Wale waliowekewa tayari ufalme ni akina nani?. (Mathayo 20:23).

by Admin | 19 January 2024 08:46 am01

Swali: Je wale waliowekewa tayari ni akina nani na kwanini Bwana Yesu aseme maneno yale?


Jibu: Tuanzie kusoma mstari wa 20..

Mathayo 20:20 “Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno.

21  Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.

22  Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.

23  Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, SINA AMRI KUWAPA, BALI WATAPEWA WALIOWEKEWA TAYARI NA BABA YANGU”.

Ili tuelewe vizuri, hebu tafakari mfano huu.. “wanafunzi wawili wamemfuata mwalimu wao wa darasa na kumwomba washike nafasi ya kwanza kitaifa na mwingine ashike ya pili kitaifa katika mitihani yao ya mwisho wa kuhitimu”.. Unadhani jibu la mwalimu litakuwa ni lipi?..

Bila shaka mwalimu atawauliza.. je! Mtaweza kusoma kwa bidii??.. Na kama wale wanafunzi watajibu NDIO!.. Bado Mwalimu hataweza kuwapa hizo nafasi, bali atawaambia mimi sina mamlaka ya kuwapa bali “Wasahishaji watakaosahisha mitihani ya wote ndio watakaotoa majibu ya mitihani yenu na kuwapanga kama mmestahili hizo nafasi au la”..

Ndicho Bwana YESU alichowaambia hawa wana wa Zebedayo!.. ambao walienda kumwomba nafasi ya kuketi pamoja naye katika kiti chake.. na jibu la Bwana YESU likawa, ni “kukinywea kikombe”.. maana yake kukubali mateso kwaajili yake!.. Na wao wakajibu “wataweza”.. Lakini jibu la Bwana likawa “Nafasi hizo watapewa waliowekewa tayari”..maana yake waliostahili.

Na hao waliostahili ni akina nani?

Ni wale watakaofanya vizuri Zaidi ya wengine wote katika mambo yafuatayo.

   1. KUKINYWEA KIKOMBE.

Kikombe alichokinywea Bwana Yesu ni kile cha Mateso ya msalabani (Soma Mathayo 26:39), kutemewa mate, kupigwa Makonde, kuvikwa taji ya miiba, na kugongomelewa misumari mikononi..

Na yeyote ambaye atakubali kuteswa kwaajili ya Kristo, na si kwaajili ya mtu au kitu kingine chochote, basi yupo katika daraja zuri la kumkaribia Kristo katika siku ile kuu.

  2. KUBATIZWA UBATIZO WA BWANA YESU.

Marko 10:38  “Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au KUBATIZWA UBATIZO NIBATIZWAO MIMI?”

Swali Ubatizo aliobatizwa Bwana YESU KRISTO ni upi?…. si mwingine Zaidi ya ule wa kufa, kuzikwa na siku ya tatu kufufuka, na kupaa juu (soma  Luka 12:50), Na ubatizo huu mpaka sasa hakuna rekodi ya wazi ya yoyote aliyeupitia..

Ubatizo tubatizwao sasa ni ule wa maji mengi, ambao ni ishara ya kufa na kufufuka na Kristo (Wakolosai 2:12), kwamba tunapozamishwa katika maji mengi na kuibuka juu, ni ishara ya kufa pamoja na Kristo na kufufuka pamoja naye… Lakini Ule hasa wa kufa na kufufuka na kupaa, hakuna rekodi ya wazi ya aliyeupitia.

Isipokuwa unawezekana ndio maana tunasoma katika Ufunuo 11, kuwa wale washahidi wawili, ni miongoni mwa watakaoupitia..

Ufunuo 11:10 “….Nao wakaao juu ya nchi wafurahi juu yao na kushangilia. Nao watapelekeana zawadi wao kwa wao, kwa kuwa manabii hao wawili waliwatesa wao wakaao juu ya nchi.

11  NA BAADA YA SIKU HIZO TATU U NUSU, roho ya uhai itokayo kwa Mungu ikawaingia, wakasimama juu ya miguu yao; na hofu kuu ikawaangukia watu waliowatazama.

12  WAKASIKIA SAUTI KUU KUTOKA MBINGUNI IKIWAAMBIA, PANDENI HATA HUKU. WAKAPANDA MBINGUNI KATIKA WINGU, ADUI ZAO WAKIWATAZAMA”.

Je umempokea YESU?, Fahamu kuwa tunaishi katika siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

USIWE ADUI WA BWANA

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?

UWE KIKOMBE SAFI 

Nini maana ya kikombe cha maji ya baridi(Mathayo 10:42)?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/01/19/wale-waliowekewa-tayari-ufalme-ni-akina-nani-mathayo-2023/