Watu wengi wanasoma biblia lakini si wote wanayafikia maneno SAFI YA MUNGU. Jambo ambalo watu wengi hatujui ni kuwa tunadhani, tunapoisoma biblia kwa mara moja, tayari tumeshayafikia “maneno safi ya Mungu”, yale yenye uwezo wa kubadilisha Maisha yetu katika ubora wote.
Ni vizuri ukafahamu hii biblia tunayoisoma, haipo wazi kama unavyodhani, ni kitabu kilichoficha maneno SAFI YA MUNGU (Pure word of God), Ambayo hayapatikani hivi hivi tu, kwa usomaji wa kawaida tuliouzoea sikuzote. Watu ambao wanauwezo wa kufikia hapa, basi Maisha yao ya kiroho yanakuwa na mageuzi makubwa sana, kutokana na nguvu ya Neno hilo.
Leo kwa neema za Bwana tutaona mtu anawezaje kuyafikia maneno haya;
Biblia imefananisha Neno la Mungu na madini ya fedha (Silver), sehemu nyingine na Dhahabu.
Sasa ukisoma, Zaburi 12:6 inasema..
Zaburi 12:6 “Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba”.
Maana yake ni kuwa, ili uweze kufahamu haya “Maneno safi ya Mungu” yanapatikanaje, unapaswa utazame jinsi Fedha/dhahabu safi, inavyopatikana na kusafishwa.
Kwa kawaida, madini haya yanapochimbwa, huwa hayang’ai kama unavyoona katika maduka ya VITO vya thamani. Bali yanakuwa kama miamba tu, au maudongo udongo, yaani dhahabu halisi inakuwa imechanganyikana sana na uchafu wa aina mbali mbali.
Hivyo wanachokifanya ili kuitoa takataka hizo katikati ya madini, ni kwenda kuiyeyusha katika joto kali sana. Hiyo inapelekea, uchafu kujitenga na fedha, kwani zile takataka zote zinapanda juu, na ile fedha/dhahabu, inabaki chini, kisha wanauzoa ule uchafu wote uliokuja juu, baadaye wanaicha igande tena kisha inatokea dhahabu yenyewe.
Sasa kwa kawaida,wafua fedha/dhahabu, wengine wanairudia hiyo hatua mara mbili au tatu, na kwa jinsi wanavyoirudia mara nyingi na kuondoa hata zile takataka ndogo sana, ndivyo, dhahabu hiyo inavyozidi kuleta mng’ao mzuri sana na wakuvutia sana.
Hivyo Mungu alitumia mfano huo kuonyesha pia jinsi NENO LAKE SAFI, linavyopatikana. Ni kama fedha iliyosafishwa MARA SABA katika moto,. Ikiwa na maana kuwa, zipo hatua saba, za kulifikia NENO safi la Mungu, alilokusudia limletee matokea makubwa katika Maisha yake..
Sasa hii mara saba, mtu anaifikiaje?
Ukiwa ni mtu wa kusoma biblia mara moja tu, na kujiona kuwa tayari umeshajua kila kitu, ufahamu kubwa hapo bado hujalifikia hili Neno safi la Mungu. Kulifikia kunahitaji utulivu, na pia kulitafakari tena na tena, na tena, na tena, kila siku, na sio kusoma tu kama gazeti.
Kwamfano leo unaweza kusoma habari za wana wa Israeli jinsi Mungu alivyowatoa katika nchi ya Misri, kwa mara ya kwanza ukaielewa kama stori tu, lakini ukigotea hapo, ukasema tayari nimeshaelewa hapo, sina haja ya kurudia tena siku nyingine.. Nakuambia biblia kwako itakuwa haina tofauti na vitabu kingine cha kihistoria ulichowahi kusoma huko nyuma.
Lakini ukasema siku nyingine nitatafakari, kisha ukamwomba Mungu, na kukaa katika utulivu ukairudia habari ile, utaona jambo jipya, limefunuliwa ndani yako, ambalo hukuwahi kulijua hapo mwanzo..
Wakati mwingine tena ukamwomba Roho Mtakatifu akusaidie, kisha ukarudia tena kusoma habari ile ile, utashangaa jambo lingine jipya unalipata ambalo siku za nyuma hukulipata..
Hivyo hivyo unavyozidi kuendelea, kurudia na kurudia ndivyo unavyolisafisha Neno la Mungu ndani yako,, Na matokeo yake ni kuwa, nguvu za Neno lake zinapenya katika roho yako, na kuleta mabadiliko makubwa sana, maishani mwako.
Shida inakuja pale, tunapodhani tumeimaliza biblia yote, pale tunaposoma habari Fulani na kujisemea moyoni, Aaah, tayari, yule kipofu Yesu aliishia kumpaka mate machoni akapona.. hivyo tunapita juu juu tu, kama sio kuiruka habari yote.
Wakati mwingine kanisani, unafundishwa, somo ambalo pengine ulishawahi kulisikia huko nyuma, na wewe badala ya kuwa mtulivu rohoni kusikiliza kwa makini, unasema, tayari hili nalifahamu..
Kumbuka, maneno safi ya Mungu, yanapatikana katika matanuru saba.
Hivyo natumai, kuanzia sasa sote, tutaacha kuwa wavivu wa kuyatafakari maandiko. Kwasababu lengo letu ni kuona nguvu za Neno la Mungu kweli zikifanya katika Maisha yetu ya wokovu. Tujitahidi sana kujifunza biblia.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.
EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.
Biblia inamaana gani kusema “vipo sita, naam saba”?
IEPUKE GHADHABU YA MUNGU.
DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.
Rudi nyumbani
Print this post
Amina mtumishi! Kama tukiwa hatusomi na kulitafakari Neno itakuwa rahisi kupeperushwa na kila upepo wa elimu!
Mungu wetu atuangazie Nuru yake.