by Admin | 11 November 2023 08:46 pm11
Moja ya maeneo ambayo yamekuwa na uelewa mchanga katika ukristo, ni pamoja na eneo la Roho Mtakatifu. Wengi tunachofahamu kuhusiana na huduma ya Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha tu! Basi. Lakini hilo ni tone moja kati ya bahari kubwa, tunahitaji kumwelewa kwa mapana na marefu ili tujue utendaji kazi wake ulivyo kwa wanadamu na ulimwengu.
Kipo kitabu cha Roho Mtakatifu, ikiwa utapenda kukipata wasiliana nasi kwa namba zilizo chini ya chapisho hili/ au tutumie ujumbe whatsapp.
Leo tutaona sehemu mojawapo ambayo inahusiana na mafuta ya Roho Mtakatifu. Unaweza ukajiuliza, kwanini kila mara watu waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, maandiko yanatumia neno “wakajazwa”, na sio neno kama ‘wakavikwa’ au labda ‘wakalishwa’. Kwasababu tukisema wakavishwa maana yake tunamfanya yeye kuwa kama nguo, au tukisema wakalishwa tunamfanya yeye kuwa kama chakula. Lakini tukisema wakajazwa tunamfanya yeye kuwa kama kimiminika, na hicho si kingine zaidi ya MAFUTA. Roho Mtakatifu anakuja kwetu kama MAFUTA. Ni vema kulitambua hilo!
Sasa si watu wote wanayo mafuta yote ya Roho Mtakatifu kama Bwana Yesu alivyokuwa,. Leo tutaona aina mbalimbali za mafuta hayo, kisha tujitahidi tuyapokee yote kwa msaada wa Roho.
Haya yanapatikana katika UMOJA.
Zaburi 133:1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. 2 Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake.
Maana yake ni kuwa jinsi watakatifu wanavyoshirikiana pamoja kwa umoja, rohoni, yanaonekana ni mafuta mengi yanashuka katikati yao, mengi kiasi cha kufika hata katika upindo wa mavazi. Wanatiwa mafuta, na hayo ni ya nguvu. Kwasababu palipo na umoja ndipo penye nguvu.
Na ndio maana siku ile ya pentekoste, Mungu aliwakutanisha kwanza mahali pamoja wakawa wapo orofani pale sio katika kupiga zoga, hapana, bali katika kusali na kuomba, na kutafakari maneno ya Bwana(Matendo 1:12-14). Na ghafla, wakashangaa, katika siku ya kumi, Roho Mtakatifu amewashukia wote wakajazwa nguvu. Wakawa mashahidi wa Bwana tangu siku ile na kuendelea (Matendo 2).
Jambo kama hilo utalithibitisha tena katika Matendo 12:14, walipokuwa wamekaa pamoja kumwomba Mungu, mahali pale pakatikiswa, wajazwa Roho Mtakatifu wakanena Neno la Mungu kwa ujasiri. Hivyo hivyo na sisi tupenda ushirika na wengine, hususani katika kuomba na kufunga. Tukiwa watu wa namna hii tutajazwa mafuta haya na tutapokea ujasiri mwingi sana katika wokovu wetu.
Soma (Mhubiri 4:12)
Haya yanapatikana katika usafi na utakatifu.
Waebrania 1:8 Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi,Mungu,ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. 9 Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio
Shangwe ni ile furaha iliyopitiliza, inayodhihirika hata mpaka kwa nje. Halikadhalika Roho Mtakatifu naye anayo shangwe yake, ambayo hiyo inazidi hata hii ya kidunia, kwasababu ya kwake inakufanya ufurahi sio tu katika raha bali mpaka katika majaribu. (Luka 10:21)
Kwamfano utaona Bwana Yesu alikuwa nayo hata pale msalabani.
Wakolosai 2:15 akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.
Tukiwa watu wa kupenda haki(utakatifu), mafuta haya Roho anayaminina, mioyoni mwetu. Maisha yetu yanakuwa ni ya furaha tu, daima, vipindi vyote. Haijalishi mauvimu, kero, udhia, yataonekana kwa nje, lakini rohoni ni shangwe nyingi za Roho Mtakatifu, ndivyo Mungu alichokiweka ndani ya Kristo na kwa wakatifu wa kale ( Matendo 13:52, Waebrania 11:13, , Mathayo 5:12).
Hivyo Tuchague kupenda maisha ya haki ili tuyapate mafuta haya. Ni muhimu sana, ukipoteza furaha ya wokovu, huwezi kusonga mbele.
Haya yanaachiliwa katika kulitunza Neno la Mungu ndani yako.
1Yohana 2:26 Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. 27 Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.
Kumbuka biblia ni sauti ya Mungu katika maandishi, hivyo unavyoiweka moyoni mwako, ndivyo inavyoumbika na kuwa sauti kamili ya Mungu. Na hiyo ndio itakayokufudisha, na kukusaidia kupambanua, ikiwa wewe ni mkristo na una miaka mingi katika wokovu halafu hujawahi kuisoma BIBLIA yote, bado kuna viwango Bwana hawezi kusema na wewe. Lakini Unavyozidi kujifunza Neno ndivyo mafuta haya yanavyoachiliwa ndani yako kukufundisha. “Huna Neno, huna sauti ya Mungu”
Haya huachiliwa katika kuwekewa mikono na wakufunzi wako, au kuombewa na kanisa (wazee wa kanisa).
Huu ni utaratibu mwingine Mungu ameuachilia, katika kanisa, vipo vitu ambavyo huwezi kuvipokea wewe tu mwenyewe. Bali kutoka kwa waliokutangulia kiimani.
Elisha alitiwa mafuta na Eliya, akasimama mahali pake kihuduma (1Wafalme 19:15-16)
Musa aliwatia mafuta wale wazee 70, sehemu ya roho yake ikawaingia (Hesabu 11:16-25)
Daudi na Sauli wote walitiwa mafuta ya Samweli, ndipo wakapokea nguvu kutoka kwa Mungu, kutumika. (1Samweli 15:1, 16:12,)
Vilevile Timotheo, aliwekewa mikono na mtume Paulo (2Timotheo 1:6), akapokea neema ya kuyasimamia makanisa ya Kristo, mahali pa Paulo.
Vivyo hivyo na wewe usikwepe, wala usimdharau kiongozi wako wa kiroho, hata kama atakuwa ana madhaifu. Anayo sehemu yake aliyopewa na Mungu kwa ajili yako. Jinyenyekeze omba akuwekee mikono neema ya Mungu ijae ndani yako ya kuhudumu, ili Bwana akunyanyue katika viwango vya juu zaidi.
Hivyo kwa kuzingatia aina hizo 4, tukazipokea basi tutamsogelea Bwana katika mafuta mengi sana ya juu. Mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo. Roho Mtakatifu atajifunua zaidi ndani yetu.
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?
Nini maana ya’Shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo’Ayubu 20:4
Wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza
Je tunaruhusiwa kujipaka mafuta au kujipulizia marashi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2023/11/11/kuwa-na-mafuta-yote-ya-roho-mtakatifu-ndani-yako/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.