by Admin | 3 August 2024 08:46 am08
Swali: Katika Yohana 5:22 na 27 tunaona biblia inasema kuwa Mungu amempa Mwana (Yaani Bwana Yesu) hukumu yote…. lakini tukiruka mpaka ile sura ya 12:47 tunaona tena Bwana YESU anakanusha kuwa yeye hamhukumu mtu?.. Je biblia inajichanganya hapa?.
Jibu: Awali ya yote ni muhimu kufahamu kuwa Biblia ni kitabu kilichovuviwa na Roho Mtakatifu, hivyo kamwe hakina makosa…kinachoonekana kinajichanganya si Biblia, iliyo Neno la Mungu, bali ni tafakari zetu na pambanuzi zetu.
Sasa turejee mistari hiyo..
Katika Yohana 5:22 “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, BALI AMEMPA MWANA HUKUMU YOTE………….
27 Naye AKAMPA AMRI YA KUFANYA HUKUMU kwa sababu ni Mwana wa Adamu”.
Hapa ni kweli Mwana kapewa mamlaka yote ya kufanya hukumu… Tusome tena ile Yohana 12:47..
Yohana 12:47 “Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, MIMI SIMHUKUMU; MAANA SIKUJA ILI NIUHUKUMU ULIMWENGU, ila niuokoe ulimwengu”.
Tukisoma mistari hiyo kwa juu juu, ni rahisi kuona kuwa maneno hayo yanajichanganya… lakini kiuhalisia hayajichanganyi hata kidogo.. kwani ni suala la kuelewa lugha tu hapo!.
Katika Yohana 5:22, Baba amempa Mwana hukumu yote, maana yake Amri ya kuhukumu amempa yeye.. Maana yake mamlaka yote kapewa (Bwana YESU), kama vile Farao alivyompa Yusufu mamlaka yote ya Misri.
Sasa kama Bwana YESU kapewa mamlaka yote ya kufanya hukumu… ni chaguzi lake yeye ni nani amhukumu na nani asimhukumu, ni wakati gani afanye hukumu na ni wakati gani asihukumu…(kwasababu vyote vipo mikononi mwake).
Sasa kwasababu yote yamewekwa chini ya mapenzi yake, basi mapenzi yake ni “kumtomhukumu mtu yoyote duniani”…sawasawa na maandiko hayo ya Yohana 12:47.. ingawa anayo mamlaka hayo ya kumhukumu mtu yoyote duniani kwasababu kashapewa na Baba.
Lakini hakutumia huo uwezo, wa kupitisha hukumu duniani kwa wote waliomkataa au wanaomkataa sasa, bali anawavumilia mpaka siku ya mwisho.. Mfano mzuri unaomwonyesha Bwana akiwa ameizuia hukumu yake ni ile habari tunayoisoma katika Luka 9:52-56.
Luka 9:52 “akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. 54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?
55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]
56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”.
Huo ni mfano wa hukumu ambayo Bwana angeweza kuito kwa Wasamaria hao, lakini alizuia… utasoma tena jambo kama hilo hilo katika Mathayo 26:51-53.
Mathayo 26:51 “Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
52 Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.
53 AMA WADHANI YA KUWA MIMI SIWEZI KUMSIHI BABA YANGU, NAYE ATANILETEA SASA HIVI ZAIDI YA MAJESHI KUMI NA MAWILI YA MALAIKA?”
Kwahiyo ni kweli Bwana YESU amepewa hukumu yote, lakini hatumii uwezo wa hukumu yake yote, kwetu sisi tunaoishi sasa, laiti akifanya hivyo, hakuna mwenye mwili atakayepona.. Lakini anatuvumilia sana kwasababu hataki mtu yoyote apotee (2Petro 3:9).
Ila tukiudharau wingi wa huruma zake hizi, na kupuuzia Neema mpaka siku tunaondoka katika haya maisha au siku amerudi, basi tutahukumiwa na yeye pasipo huruma… Na atatuhukumu kupitia maneno yake hayo hayo.
Hivyo ndugu yangu, YESU sasa ni mwenye huruma na mvumilivu kwetu, lakini siku ile ya hukumu hatakuwa na huruma..kwahiyo si muda wa kudharau wema wake na uvumilivu wake kwetu, bali ni wakati wa kutengeneza maisha kabla ya ile siku ya hukumu..
Warumi 2:4 “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?
5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu,
6 atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake”
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
IKIWA MWENYE HAKI AKIOKOKA KWA SHIDA, MWENYE DHAMBI ATAONEKANA WAPI?
Tirano alikuwa nani na darasa lake lilikuwaje? (Matendo 19:9)
Mithali 24:17 inamaana gani kusema Tengeneza kazi yako huko nje?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/08/03/je-biblia-inajichanganya-kwa-habari-ya-hukumu-ya-mungu-yohana-1247-na-yohana-522-27/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.