by Admin | 2 December 2024 08:46 pm12
SWALI: Je! Paulo, alikuwa na injili yake, tofauti na wengine? sawasawa na (Warumi 2:16)
Warumi 2:16 katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.
JIBU: Katika habari hiyo mtume Paulo hakumaanisha kwamba anayo injili nyingine ya kipekee tofauti na mitume wengine wa Kristo, na kwamba ya kwake tu ndiyo Mungu atakayoitumia kuzihukumu siri za wanadamu.
Hapana mitume wote walikabidhiwa “injili moja”. Nayo ni kushuhudia wokovu ulioletwa duniani na mtu mmoja tu, ambaye ni YESU KRISTO, kwa lile tendo la kufa na kukufuka kwake kama fidia ya dhambi za ulimwengu, ambapo mtu akiamini basi amepokea ondoleo la dhambi na uzima wa milele. Na mtu yeyote ambaye hatamwamini huyu basi hukumu ya Mungu inakuwa juu yake.
Kwahiyo Paulo kama mmoja wa hao waliokabidhiwa injili hiyo, alikuwa na ujasiri kuwaeleza watu wale wa Rumi, kwamba kupitia injili yake hiyo sahihi, Mungu atawahukumu wanadamu, kwasababu anayehubiriwa ni Yesu Kristo. Ni sawa tu na Petro, au Yohana, au Yakobo, wangesema maneno kama hayo, wasingewezeka kupingana na Paulo kwasababu wanachokishuhudia wote ni kitu kimoja. Ndio maana tunaona maneno ya mitume wote, yameunganishwa katika kitabu kimoja kinachoitwa BIBLIA.
Lakini kwa nini Paulo aliongeze Neno hilo “sawasawa na injili yangu” Na asingeishia kwenye injili tu?.
Ni kwasababu wakati ule kulikuwa na watu waliomhubiri Yesu mwingine na injili nyingine, tofauti na ile waliyoihubiri mitume wa kweli. Na hawa watu, wengi wao walikuwa ni wayahudi wa tohara, Hivyo ilimbidi aliweke wazi hilo ili watu wabakie kwenye injili sahihi ya kweli.
Injili hizo Paulo aliziona kwenye makanisa kadha wa kadha kama tunavyosoma katika vifungu hivi;
2Wakorintho 11:4 Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!
Na..
Wagalatia 1:6 Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na
kugeukia injili ya namna nyingine. 7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.
Umeona, hiyo ndio sababu ya Paulo na kule Rumi kuitamka kauli hiyo, “sawasawa na injili yangu”. Ili kuwapa ufahamu kuwa hizo nyingine wanazozisikia huko nje, hazina uhai wowote wa kumwokoa mtu, au kumtetea siku ile ya hukumu.
Hata sasa, mambo ni yale yale, kumekuwa na madhehebu mengi, imani nyingi, ambazo zote zinadai ni za kikristo, lakini ukiangalia uhalisia wake humwoni Kristo ndani yake, wala injili ya Kristo. Fundisho lililo mule ndani sio fundisho la mitume. Watu hawahubiriwi tena toba ya kweli na kumwangalia Kristo kama kiini cha wokovu wao. Wanafundishwa mambo mengine kabisa wengine mafanikio, wengine uchawi, wengine miujiza n.k kama ndio utimilifu wa ukristo. Sasa mambo kama hayo, hayaweza kumtetea mtu siku ya hukumu.
Bali injili ya Yesu Kristo, kupitia mitume wake. Ambayo ni hii biblia tuliyonayo, ndio tunayopaswa tuiegemee, kwasababu katika hiyo ndio tutakayohukumiwa.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/02/sawasawa-na-injili-yangu-kwa-kristo-yesu-warumi-216/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.