Biblia inasemaje kuhusu Kazi?

Biblia inasemaje kuhusu Kazi?

Jibu: Biblia imetuelekeza kufanya kazi za Mikono, ambayo kupitia hiyo Mungu atatupa riziki zetu za kila siku.

1Wathesalonike 4:11  “Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza;

12  ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote”

Hivyo ni wajibu wa kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi, afanye kazi, aidha za Mikono au za kiutumishi.

Kazi za mikono ni zile zote zinazohusisha kuajiriwa au kujiajiri, na kazi za kiutumishi ni zile zote za Madhabahuni au za kiinjilisti. Mkristo yoyote ni lazima awepo katika kundi mojawapo ya hayo mawili, akikosekana katika yote (na ilihali ni mzima, au hana tatizo lolote lile) basi mtu huyo yupo kinyume na Neno la Mungu, aidha kwa kujua au kutokujua.

Mtume Paulo alisema kwa uongozo wa Roho, kuwa mtu yeyote asiye na shughuli yoyote katika Mwili wa Kristo, yaani asiyefanya kazi yoyote ya Madhabahuni  kama Uchungaji, Uinjilisti, au Shemasi, au Mzee wa kanisa au ya Uinjilisti, au mfanya kazi wa kanisani (inayomfanya muda wake mwingi atumie kuhubiri) mtu huyo basi asipewe fungu lolote kutoka kanisani..

1Wathesalonike 3:10 “ Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.

11  Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.

12  Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe”

Kumbuka pia unapoamua kufanya kazi za Mikono, basi huwezi kuwa Mchungaji kwa wakati huo huo, kwasababu huwezi kushikilia mambo mawili kwa wakati mmoja.. Ni aidha ushikilia moja uache lingine! Huwezi kuwa mchungaji na huku ni Mbunge, huwezi kuwa Mchungaji na huku ni Mfanya biashara mashuhuri.. jambo hilo haliwezekani!, haijalishi mtu atalilazimisha kiasi gani?.

Mathayo 6:24  “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali”

Tofauti na inavyodhaniwa na wengi kwamba Mtume Paulo alikuwa anafanya kazi muda wote!, kwamba alikuwa anashona Mahema kila wakati ili kujipatia riziki, nataka nikuambie kuwa haikuwa hivyo, ni sehemu chache sana ndizo alizokuwa anashona mahema, lakini sehemu kubwa ya maisha ya Paulo ilikuwa ni kuhubiri injili, na Mungu alikuwa anamfungulia milango ya riziki kupitia injili hiyo, na alikuwa haombi kwa watu fedha wala mali, (ili awe kielelezo) bali watu walikuwa wanampa kwa kadiri wanavyoguswa.

Tunalithibitisha hilo katika kitabu cha Wafilipi, 4:1-19, (Zingatia Mistari iliyoainishwa kwa herufi kubwa)

Wafilipi 4:14  “Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu.

15  Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika HABARI HII YA KUTOA NA KUPOKEA, ila ninyi peke yenu.

16  KWA KUWA HATA HUKO THESALONIKE MLINILETEA MSAADA KWA MAHITAJI YANGU, WALA SI MARA MOJA.

17  Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.

18  Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; NIMEPOKEA KWA MKONO WA EPAFRODITO VITU VILE VILIVYOTOKA KWENU, HARUFU YA MANUKATO, SADAKA YENYE KIBALI, IMPENDEZAYO MUNGU.

19  Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”

Umeona hapo ? Sio wakati wote Paulo alikuwa anafanya kazi ya kushona, Soma pia 2Wakorintho 8:1-5..

Lakini biblia inatufundisha nini katika hali tulizopo (yaani ya kufanya kazi ya Mikono au ya Madhabahuni)?

Biblia imetufundisha kutumika kwa uaminifu popote pale tunapopatumikia, maana yake kama ni Mtumwa basi tumika ipasavyo kwa Bwana wako (maana yake Boss wako, au Mkubwa wako) kana kwamba unamtumikia Kristo.

Waefeso 6:5  “Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo;

6  wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

7  kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

8  mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru”.

Vile vile kama tunatumika katika utumishi wowote ule.. Maandiko yanatufundisha  KURIDHIKA, Maana yake TUSIJISIKIE VIBAYA kutumika pale tulipopachagua sisi, kwasababu ni mapenzi ya Mungu. Kama ni Mfanyakazi wa kuajiriwa maana yake wewe ni Huru kwa kazi ya Bwana ya madhabahuni, hivyo usijisikie vibaya kuifanya kazi hiyo, kilicho kikubwa na cha muhimu ni wewe kuwa Mwaminifu katika kazi unayoifanya na pia katika kumtolea Bwana, na mwisho wa siku utapokea thawabu kutoka kwa Mungu, vile vile kama wewe ni mtumishi wa Madhabahuni au wa Injili, maana yake wewe ni Huru katika utumishi wa kazi za kidunia, hivyo basi usijisikie vibaya kutumika hivyo, maana ni Mungu kakuita katika hali hiyo, wala usiitamani kazi nyingine zaidi ya hiyo uliyopewa!.  

1Wakorintho 7:21  “Je! Uliitwa u mtumwa? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia.

22  Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.

23  Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

MAOMBI YA KUFUNGULIWA KIUCHUMI.

Orodha ya mistari ya biblia kuhusu watoto.

Kwanini iwe ni nchi ibubujikayo maziwa na asali?

Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments