Kunyoa denge ni kufanyaje na je ni dhambi? (Walawi 19:27).

by Admin | 9 January 2024 08:46 am01

Jibu: Tusome,

Walawi 19:27 “Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu”.

“Denge” ni mtindo wa kunyoa nywele kwa kuziacha nyingi upande wa juu (katikati) na kuziacha chache au kuzimaliza zote kwa upande wa chini (kuzunguka kichwa), kwa lugha ya sasa ni maarufu kama “Panki”.

Zamani sana nyakati za biblia mtindo huu waliokuwa wananyoa walikuwa ni watu wanaoabudu miungu, (wakiamini kwa kunyoa vile basi watajikinga na madhara Fulani ya kiroho), lakini siku zilivyozidi kwenda mtindo huu ulikuwa unatumiwa na watu wa ulimwengu kama fasheni, kiasi kwamba walionyoa hivyo basi walikuwa wanajulikana kama “wahuni” (wenye lengo la kupalilia zinaa na uasherati)  , lakini zama hizi mtindo huu unatumiwa na watu wote, hadi wachungaji!!, na hauonekani kuwa ni tatizo.

Sasa swali ni je! Ni dhambi kunyoa denge/panki?

Jibu ni Ndio!..na itabaki kuwa ndio pasipo kujalisha ni watu wangapi wanafanya hivyo..

Na kwanini ni kosa?…kwasababu ile ile ya kuchanja chale..

Walawi 19:27 “Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. 

28 MSICHANJE CHALE YO YOTE katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana”.

Mtu anayenyoa denge, na anayechanja chale.. NI MAMOJA! Zote ni alama katika mwili ambazo zilitambulisha ibada Fulani, na mpaka leo zinafanya kazi hiyo hiyo… ni agano kamili katika mwili wa mtu linalohubiri ibada za miungu, haijalishi mtu huyo anajua au hajui..ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kufuatilia historia ya kitu kabla ya kukitumia kitu hicho/ mtindo huo…

Kwasababu si kila mtindo unaokubaliwa na wengi ni wa kiMungu, wala si kila desturi inayokubaliwa na kutumiwa na wengi ni ya kiMungu, nyingi ya tamaduni, desturi na mitindo ya kimaisha asili yake ni adui.

Na huwezi kukitumia kidonge chenye lengo la matibabu kama PIPI kwasababu tu kina utamu, halafu kisiwe na madhara kwako, vile vile huwezi kutumia elimu ya shetani au malighafi za shetani na kuzifanya mtindo, au urembo, halafu zisiwe na madhara kwako!..

Chale ni tiba ya shetani, denge ni tiba ya shetani, mitindo hiyo ilibuniwa na yeye kufanya tiba za kishetani… hivyo zinapotumiwa kama urembo! au fasheni! Ni kweli zitaleta mvuto kwa macho ya nje ya kibinadamu lakini zitabaki kubeba madhara yale yale katika kiroho. Ndio maana biblia ikakataza tusinyoe denge!.

Na hii sio sheria, kwamba ni agano la kale..na sasa tupo agano jipya hivyo kila kitu ni ruksa… Suala la ibada kwa miungu migeni litabaki kuwa katazo kwetu kwa nyakati zote.. Na denge, pamoja na chale ni ibada hizo…kama vile unavyoikimbia chale vile vile ikimbie kimbia denge.

Wala usiseme “ni nywele tu hazina maana”…Nywele zako zinamaana sana kiroho, ndio maana Bwana amekukataza usinyoe denge.. Bwana YESU alisema maneno yafuatayo..

Mathayo 10:30  “lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote”

Na tena alisema katika Luka..

Luka 21:18  “Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu”

Sasa kama nywele za vichwa vyetu Mungu hazitazami wala hashughuliki nazo..basi atakuwa mwongo aliposema hapo kuwa “zimehesabiwa zote na tena hakuna hata moja itakayopotea”.. Lakini kama Mungu ni kweli, basi pia nywele zetu ni lazima tuziweke kama atakavyo..

Ukizipunguza punguza kama unavyotaka wewe unaharibu mahesabu ya kimbingu, ukizisuka suka na kuziongezea marasta unaharibu mahesabu ya kimbingu, na hivyo unajiingiza katika mahesabu ya kishetani.

Hivyo usinyoe denge mtu wa Mungu,  wala usisuke marasta…kama miaka ya zamani (katika biblia)mtu aliyenyoa denge alionekana ni mshirikina, iweje leo dunia ikuhubirie wewe ni mtakatifu?..kama miaka ya nyuma tu mtu aliyenyoa denge(panki) alionekana muhuni, iweje leo hii dunia ikuambie kuwa sio ni urembo?.. Huoni kama kuna udanganyifu mkubwa unaondelea sasa kutoka kwa adui..

Usiangalie ni idadi kubwa kiasi gani ya watu wananyoa denge, au wanasuka rasta na kuamini kuwa ni sawa, wewe liangalie Neno la Mungu..kwani nyakati tunazoishi ni za hatari.

Bwana akubariki.

Ikiwa bado hujaokoka fahamu kuwa Siku ya Wokovu ni leo, wala usingoje kesho.. kwa msaada wa kuongozwa sala ya kumkiri BWANA YESU basi fungua hapa >>>KUONGOZWA SALA YA TOBA

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Je kwa mkristo aliyeokoka, ni dhambi kunyoa ndevu zake?

Je! kuchora tattoo ni dhambi?

UMETEKWA NA UPENDO WA KRISTO?

Nini maana ya mbingu na nchi zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamwe? (Mathayo 24:35).

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/01/09/kunyoa-denge-ni-kufanyaje-na-je-ni-dhambi-walawi-1927/