SADAKA INAKOMESHA LAANA!

SADAKA INAKOMESHA LAANA!

Karibu katika mfululizo ya masomo yahusuyo matoleo!

(Ifahamu Nguvu iliyopo katika Sadaka)

Tangu Adamu aanguke ardhi ilianza kulaaniwa; kila siku laana ilikuwa inajiongeza juu ya laana, ndio maana utaona Mungu alimwambia Adamu ardhi imelaaniwa kwaajili yake yeye na uzao wake (Mwanzo 3:17), lakini ukizidi kusoma utaona tena ardhi inalaaniwa mara ya pili kwa Kaini (Mwanzo 4:11).

Na desturi hiyo iliendelea juu ya wanadamu, (Maana yake kila kukicha ardhi ilikuwa inalaaniwa juu ya wanadamu, kutokana na maasi).

Lakini tunasoma alipozaliwa Nuhu maandiko yanamtaja kama mwana wa Faraja, atakayeikomesha laana iliyo juu ya ardhi.

Mwanzo 5:28 “Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana. 

29 Akamwita jina lake Nuhu, AKINENA, HUYU NDIYE ATAKAYETUFARIJI KWA KAZI YETU NA KWA TAABU YA MIKONO YETU KATIKA NCHI ALIYOILAANI BWANA”

Sasa unaweza kujiuliza ni wakati gani ambao Nuhu alileta faraja katika Nchi aliyoilaani Bwana?

Tusome Mwanzo 8:20-22.

Mwanzo 8:20 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 

21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, SITAILAANI NCHI TENA BAADA YA HAYO KWA SABABU YA WANADAMU, MAANA MAWAZO YA MOYO WA MWANADAMU NI MABAYA TANGU UJANA WAKE; WALA SITAPIGA TENA BAADA YA HAYO KILA KILICHO HAI KAMA NILIVYOFANYA. 

22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”

Umeona hapo? Baada ya Nuhu kumjengea Bwana madhabahu na kumtolea Bwana sadaka nzuri na ya kumridhisha, ndipo akaikomesha ile laana yote iliyokuwa inaendelea juu ya ardhi, kukawa hakuna tena kulaaniwa kwa nchi baada ya hapo!, ndio maana mpaka leo tunaona misimu ya mvua ipo, misimu ya kiangazi cha mavuno ipo, majira ya kuvuna na kupanda bado yapo, kama isingelikuwa ile sadaka Nuhu aliyoitoa huenda leo tungekuwa dunia ingekuwa mahali pabaya.

Lakini siri ya KUIKOMESHA HIYO LAANA!, Nuhu alifahamu ni kwa NJIA YA MATOLEO TU!..Na ni kanuni gani Nuhu aliyoitumia kutoa sadaka mpaka kufikia kuvunja misingi ya laana ya ardhi?

1.Alijenga Madhabahu.

Na sisi ni lazima tujenge madhabahu kwanza, na Madhahabu ya sasa, Agano jipya si ile ya mawe bali ni MIOYO YETU, Hiyo inapaswa iwe misafi kabla ya kufikiri kumtolea BWANA sadaka. Kwasababu maandiko yanasema sadaka ya mtu mbaya ni machukizo kwa Bwana (Mithali 15:8).

2. Kutoa vilivyo safi.

Baada ya Nuhu kutoka kwenye safina alitwaa wanyama walio safi tu na kumtolea Mungu, Na sisi ni lazima tumtolee Mungu vitu vilivyo visafi, hatupaswi kumtolea Mungu vitu vilivyopatikana kwa njia haramu kama ukahaba, dhuluma, rushwa, wizi, utapeli, na njia nyingine zote zinazofanana na hizo.

Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.”

3. Kutoa katika KILA kilicho safi!

Hii ni kanuni ya mwisho na ya muhimu sana, Ni lazima kutoa katika “KILA” kilicho safi, na si katika “BAADHI ya vilivyo safi”. Nuhu hakutoa tu Ng’ombe pekee yake kama sadaka, na kuwahifadhi mbuzi kwaajili ya chakula chake na biashara yake,  au hakutoa kondoo pekee yake, na kuwaacha kuku na mbuzi…bali alitoa katika vyote vilivyo safi, ikiwemo kondoo, mbuzi, ng’ombe, njiwa, kuku na vinginevyo.. kila kimoja kwa sehemu yake..Hiyo ikafanya sadaka yake kumridhisha Mungu, na hivyo kufuta laana zote zilizokuwepo juu ya nchi, ambapo mpaka leo tunakula matunda yake.

Na wewe una vitu gani vilivyo safi mbele za Mungu?, je katika vyote unavyovifanya huwa unafikiri kumtolea Mungu katika hivyo?, Je katika zawadi unazopewa ulishawahi kufikiri kumtolea Mungu sehemu ndogo katika hiyo?, au unafiki ni sehemu ya mshahara tu ndio Mungu anaitaka?!

Je katika mifugo yako yote ulishawahi kufikiri kumtolea Mungu sehemu ya hiyo? Usimtolee Mungu kuku na kuacha Mbuzi!.. Jaribu siku moja kumtolea mbuzi na kuku kwa pamoja, na uone matokeo yake, (Mungu ameruhusu tumjaribu kwa njia hiyo, Malaki 3:10).

Utaona laana zinavyoondoka juu yako!!.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).

Chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ndio kipi? (Matendo 21:25).

Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,

UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?

Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments