TUUTAFUTE USEMI MMOJA. TUUJENGE MNARA WA MUNGU

by Admin | 17 April 2023 08:46 am04

Nakusalimu katika jina tukufu sana la mwokozi wetu Yesu Kristo, Nakualika katika kuyatafakari maneno ya uzima.

Leo tutajifunza siri mojawapo iliyokuwa nyuma ya watu wa zamani, ambayo tukiitumia na sisi italeta mageuzi makubwa sana katika ulimwengu huu tunaoishi. Wengi wetu tunadhani watu wa leo wanayoakili zaidi ya kuwashinda wale, lakini ukweli ni kwamba yapo mambo mengi yalifanywa na watu wa kale, ambayo mpaka leo hatuwezi kuyafanya. Mfano mmojawapo ni yale mapiramidi yaliyopo Misri (ambayo yapo katika maajabu saba ya dunia), teknolojia iliyotumika pale, hadi sasa hakuna ujenzi unaoweza kuwa kama ule, ijapokuwa tunazo teknolojia kubwa na za kisasa.

Tukisoma katika maandiko tunaona, Jinsi Babeli ilivyoanza kujengwa na kusitawi. Lakini hilo halikuwa jambo zito, kwasababu miji mingi pia ilikuwa inajengwa. Jambo lililoipelekea Babeli kuwa tofauti na miji mingine ni pale watu walipotaka kuunda Mnara, ndani ya mji ule, lengo lao likuwa ni kufika MBINGUNI, ili wajipatie jina. Sasa wengi wetu tunaona kama walikuwa ni wajinga kuunda hiyo Projekti yao. Tunadhani walikuwa wanafanya jambo la masiara au walikuwa hawaelewi kitu wanachokifanya. Ni sawa na leo mtu akumbie ninaunda ndege, ambayo itanifikisha mbinguni, ni rahisi kusema amerukwa na akili. Lakini maandiko yanatuonyesha watu hawa, walikuwa wanajua wanachokifanya mpango huo wangeweza kufanikiwa kama Mungu asingeingilia kati. Embu tusome habari hiyo tuombe jambo hilo;

Mwanzo 11:1 “Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.  2 Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. 

3 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.  4 Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. 

5 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.  6 Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, WALA SASA HAWATAZUILIWA NENO WANALOKUSUDIA KULIFANYA. 

7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.  8 Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.  9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote”.

Umeona hapo? Mungu hakusema hawa watu wamerukwa na akili, wanafanya kazi isiyokuwa na faida, bali alisema hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Maana yake ni kuwa watafanikiwa, Hivyo Mungu akaangalia NGUVU yao ya kufikia adhma yao ipo wapi? Akaona kuwa sio katika ile teknolojia, bali katika ule USEMI MMOJA waliokuwa nao.

Usemi maana yake ni NIA. Hawa watu waliingia maagano,wakapatana kwa moyo mmoja, kwamba kila mmoja atajitoa kwa akili, hali na mali, kuhakikisha Mnara huo unajengeka na kilele chake kinafika mbinguni, hata kama itawagharimu miaka 1000, lakini mwisho wa siku ni lazima wafike mbinguni. Lakini Mungu akaenda kuuchafua usemi wao wakawa hawaelewani baada ya pale, kwasababu walichokuwa wanakijenga ni kwa ajili ya JINA LAO na sio jina la MUNGU. Hivyo Usemi wao ukachafuliwa wakawa hawaelewani, mpaka na lugha zao zikageuzwa pia.

Ni nini Bwana anataka tuone hapo,

Ni nguvu ya USEMI MMOJA.

Na sisi kama kanisa la Kristo lililo hai. Nafasi yetu ya kuufikia utukufu WOTE wa Mungu ulio mbinguni tunao.

Kwasababu Tayari siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alirudisha USEMI HUU mmoja katikati yetu. Na ndio maana siku ile utaona watu walianza kunena kwa lugha za mataifa mengine magheni, kuonyesha kuwa Sasa Mungu anataka mataifa yote wakaribie waliunde taifa la Mungu haijalishi lugha zao, jinsia zao, rangi zao. Alikuwambusha tukio lile la Babeli, kwamba sasa lianze kufanyika tena kwa jina la Bwana.Watu wale wakatii na siku ile ile kanisa likaanza. Mnara wa Mungu ukaanza kujengwa duniani.

Matendo 2:1  “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2  Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 3  Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4  Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. 5  Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. 6  Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7  Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? 8  Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? 9  Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia.

10  Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,.11  Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

12  Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?

Na ndio maana hatushangai kwanini Kanisa la kwanza lilikuwa na mapinduzi makubwa sana. Kwa kipindi kifupi sana injili ilinea duniani kote, na walikuwa hawana vyuo vya biblia. Ni kwasababu walikuwa na USEMI mmoja.

Lakini leo kanisa limevunjika vunjika, shetani kalisambaratisha, kachafua lugha yetu. Hata ndani ya kanisa moja kila mmoja anao usemi wake. Ijapokuwa wote mnaliamini Neno hilo hilo moja. Kwasababu gani, ni kwasababu tunatafuta utukufu wetu wenyewe na sio ule wa Mungu.

Ni kweli tutaunganishwa na Neno lakini tusipotaka kujishusha na kutii, ili tumwinue Kristo na sio sisi wenyewe, kamwe hatutaona utukufu wa Mungu kama vile inavyopaswa. Hatutaufikia moyo wa Mungu mbinguni, hatutaona udhihirisho wa wazi wa Miujiza mikubwa ya Mungu katika kanisa. Ni sharti tujikane nafsi zetu kila mmoja tumfuate Yesu , ili tuujenge mnara huu wa Bwana.

Luka 14:27  “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 28  Maana ni nani katika ninyi, KAMA AKITAKA KUJENGA MNARA, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? 29  Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki”.

Tufahamu kuwa kanisa sio shirika la kijamii, sio huduma, wala sio chuo Fulani, bali ni udhihirisho wa Mungu duniani kupitia watu wake aliowakomboa. Hivyo ni lazima sisi kama viungo vya Kristo tujishikamanishe tuwe mwili mmoja Ili Kristo atende kazi zake duniani kama alivyokuwa anatenda zamani. Na hii inaanza na mtu mmoja mmoja, pale tunapodhamiria kuyatii maneno ya Kristo.

Bwana atujalie kuliona hilo.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?

Pentekoste ni nini?

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA YOANA NA MANAENI?

USIIKARIBIE DHAMBI, KAA NAYO MBALI.

Kibiriti ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/04/17/tuutafute-usemi-mmoja-tuujenge-mnara-wa-mungu/