MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

by Admin | 2 November 2023 08:46 pm11

Safari ya wokovu ya mkristo inafananishwa na safari ya Wana wa Israeli kutoka Misri kwenda Kaanani. 

Na kama vile maandiko yanavyotuonyesha walikombolewa wote Kwa damu ya Mwana kondoo, Kisha Wakabatizwa katika bahari ya Shamu, wakawa chini ya wingu la Roho Mtakatifu kule jangwani,.. Lakini katika hayo yote bado tunaambiwa wengi wao hawakuweza kuiona Ile nchi ya ahadi. Isipokuwa wawili tu, (yaani Yoshua na Kalebu), waliotoka nchi ya Misri.

Biblia inatuonyesha walipishana na majaribu 5, ambayo yaliwafanya waangamie jangwani. Na majaribu yenyewe tunayasoma katika 1Wakorintho 10:1

1 Wakorintho 10:1-12

[1]Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; [2]wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

[3]wote wakala chakula kile kile cha roho; [4]wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. [5]Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.

[6]Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. [7]Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.

[8]Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. [9]Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

[10]Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. [11]Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. [12]Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

Kama tunavyosoma hapo. Makosa hayo yalikuwa ni haya;

  1. Kutamani mabaya
  2. Kuabudu sanamu
  3. Kufanya uasherati
  4. Kumjaribu Mungu
  5. Kunung’unika

1) Kutamani mabaya

Mungu aliwapa MANA kama chakula pekee ambacho wangekula jangwani, wao na mifugo Yao, lakini, baadaye waliikinai wakataka NYAMA, na vyakula vingine (Hesabu 11:4-35), matokeo yake ikiwa Mungu kuwaua, wengi wao.

Kama wakristo tuliookoka MANA yetu ni NENO LA MUNGU, Hatupaswi kulikinai, tukakimbilia chakula kingine kisicho Cha kiMungu. Tukataka tuongozwe na mifumo ya kidunia. Ndugu ni hatari mbaya sana. Kumbuka Ile mana ijapokuwa kilikuwa ni chakula Cha aina Moja, lakini hawakuwahi kuumwa, Wala kudhoofika, Wala miguu yao kupasuka, tofauti na walivyokuwa Misri penye vyakula vingi, lakini vimegubikwa na magonjwa. 

Ndugu Lipokee Neno la Mungu, ishi Kwa hilo, hata kama halitavutia (kidunia), lakini limebeba virutubisho vyote vya kimwili na kiroho. Wanaotembea Kwa Neno la Mungu, hawatikisiki hustawi milele.

2) kuabudu sanamu:

Walipomwona Musa amekawia mlimani, na Mungu hazungumzi chochote Kwa wakati ule  wakajiundia sanamu zao za ndama waziabudu. Wakacheza, wakala na kinywa (Kutoka 32). Hii ni kuonesha kuwa kitu chochote kinachokufanya ushangilie  tofauti na Mungu wako, ni ibada ya sanamu.

Rafiki kuwa makini Kwa wakati wa Leo mkristo kushabikia mipira, kwenda Disko, kutumikia Mali, kufuatilia vipindi vya sinema kulikopitiliza, chattings, kupenda anasa. Ni ibada za sanamu waziwazi.

 Kwasababu gani?. Kwasababu ndio bubujiko lako la roho lilipo kama ilivyokuwa Kwa Wana wa Israeli, Kwa sanamu zile. Ikapelekea watu wengi kufa siku Ile. Ibada Yako iwe Kwa Bwana. Mungu ni mwenye wivu. Mpira ukichukua nafasi zaidi ya Mungu wako ni kosa.

3) Kufanya uasherati

Walipokuwa jangwani Mungu aliwakataza wasitangamane na wageni, kwasababu watawageuza mioyo na kuiabudu miungu Yao. Lakini wao walipowaona wanawake wa taifa la Moabu, wakaenda kuzini nao, Kisha wakageuzwa mioyo wakaabudu miungu Yao. Hiyo ikawa sababu ya Mungu kuwaua waisraeli wengi sana idadi yake 23,000.

Na sisi kama wakristo tulishapewa tahadhari kwenye maandiko. Tusifungwe nira na wasioamini isivyo sawasawa (2Korintho 6:14-18). Kwasababu hakuna ushirika kati ya Nuru na Giza. Hivyo hatuna budi kuwa makini na ulimwengu, tushirikiane nao kwenye mambo ya kijamii na ya msingi, pale inapokuwa na ulazima, lakini ya kiroho, hatupaswi hata kidogo kuwa na urafiki nao kwasababu ni rahisi kugeuzwa moyo na kuambatana nao kitabia, na matokeo yake tukamwasi Mungu.

Sulemani aligeuzwa moyo, Wana wa Mungu tunaosoma kwenye Mwanzo 6 nao pia waligeuzwa mioyo Kwa jinsi hiyo hiyo, na wewe pia usipojiwekea mipaka na watu ambao ni wa kidunia, Unaweza kupoteza taji lako. Pendelea zaidi kuwa na kampani ya waliookoka. Ni Kwa usalama wako. Usijikute unafanya uasherati wa kiroho.

4) Kumjaribu Bwana

Wana wa Israeli walimjaribu Bwana, wakati Fulani wakamnun’gunikia Mungu na Musa, wakisema chakula hiki dhaifu, wakitaka Kwa makusudi Bwana awafanyie Tena muujiza mwingine, Mungu akakasirishwa nao, akawaangamiza Kwa nyoka (Hesabu 21:4-9).

Kama mkristo tambua kuwa Mungu haendeshwi kama “robot”. Kwamba ni lazima afanye jambo Fulani Kila tutakapo ndio tuthibitishe yeye yupo na sisi. Ndugu ukristo wa hivi ni hatari, wengi wameishia kuanguka kwasababu hii. Jaribu kama hili aliletewa Bwana Yesu na shetani jangwani. Ajitupe kutoka kinarani, kwasababu maandiko yanasema Mungu atamuagizia malaika wake wamchukue salama. lakini Bwana Yesu alimwambia shetani usimjaribu Bwana Mungu wako.

Kamwe usimwendeshe Mungu, mwache yeye ayaendeshe maisha Yako. Tuwe na hofu na Mungu wetu.

5) Kunung’unika.

Wana wa Israeli tangu mwanzo wa safari Yao Hadi karibia na mwisho, waligubikwa na manung’uniko tu,(Kutoka 23:20-21) wengi wao hawakuwa watu wa shukrani. Ijapokuwa walilishwa mana, waliouna utukufu wa Mungu Kwa wingi. Lakini bado manung’uniko yalizidi shukrani.

Biblia inatuasa sisi tuliookoka tuwe watu wa Shukrani (Wakolosai 3:15), Kwa kazi aliyoimaliza Yesu pale msalabani ya kuondolewa dhambi ni fadhili tosha zaidi hata ya wale Wana wa Israeli kule jangwani. Hata tukikosa Kila kitu, maadamu tumeahidiwa uzima wa milele. Hatuhitaji kuwa na hofu na jambo lolote. Wokovu wetu ndio uwe faraja.

Epuka Maisha ya manung’uniko.

Bwana akubariki.

Ikiwa tutashinda majaribu haya MATANO katika safari yetu ya wokovu. Basi tutalipokea taji timilifu Kwa Bwana  siku Ile mfano wa Yoshua na Kalebu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/11/02/majaribu-matano-5-ya-mkristo/