mwenyewe anasema anavitoa kwa lengo la  kuwakamilisha watakatifu, na kuujenga mwili wa Kristo (Waefeso 4:12), na si vinginevyo, Hivyo utaujengaje mwili wa Kristo endapo unajitenga na wenzako?

Kumbuka ofisi kuu, tuliyonayo sasa ni ya Roho Mtakatifu. Hivyo, tunamuhitaji sana ajae ndani yetu ili atuongoze katika kweli yote. Tukimzimisha, au tukimuhuzunisha, tutashindwa kumshinda shetani katika zama hizi za siku za mwisho.

Hivyo penda ushirika, penda umoja na watakatifu. Na Roho Mtakatifu atachukua nafasi yake juu yako.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

Roho Mtakatifu ni nani?.

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

Je! Unaweza kubatizwa na usipokee Roho Mtakatifu?. Na Je! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono?

USINIONDOLEE ROHO WAKO MTAKATIFU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2022/12/05/ushirika-wa-roho-mtakatifu-ukae-nanyi-nyote/