Je ni kweli wanafunzi wa Yesu walikuwa hawanawi mikono?

by Admin | 29 March 2023 08:46 am03

Swali: Je ni kweli Bwana Yesu mwenyewe na wanafunzi wake walikuwa hanawi mikono kabla ya kula?..kulingana na Mathayo 15:2, na Luka 11:37

Jibu: Turejee,

Mathayo 15:1 “Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema

2 Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula”

Tusome tena, Luka 11:37..

Luka 11:37  “Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani.

38  Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula”.

Je ni kweli Bwana Yesu na wanafunzi wake walikuwa hawanawi mikono kabla ya kula kulingana na mistari hiyo?

Jibu ni la! Bwana Yesu na wanafunzi wake walikuwa wananawa mikono kabla ya kula, huo ni usafi wa kawaida tu ambao kila mtu anao.

Hauwezi kutoka kushika mavumbi halafu uanze kula hivyo hivyo, labda uwe hauna akili timamu. Na Bwana pamoja na wanafunzi wake walikuwa ni watu wenye akili timamu, kama Bwana aliweza kuwaosha wanafunzi wake miguu kunawa mikono ni nini kwake? (Yohana 13:9-10).

Sasa swali kama Bwana na wanafunzi walikuwa wananawa mikono, kwanini Mafarisayo na Masadukayo waseme alikuwa hanawi?

Jibu ni kwamba Mafarisayo walikuwa wanafuata desturi za wazee, ambao kulingana na sheria ilikuwa kabla ya kula ni lazima mtu aoshe mikono mpaka kwenye kiwiko!.. Jambo ambalo halikufanywa na wanafunzi wa Yesu wala Bwana Yesu mwenyewe… kwani Bwana na wanafunzi wake walikuwa wananawa tu kawaida, bila kufikisha maji kwenye viwiko.

Marko 7:2  “wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa.

3  Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao”

 Kama tu leo sisi tunavyonawa kabla ya kula, tukitaka kula huwa tunaosha tu viganja, lakini hatuoshi mkono mzima mpaka kwenye kiwiko, hivyo kulingana na desturi za wayahudi, mtu aliyeosha kiganja tu, bila kufika mpaka kwenye kiwiko, mtu huyo anahesabika kama bado hajanawa kabisa.

Hivyo kulingana na desturi hizo za kiyahudi, hata sisi tunaonawa sasa katika viganja tu, mbele zao tunahesabika kuwa  watu wanaokula bila kunawa!. Kwahiyo na Bwana pamoja na wanafunzi wake hawakuwa wananawa hadi kwenye viwiko, ndio maana wakashutumiwa vile, lakini walikuwa wananawa kama tu sisi tunavyonawa sasa.

Na ni kwasababu gani wanafunzi, hawakufuata desturi hizo za wazee za kunawa mpaka kwenye kiwiko?

Bwana Yesu alishatoa sababu kuwa kinachomwingia mtu hakiwezi kumtia unajisi bali kinachomtoka.

Mathayo 15:17  “Hamjafahamu bado ya kuwa kila kiingiacho kinywani hupita tumboni, kikatupwa chooni?

18  Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19  Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano”

Hivyo na sisi tujihadhari sana na vitu tunavyovitoa katika vinywa vyetu kwasababu vinakuwa vinatoka mwilini, lakini zaidi sana tujitahidi kuwa wasafi kimwili, kwasababu hata Bwana Yesu alikuwa ananawa.

Bwana atubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

Mikono iliyotakata ni mikono ya namna gani? (1Timotheo 2:8).

MPENDEZE MUNGU ZAIDI.

Biblia inasemaje kuhusu Kazi?

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/03/29/je-ni-kweli-wanafunzi-wa-yesu-walikuwa-hawanawi-mikono/