Biblia inasema tujihadhari na “Mbwa” hawa mbwa ni akina nani? (Wafilipi 3:2)

by Admin | 7 February 2023 08:46 pm02

Jibu: Tusome..

Wafilipi 3:2  “Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao”

Hapa kuna makundi matatu yaliyotajwa ambayo tunapaswa tujihadhari nayo, kundi la Kwanza ni “MBWA” kundi la Pili ni “WATU WAJIKATAO” na kundi la tatu ni “WATU WATENDAO MABAYA”.

Sasa kabla ya kwenda kuangalia Mbwa ni watu wa namna gani, kwanza tuyatazame haya makundi mawili ya mwisho, ambayo ni watu wajikatao na watenda mabaya..

Watu “watendao mabaya” wanaozungumziwa hapo, ni watu walio ndani ya imani lakini wanatenda mabaya.. watu hawa biblia imetuonya tujihadhari nao, yaani tusichangamane.. Mtume Paulo alizidi kuliweka hili vizuri katika kitabu cha 1Wakorintho 5:9-11.

1Wakorintho 5:9  “Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.

10  Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.

11  Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye”.

Lengo la kutochangamana na makundi haya ya watu walio ndani ya kanisa lakini ni watenda mabaya, ni ili wajisikie aibu kwa wanayoyafanya na hatimaye wageuke na kutubu.

Kundi la Pili: Ni “Watu Wajikatao”.. kumbuka hapa anasema “watu wajikatao” na sio “watu wajikataao” kuna tofauti ya kujikata na kujikataa.. hapa wanazungumziwa watu wanaojikata!.. Sasa ni watu gani hao wanaojikata?.. si wengine bali walikuwa ni wayahudi ambao walikuwa wanashinikiza tohara, kuwa ndio dalili ya kukubaliwa na Mungu..

Lilikuwepo kundi la walioamini, ambao hata sasa lipo lililokuwa linasisitiza tohara kuwa ni jambo la lazima, na kwamba mtu asipotahiriwa hawezi kukubaliwa na Mungu. Watu hawa walikuwa kweli wamemwamini Yesu lakini sheria za torati bado zilikuwa zinawaendesha, ambazo kimsingi hizo haziwezi kumkamilisha mtu, bali Neema ya Yesu pekee… kushika mwezi, mwaka, siku, sabato haya yote hayafai katika kumkamilisha mtu.

1Wakorintho 7:19  “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu.

20  Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa”

Kwa maelezo mengine marefu kuhusiana na watu wajikatao unaweza kufungua hapa >>> WATU WAJIKATAO

Na kundi la Tatu na la Mwisho, ambalo biblia imetaja tujihadhari nalo ni kundi la “MBWA”.

 Sasa utajiuliza hawa “Mbwa” ni akina nani?

Bwana Yesu aliwataja wazi kabisa hawa Mbwa ni wakina nani.. Tusome..

Mathayo 7:15  “Jihadharini na MANABII WA UONGO, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni MBWA-MWITU WAKALI.

16  Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti”

Umeona?… Kumbe Mbwa wanaozungumziwa hapo ni “Manabii wa Uongo” na tena hawajatwi kama Mbwa tu!, bali kama “Mbwa-Mwitu” tena wakali!.. maana yake wasiohurumia kundi.. Na hatutawatambua kwa mionekano yao, kwasababu kwa nje wamevaa mavazi ya kondoo, (wanafanana na watumishi wa kweli wa Mungu) lakini tutawatambua kwa matunda yao, maana yake kwa yale wanayoyafundisha na wanayoyaishi.

Na manabii wa uongo ni mjumuisho wa Mitume wa Uongo, wachungaji wa uongo, waalimu wa Uongo, pamoja na waimbaji wa Uongo. Kwaufupi watu wote wanaosimama kutangaza injili kwa wengine! Lakini maisha yao ya ndani si wakristo, ila kwa nje wanasifika kama watumishi wa Mungu.

Ikiwa mtu atasimama na kuhubiri injili nyingine tofauti na ile iliyoandikwa katika biblia, basi huyo kibiblia ni “Mbwa”, ikiwa mtu atahubiri injili isiyo ya wokovu, badala yake ya kumpoteza mtu au kumfanya afurahie dhambi..mtu huyo kibiblia ni Mbwa, na tumetahadharishwa kukaa mbali naye.

Nabii wa Kweli wa Mungu atakuwa kama Musa!, Mpole kuliko wote, na mwenye kuwaelekeza watu kwa Mungu na si kwake wala kwa shetani.

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

 2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

 3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye”

Je! Unaongozwa na nani?.. Manabii wa Uongo, Miujiza na Ishara au NENO LA MUNGU?.

Kumbukumbu 6:4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 

5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Watu wajikatao ni watu wa namna gani? (Wafilipi3:1).

Mstari huu una maana gani? “Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi”. (Mhubiri 11:1)Kutekewa maana yake nini?(Mathayo 22:12)

Mungu anatufundisha kusamehe mara saba sabini, ila Kwanini yeye hakumsamehe Adamu alipoasi?.

HAKUONA MAHALI PA KUTUA KWA WAYO WA MGUU WAKE.

VICHEKESHO NA UTANI MADHABAHUNI

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/02/07/biblia-inasema-tujihadhari-na-mbwa-hawa-mbwa-ni-akina-nani-wafilipi-32/