by Admin | 14 March 2023 08:46 pm03
Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo.
Naamini kuwa ulishawahi kusoma katika maandiko kuwa kuna mahali Yesu alilala. Lakini ulishawahi kujiuliza ni kwanini habari ile iandikwe kulikuwa na umuhimu gani?
Kumbuka kila tukio lililoandikwa katika biblia limebeba somo kwetu sisi watakatifu.
Jambo pekee lililomfanya Yesu alale usingizi mzito namna ile, sio kuchoka kama wengi wanavyodhani, kuna nyakati nyingi Yesu alikuwa anachoka kuliko hata hapa, lakini alikuwa halali, anapanda mlimani kuomba…lakini ni nini kilichompelekea alale?
Jambo lililompa Yesu usingizi mzito, ni ile DHORUBA iliyoanza kule baharini.
Marko 4:36-39
[36]Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye.
[37]Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji.
[38]Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia?
[39]Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu.
[40]Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
Umeona hapo, hakuna mahali popote biblia inarekodi Yesu alipitiwa na usingizi, isipokuwa hapo kwenye dhoruba kuu.
Wakati wengine wanahangaika na matatizo, hawapati usingizi, wanapambana na changamoto zao..upande wa pili wa Yesu mambo ni tofauti,kule kuyumba kwa chombo kumbe ndio kulikuwa kunavuta usingizi vizuri.
Lakini ni nini Bwana anataka tujifunze juu ya tabia hii ya Kristo?
Ni kwamba hata yeye akiwa amejaa vizuri ndani yetu, tutadhihirisha tabia kama zake.
Ni kwanini leo hii tuna hofu ya maisha, tuna hofu ya kesho, tutaishije, tutakula nini, tutavaa nini? tuna hofu ya wezi, tuna hofu na kufukuzwa kazi, tuna hofu ya magonjwa?
Ni kwasababu Kristo hajajaa ndani yetu vizuri, ni kwasababu hatujapokea uhakika wa kuwa salama daima.
Wakristo wengi, wakiwa kwenye matatizo, mbalimbali hawana raha, wanapoteza utulivu..wanahangaika huku na kule kama wakina Petro. Hii ni hali ya kawaida ya kibinadamu. Lakini Yesu anaweza kukupa usingizi katikati ya tufani na dhoruba..endapo atajaa ndani yako vizuri.
Unachopaswa kufanya ni jiachie tu kwa Yesu, mwache yeye ahangaike na hiyo tufani, itaisha tu yenyewe, haitadumu muda mrefu, atakufungulia mlango wa kutoka katika hilo jaribu, haijalishi ni kubwa kiasi gani.
Jiachie tu kwa Yesu mtafakari yeye muda wote, muwaze yeye na uweza wake, Kama hujaokoka, hakikisha unafanya hivyo sasa, hivyo kwa jinsi utakavyokuwa unaendelea kumsogelea yeye ndivyo atakavyokupa wepesi kwa kukabiliana na mambo yote, na changamoto zote unazokutana nazo..Na hatimaye zitaisha tu bila hata kusumbuka kwasababu yeye yupo kazini.
Mkaribie Yesu sasa acha kuzitegemea akili zako mwenyewe..Naye atakusaidia, yeye mwenyewe anasema;
Mathayo 11:28-29
[28]Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
[29]Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu
Anasema pia..
Mathayo 6:31-34
[31]Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
[32]Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
[33]Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
[34]Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Mkaribie Yesu, Akutue mizigo. Akupe uzingizi, akupe raha.
Zaburi 127:2 “Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi”
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.
WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.
NA WATU WOTE WALIKUWA WAKIAMKA MAPEMA, WAENDE HEKALUNI.
Dia ni nini katika biblia? (Mithali 13:8)
SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!
KATAA KUWA EUTIKO, WA KUSINZIA IBADANI.
BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/03/14/yesu-katika-usingizi-wake/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.