Roho ya Malipizi/ roho za malipizi ni nini?

by Admin | 5 March 2024 08:46 pm03

Swali: roho za Malipizi ni nini na mtu anawezaje kuzifunga?


Jibu: roho ya Malipizi au roho za malipizi ni roho zinazojilipiza kisasi baada ya kushindwa vita.

Maandiko yanasema vita vyetu sisi si juu ya damu na nyama, bali juu ya falme na mamlaka za giza katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”.

Sasa hizi roho za mapepo na za wakuu wa giza, zinaposhindwa vita dhidi ya mtu, au watu, au kanisa basi, huwa zina tabia ya kukimbilia kutafuta sehemu nyingine iliyo dhaifu ya huyo mtu, au watu au kanisa na kushambulia ili kumwumiza yule aliyekuwa anashindana nazo.

Tuchukue mfano, mtu mmoja aliyeokoka ameomba kwaajili ya familia yake (Labda kwajili ya Mke wake au Mume au watoto), na katika kuomba kwake, ameomba ulinzi, na neema ya kumjua Mungu, na Zaidi sana amezikemea roho zote zinazopambana na familia yake, (roho za kurudi nyuma, roho za magonjwa na matatizo mengine) na amezishinda kwa maombi na kuziadhibu sawasawa na 2Wakorintho 10:6.

Sasa roho hizo (za mapepo na wakuu wa giza) zinapoanguka na kushindwa namna hiyo, huwa zina tabia ya kulipiza kisasi…kwa wakati huo zinaondoka na kwenda kutafuta sehemu nyingine ya maisha ya huyo mtu zilizo dhaifu na kuzivamia au kufanya nazo vita kutokana na uchungu na hasira za kushindwa..

Ndio hapo zitaacha kushughulika na familia ya huyo mtu kwa muda, na kwenda kupiga marafiki wa karibu wa huyo mtu, au wazazi, au watu wengine wowote walio wa muhimu katika maisha ya huyo mtu, lengo ni ili kumwumiza huyo mtu au kumsumbua na zinaweza kwenda kupiga kwa magonjwa, hasara au hata mauti kabisa..

Hivyo ni muhimu sana kumalizia maombi kwa kuomba ulinzi kwa watu wote walio karibu nawe ili wazidhurike na ghadhabu za hizo roho.

Hiyo siku zote ndio tabia ya shetani na majeshi yake, “kujilipiza kisasi”

Sasa  pengine utauliza ni wapi katika biblia jambo kama hilo limetokea?..tusome maandiko yafuatayo..

Ufunuo 12:7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;

8  nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.

9  Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.

10  Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.

11  Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.

12  Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! KWA MAANA YULE IBILISI AMESHUKA KWENU MWENYE GHADHABU NYINGI, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu”.

Umeona hapo mstari wa 12, maandiko yanasema yule ibilisi aliposhindwa alitupwa chini mwenye ghadhabu nyingi, na anashuka kujilipiza kisasi kwa kufanya vita na hao wakaao juu ya nchi na bahari kutokana na kushindwa kwake vita mbinguni. Na hapa tumeshapata jibu kwanini shetani anafanya vita na sisi wanadamu?.. sababu si nyingine Zaidi ya kisasi alichonacho, lakini ashukuriwe Kristo YESU Bwana wetu yupo katika mkono wa kuume akituombea (Warumi 8:34) .

Lakini tukizidi kusoma maandiko hayo mpaka ule mstari wa 17  bado tunaendelea kuona kisasi cha shetani baada ya kushidwa tena vita dhidi ya yule ya yule mtoto (YESU KRISTO) na dhidi ya yule mwanamke (Israeli).

Ufunuo 12:13 “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14  Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.

15  Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.

16  Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.

17  Joka akamkasirikia yule mwanamke, AKAENDA ZAKE AFANYE VITA JUU YA WAZAO WAKE WALIOSALIA, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari”.

Umeona tena hapo?.. baada ya Ibilisi kumshindwa “mtoto na yule mwanamke” anapanga tena malipizi juu ya uzao wake, hiyo yote ni kuonyesha roho mbaya ya kisasi aliyonayo adui.

Vivyo hivyo, mpaka leo hiyo roho anayo pamoja na mapepo yake, yakishindwa vita yanaenda kutafuta wengine kumalizia hasira zao, kwahiyo ni muhimu sana pia kuomba maombi ya kufunga na kuzuia hizo roho zisiende kuleta madhara sehemu nyingine ya maisha ya watu unaohusiana nao!.

Na huu ndio umuhimu wa kuwaombea wengine, na pia ndio umuhimu wa kuomba.. Usipokuwa mwombaji na kusubiri kuombewa tu mara kwa mara, upo katika hatari ya kuvamiwa na maroho ya malipizi kutoka katika kila kona (kutokana na maombi ya wengine) endapo hawatafunga hizo roho. Kwahiyo ni muhimu sana kuomba na kuwaombea wengine.

2Wakorintho 10:4 “(maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

6  tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia”

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

USILIPIZE KISASI.

UFUNUO: Mlango wa 12

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/03/05/roho-ya-malipizi-roho-za-malipizi-ni-nini/