by Devis Julius | 4 June 2023 08:46 pm06
Swali: Maandiko yanatuonyesha Tera, baba yake Abramu aliishi jumla ya miaka 205 (Mwanzo 11:32) na tena yanaonyesha kuwa Tera alimzaa Abramu akiwa na miaka 70 (Mwanzo 11:26), na ukirudi kwenye Mwanzo 12:4 biblia inatuonyesha tena Abramu alitoka nchi ya Harani alipofikisha miaka 75.
Sasa ukipiga mahesabu vizuri utaona miaka aliyoishi Tera baba yake Abramu isingepaswa iwe 205, bali iwe miaka 145 yaani (70+75=145) kama Abramu aliondoka kwelii Harani baada ya kifo cha babaye! , Lakini tunaona biblia inatuambia umri wa Tera ulikuwa ni miaka 205. (Je biblia inajichanganya!)
Jibu: Jibu ni kwamba Biblia haijichanganyi na wala haijawahi kujichanganya, vinginevyo ingekuwa ni kitabu cha uongo!. Lakini tunaona maneno yaliyomo ndani ya biblia ni ya uzima tena yenye Nguvu.
Sasa tukirudi kwenye swali letu, je! Abramu alitoka Nchi ya Harani kabla au baada ya kufa baba yake? Jibu ni kwamba alitoka BAADA YA BABA YAKE KUFA!, Na si kabla!. Tunalithibitisho hilo Zaidi katika kitabu cha Matendo ya Mitume..
Matendo 7:2 “Naye akasema, Ndugu zangu na baba zangu, sikilizeni: Mungu wa utukufu alimtokea baba yetu Ibrahimu, alipokuwa katika Mesopotamia, kabla hajakaa Harani,
3 akamwambia, Toka katika nchi yako na katika jamaa zako, ukaende hata nchi nitakayokuonyesha.
4 Ndipo alipotoka katika nchi ya Wakaldayo, AKAKAA HARANI, AKATOKA HUKO BAADA YA KUFA BABAYE, Mungu akamhamisha mpaka nchi hii mnayokaa ninyi sasa.
Sasa kama ni hivyo kwanini hesabu ya miaka haikai sawa..badala ya miaka 145 anaonekana kufa akiwa na miaka 205?.
Jibu ni kwamba Tera hakumzaa Abramu akiwa na miaka 70, bali maandiko yanasema alipofikisha umri wa miaka 70 akamzaa Abramu, Nahori na Harani. (watoto watatu).
Mwanzo 11:26 “Tera akaishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani”.
Maana yake ni kwamba watoto hawa watatu walianza kuzaliwa baada ya Tera kufikisha miaka 70, na si kwamba wote watatu walizaliwa ndani ya mwaka mmoja, bali walizaliwa katika vipindi tofauti tofauti pengine walipishana miaka mitano mitano au hata kumi kumi au hata Zaidi ya hapo, lakini Tera alipofikisha miaka 70 ndipo alipoanza kuzaa!
Sasa swali la msingi hapa ni mtoto yupi aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa na yupi aliyekuwa wa mwisho kati ya hao watatu..
Katika hiyo Mwanzo 11:26 tunaona Abramu akitajwa wa kwanza, sasa hiyo haimaanishi kuwa yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzaliwa!!.. Orodha hiyo imetajwa kufuatia heshima ya watu hao na si ukubwa!.. Abramu ndiye aliyetukuka mbele za Mungu Zaidi ya hao ndugu zake wawili ndio maana kawekwa hapo wa kwanza..kwasababu habari inayoendelea itamhusu yeye yeye na uzao wake.. hiyo ndio sababu ya yeye kutajwa wa kwanza na si nyingine.. Lakini kuhalisia aliyekuwa mkubwa kuliko wote pale ni Harani.
Tunajuaje Harani ndiye aliyekuwa mkubwa kuliko Abramu na Nahori?…
Kwanza Abramu alisafiri na Lutu, ambaye alikuwa ni mtoto wa Harani kaka yake.. Na wakati huo tayari Lutu alikuwa mtu mzima kipindi anasafiri na Abramu (Mwanzo 12:5)… Pili Abramu na Nahori aliyetajwa wa pili kwenye orodha alimwoa mtoto wa Harani kaka yake.
Mwanzo 11:29 “Abramu na Nahori wakajitwalia wake. Jina la mkewe Abramu aliitwa Sarai, na jina la mkewe Nahori ALIITWA MILKA, BINTI HARANI, ambaye alikuwa baba wa Milka na wa Iska”.
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Abramu hakuwa mtoto wa kwanza wa Tera bali huenda alikuwa wa pili au wa tatu, Harani ndiye aliyekuwa wa kwanza ingawa kwenye orodha ameonekana wa mwisho…na Tera hakumzaa Abramu akiwa na miaka 70 bali akiwa na miaka 130. Na Abramu aliondoka Harani alipofikisha miaka 75 baada ya kifo cha baba yake, ambaye alikufa akiwa na miaka 205.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Je! biblia inajichanganya katika 1Petro 2:13 na Matendo 5:29.
Je Henoko aliyeenda na Mungu alikuwa ni mwana wa Kaini? (Mwanzo 4:16)
NINI KINAFUATA SIKU ILE ILE YA KUOKOKA!
Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/06/04/je-abramu-aliondoka-harani-kabla-ya-baada-ya-kifo-cha-baba-yake/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.