USILIPIZE KISASI.

USILIPIZE KISASI.

Kwanini hatupaswi kujilipiza kisasi?… Kwasababu maandiko yanatufundisha kuwa kisasi ni juu yake yeye atalipa.

Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, KISASI NI JUU YANGU MIMI; MIMI NITALIPA, ANENA BWANA.

20 Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake”.

Tabia ya kujilipiza kisasa Bwana Mungu aliikataa tangu Mwanzo na Bwana Yesu akaja kuithibitisha tena katika Mathayo 5.

Tunaona baada ya Kaini kumwua ndugu yake Habili kwasababu ya wivu, Mungu alimlaani Kaini kwa kosa lile..

Lakini Mungu hakumwua Kaini bali alimlaani juu ya ardhi kwamba ataendelea kuishi lakini ardhi itamkataa… Kila kilimo atakachokifanya juu ya ardhi hakitafanikiwa, ndio maana baada ya pale hatuoni Kaini na uzao wake wakiendelea na kazi yake ya ukulima badala yake tunasoma wanaanza kutengeneza vyuma, na wapiga filimbi (Mwanzo 4:17-22).

Sasa baada ya Bwana Mungu kumlaani Kaini alijua kabisa kuna watu watakuja kusikia habari zake kwamba ni mwuaji, na pia kalaaniwa na Mungu, hivyo watataka wajichukulie hukumu aidha ya kumwua au kumnyanyasa…

Sasa Mungu kwa kulijua hilo, akamwekea Kaini alama, ili kila mtu atakayemwona asimguse…

Na alama hiyo ikaendelea kuwepo juu ya Kaini na uzao wake, iliyowatofautisha uzao wa Kaini na uzao mwingine.

Na Bwana akasema mtu atakayemwua Kaini, basi atalipwa kisasi mara 7,

Mwanzo 4:13 “Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

15 BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga”

Hivyo watu walivyosikia hivyo wakaogopa kumnyooshea mikono yao Kaini, kwasababu walijua kuna adhabu kubwa sana katika kufanya hayo…

Umeona?..Kumbe kisasi na hasira ndani ya maisha ya mtu ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu..
Ndivyo maandiko yanasema…

Mithali 24:17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18 BWANA asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”.

Ikiwa na maana kuwa kama adui yako amekutenda mabaya na wewe usimrudishie yale mabaya, mwombee Bwana ambadilishe, itakuwa heri kwako…na utasikia ule mzigo umeondoka ndani yako…

Lakini kama ukifikiri kwamba njia ya kuondoa mzigo (uchungu) ndani yako ni wewe kujilipiza kisasi, nataka nikuambie kuwa ndio utauongeza badala ya kuupunguza, kwasababu utakayemlipa kisasi utakuwa umeweka uadui naye hivyo shetani anaweza kumtumia tena kufanya jambo lingine kwa wakati mwingine kwa njia nyingine…lakini lililo baya zaidi ni kwamba utakuwa umekosana na Mungu pia.

Sasa nini kifanyike ili kuishinda nguvu ya kisasi ndani yako?

1. Wokovu.

Wokovu ndio mlango wa Imani. Ni lazima kumwamini Yesu na kumkiri.


2. Maombi (yanayoambatana na mifungo).

Baada ya kuokoka ni lazima uwe mtu wa maombi. Maombi yatakufanya uwe na nguvu za kiroho ambazo zitakusaidia wewe kushinda dhambi.

3 .Kusoma Neno.

Neno la Mungu (biblia) litakusaidia kukujenga utu wako wa ndani. Kwamfano Neno lifuatalo ukilijua litakusaidia wewe kutolipiza kisasi.

Mhubiri 7:21 “Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.

22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine”.

Mambo haya matatu ukiyazingatia sana basi Nguvu ya kisasi haiwezi kufanya kazi ndani yako, utakuwa mtu wa kusamehe na kuombea wanaokuudhi, na mengine kumwachia Bwana, na hivyo utu wako wa ndani utajengeka sana.

Maran atha!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?

KISASI NI JUU YA BWANA.

Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?

SADAKA INAKOMESHA LAANA!

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments