MSALABA NI ZANA YA UJENZI WA MAISHA YAKO.

by Admin | 1 April 2024 08:46 pm04

Mwimbaji mmoja wa tenzi za rohoni aliandika hivi “Kama alivyoonyeshwa Yakobo zamani, msalaba umekuwa ngazi ya mbinguni (Tenzi no. 81, ubeti wa 2)”.. akirejea wakati ule  Yakobo alipokuwa amelala pale Betheli na akaona maono, ngazi kubwa kutokea mbele yake, na malaika wakikwea na kushuka kutoka mbinguni.

Mwanzo 28:11 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

12 Akaota ndoto; na tazama, NGAZI IMESIMAMISHWA JUU YA NCHI, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake…..

16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.  17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, NAPO NDIPO LANGO LA MBINGUNI”.

Na ufunuo wa ngazi hiyo ni MSALABA.. Hakika! Kupitia msalaba wa YESU tunafika mbinguni, kupitia ufunuo wa msalaba wa BWANA YESU maishani mwetu, na si shingoni mwetu, tutamwona MUNGU!..

Lakini nataka pia tuutafakari msalaba kwa jicho lingine, kama “ZANA YA KUJENGEA MAISHA”. Hebu turejee kisa kimoja katika biblia kilichomhusu Nabii Elisha pamoja na wana wa manabii na kisha tutauelewa Zaidi msalaba wa BWANA.

2Wafalme 6:1 “Kisha, wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu.

2 Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni.

3 Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.

4 Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti.

5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.

6 Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. AKAKATA KIJITI, AKAKITUPA PALE PALE, CHUMA KIKAELEA.

7 Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa”

Nataka tuutafakari huo mstari wa sita..“AKAKATA KIJITI, AKAKITUPA PALE PALE, CHUMA KIKAELEA”.

Hiki kijiti ni NINI?, na Chuma ni nini?

Chuma ni zana ya ujenzi, kumbuka huyu mtu alikuwa anakata mti kwaajili ya ujenzi ya makazi, na kwa bahati mbaya kichwa cha shoka kikaangukia majini, na shoka halikuwa la kwake bali aliazima tu!. Hivyo kazi ya ujenzi wa makazi yake ikasimama, na vile vile akabaki na deni ya kulipia kile kifaa.

Huenda shoka lako likawa ni elimu uliyo nayo, ambayo pengine kupitia hiyo ndio umefikiri kujenga maisha yako, au kazi uliyo nayo ambayo kupitia hiyo ndio unafikiria kujenga maisha yako, na makazi yako..Huenda shoka lako ni kipawa au uwezo Fulani ulionao ambao kupitia huo unaamini kazi yako itaisha salama.

Nataka nikuambie wakati unafikiri Elimu yako ni chuma kigumu cha kujenga maisha, au kazi yako ndio chuma kigumu cha kujenga maisha yako, au utashi wako ndio chuma kigumu cha kuchonga maisha yako..usisahau kuwa yapo maji pembeni yako!!!, na hiko chuma saa yoyote kitazama..na kile ulichotazamia kukikamilisha kitasimama, na hata kupata hasara kubwa ya madeni.

Sasa kitu pekee kinachoweza kutoa chuma ndani ya maji, hata kielee, si winchi, au sumaku, au kifaa kingine chochote chenye uwezo…bali ni KIJITI KIDOGO TU!.. Na kijiti hiko si kingine Zaidi ya MSALABA BWANA YESU!!.

(Kumbuka msalaba wa Bwana YESU si Rozari shingoni, au sanamu madhahabuni, au mti wa msalaba juu ya kaburi, bali ni ufunuo wa Mauti ya YESU moyoni)…Maana yake wokovu unaopatikana kupitia uelewa wa mauti ya BWANA YESU…ambao huo unazaa mtu kujitwika msalaba wake na kumfuata yeye.

Marko 8:34  “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35  Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.

Je! msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako??, Umeubeba msalaba wako na kumfuata yeye??.. Au unajitumainisha na chuma ulicho nacho!..ukiamini kuwa elimu yako itakuokoa, au kazi yako, au cheo chako.. Hivyo vyote ukiwa navyo na KRISTO HAYUPO MOYONI MWAKO, UNAFANYA KAZI BURE!!!.

Na tena ni heri ukose hivyo vyote, Ukose elimu, ukose kazi, ukose cheo, ukose kila kitu…lakini msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako, kuliko kuwa na vyote hivyo halafu huna YESU moyoni!!…NI HASARA KUBWA!!!

Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa BWANA YESU leo, kama bado hujafanya hivyo, na BWANA ATAKUSAIDIA, Ikiwa utahitaji msaada huo wa kumpokea YESU, basi waweza wasiliana nasi na utapata msaada huo…

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ONA FAHARI JUU YA BWANA.

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

NJIA YA MSALABA

Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?

UTHAMINI WITO WA PILI WA YESU ZAIDI YA ULE WA KWANZA.

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/04/01/msalaba-ni-zana-ya-ujenzi-wa-maisha-yako/