JE! TUNAPASWA TUOMBE MARA NGAPI KWA SIKU?

by Admin | 25 September 2023 08:46 am09

Biblia haijatoa ‘fomula’, ya idadi ya nyakati tunazopaswa kuomba kwa siku. Ila imesema ‘tuombe kila wakati’ na sehemu nyingine imesema ‘tuombe bila kukoma’. Hiyo ni kutupa uelewa kwamba maombi yanapaswa yawe ni endelevu lakini pia yawe ya wakati wote. Na hakuna mahali maandiko yanatoa nafasi ya mwaminio kutokuomba kabisa.

Waefeso 6:18  “kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;”

1Wathesalonike 5:17  “ombeni bila kukoma”

Hivyo ni sisi kutazama, watakatifu walikuwa na desturi gani, na nidhamu gani waliyojijengea katika kuomba. Je! Walitumia vipindi vingapi kwa siku? Vilevile tutaona Bwana Yesu anasemaje kuhusiana na hilo pia. Ili na sisi tuige vielelezo vyao katika  utaratibu wetu wa kusali.

DAUDI

Daudi aliomba mara tatu(3) kwa siku . Asubuhi, adhuhuri na jioni.

Zaburi 55:17 Jioni, asubuhi, na adhuhuri nitalalama na kuugua, Naye ataisikia sauti yangu.

DANIELI

Danieli pia aliomba mara tatu (3), kwa siku.

Danieli 6:10 Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo.

Hivyo hii ni kutuonyesha kuwa ilikuwa ni desturi ya watakatifu wa kale, kwenda magotini walau mara 3 kwa siku. Na maombi waliyoyaomba hayakuwa ‘sala’ za dakika tano (kama zile za kuombea chakula).  Bali ni maombi ambayo huwenda yalizidi saa moja, kwasababu maombi  ya kulalama, na kuugua, (mfano wa hayo ya Daudi) sio ya dakika chache.

YESU KRISTO.

Bwana Yesu aliomba alfajiri na usiku, na majira mengi nyakati za adhuhuri aliahirisha huduma na kwenda mahali pa utulivu kusali.

Marko 1:35  “Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko”

Na usiku

Mathayo 26:40  “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41  Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu”.

Adhuhuri

Luka 5:16  “Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba”

Hivyo tunaona pia Bwana aliomba nyakati zote. Alipopata nafasi.

Hivyo kiwango cha chini kabisa cha nyakati za kuomba kwa siku kwa sisi wakristo ni MARA MBILI. Yaani asubuhi na jioni.  Unapoanza siku huna budi kuanza na Bwana kwa kumshukuru na kumwomba mwongozo wa siku hiyo, vilevile unapomaliza siku wapaswa ufanye hivyo hivyo.

Na ndio maana Bwana alisema maneno haya, kwa watu wake wanaoomba alisema;

Luka 18:7  Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

Kumbe usiku na mchana tunapaswa tuombe. Walau mara mbili kwa siku. Alisema, Yeye ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho. Kufunua kuwa yupo katika mwanzo wetu na mwisho wetu. Hakikisha uanzapo siku unatenga muda wa kutosha wa kuingia uweponi, na umalizapo siku unafanya hivyo hivyo. Utakuwa imara sana kiroho.

Lakini zaidi sana Bwana anataka tuwe watu wa kuomba siku zote kufikia hata kukesha. Hivyo ikizidi hapo ni vema sana, kwasababu utajiwekea akiba ya maombi kwa wakati ambao utakuwa na nguvu chache.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

HIZI NI NYAKATI ZA KUFUNGA NA KUOMBA

Fahamu Namna ya Kuomba.

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?.

MAUTI NA UZIMA HUWA KATIKA UWEZO WA ULIMI.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/09/25/je-tunapaswa-tuombe-mara-ngapi-kwa-siku/