by Admin | 10 July 2018 08:46 pm07
Danieli 4:
JINA LA BWANA wetu YESU KRISTO, Mkuu wa milki zote za dunia lihimidiwe.
Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Danieli;
Sura hii inaelezea Maono Mfalme Nebukadreza aliyoyaona na kumpelekea kubadili fikra zake na kuwa mtu mkamilifu mbele za Mungu, aliandika barua hii..
Danieli 4:1 Mfalme Nebukadreza, kwa watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wanaokaa katika dunia yote; Amani iongezeke kwenu.
2 Mimi nimeona vema kutangaza habari za ISHARA NA MAAJABU, aliyonitendea Mungu aliye juu.
3 Ishara zake ni kubwa kama nini! Na maajabu yake yana uweza kama nini! Ufalme wake ni ufalme wa milele; na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.
Hapa tunaona Nebukadreza anaanza kwa kushuhudia ISHARA na MAAJABU Mungu aliyomtendea alipokuwa amestarehe katika ufalme wake, tunajua siku zote jambo fulani Baya Mungu akitaka kulileta kwa mtu/watu kabla ya kulileta jambo hilo huwa anatanguliza ishara kwanza kama onyo, na kazi ya ishara ni kumfanya mtu atubu, kwamfano tunaona wakati wa kipindi cha Yona,
Kabla ya Mungu kuiangamiza Ninawi ndani ya siku 40, Mungu alitangulia kuwapa ishara kwanza ya Yona kukaa ndani ya tumbo la samaki siku tatu, ili watakapoiona ishara kama hiyo watubu,na wasipotubu wataangamizwa, lakini tunaona walitii na kutubu na Mungu akaghahiri kuleta ubaya ule.
Vivyo hivyo na kwa Nebukadreza katika utawala wake Mungu alishatangulia kumpa ISHARA nyingi ili aache uovu wake lakini hakutubu, Kwamfano ile ndoto aliyoota ya kwanza “ya sanamu KUBWA” ilikuwa ni ishara kuwa ufalme wake siku moja utaangushwa, hivyo amgeukie Mungu lakini hakufanya hivyo, na Mwishoni pia Mungu alimpa ISHARA nyingine ya ndoto juu ya ule mti mrefu sana, uliokatwa na kuachwa kisiki tu, ambao ulimuhusu yeye moja kwa moja ili atubu aache maovu yake lakini hakutubu..Na ndio maana hapa tunaona anashuhudia na kusema ISHARA ZAKE NI KUBWA KAMA NINI!!.
Pia tazama..
Licha ya Ishara alionyeshwa pia na maajabu, ambayo ni miujiza mfano wa ya akina Shedraka, Meshaki na Abednego ya kukaa katika moto mkali pasipo kuteketea, mambo ambayo hakuwahi kuyaona hata kwa wachawi wake aliokuwa nao Babeli na ndio maana alisema anaona vizuri kuandika maajabu Mungu aliyomtendea, yenye UWEZA MKUBWA.
Vivyo hivyo hata kwa mtu yeyote kabla ya Mungu kufanya jambo huwa anatanguliza kwanza ISHARA NA MAAJABU kama ONYO kumfanya mtu huyo atubu, lakini asipotubu mambo mabaya yatamkuta kama yalivyomkuta Mfalme Nebukadreza. Na kizazi tunachoishi sasa hivi kilishapewa ISHARA kama ya NINAWI ili kitubu na ishara hiyo si nyingine zaidi ya YESU KRISTO mwenyewe Ukisoma..
Mathayo 12:38-42″ Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.
39 Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ISHARA YA NABII YONA.
40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.
41 Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao WALITUBU kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona.
42 Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani. “
Na MAAJABU pia Mungu anatutenda, tunayaona kila siku katika maisha yetu, wafu wanafufuliwa, viwete wanatembea, vipofu wanaona, watu wanaponywa magonjwa yao, wenye UKIMWI, Cancer, magonjwa yasiyotibika yote yanapona, n.k. Hivi vyote Mungu anavifanya ili watu watubu na kumgeukia yeye, lakini wengi wanakimbilia kwa Mungu ili watendewe miujiza tu na sio kwa ajili ya TOBA, Lakini Bwana alisema…
Mathayo 11:20 -24 “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu HAIKUTUBU.
21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.
23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama MIUJIZA iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe. “
Kwahiyo dhumuni KUBWA la Mungu Kuruhusu ishara na maajabu sio kututimizia mahitaji yetu pekee, bali ni KUTUONYA na kutufanya TUTUBU, ili tusije tukaangukia hukumu, jiulize, Mungu amekufanyia Ishara na Maajabu mara ngapi katika maisha yako? na Je! yalikufanya wewe utubu na kuacha dhambi au umkaribie Mungu zaidi? Kama sivyo jitathimini tena.
Tukirejea kwenye ule mstari wa nne tunaona Nebukadreza aliendelea na kusema:
Danieli 4:4-17″
4 Mimi, Nebukadreza, nalikuwa nikistarehe katika nyumba yangu, nikisitawi katika nyumba yangu ya enzi.
5 Nikaota ndoto iliyonitia hofu; mawazo niliyokuwa nayo kitandani mwangu, na njozi za kichwa changu, zikanifadhaisha.
6 Basi nikatoa amri kwamba wenye hekima wote wa Babeli, waletwe mbele yangu, ili kunijulisha tafsiri ya ndoto ile.
7 Ndipo wakaingia waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu; nikawahadithia ile ndoto; wao wasiweze kunijulisha tafsiri yake.
8 Bali hatimaye Danieli akaingia mbele yangu, ambaye jina lake ni Belteshaza, kwa kufuata jina la mungu wangu; tena ndani yake inakaa roho ya miungu watakatifu; nikamhadithia ile ndoto, nikisema,
9 Ee Belteshaza, mkuu wa waganga, kwa sababu ninajua ya kuwa roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yako, na ya kuwa hapana neno la siri likushindalo, niambie njozi za ndoto yangu niliyoiona, na tafsiri yake.
10 Njozi za kichwa changu kitandani mwangu zilikuwa hivi; naliona, na tazama, palikuwa na mti katikati ya nchi, urefu wake mkubwa sana.
11 Mti ule ukakua, ukawa na nguvu, urefu wake ulifika mpaka mbinguni, na kuonekana kwake mpaka mwisho wa dunia.
12 Majani yake yalikuwa mazuri, na matunda yake mengi, na ndani yake chakula cha kuwatosha watu wote; wanyama wa kondeni walipata uvuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake; kila kitu chenye mwili kilipata chakula kwake.
13 Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, “MLINZI”, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni.
14 Akapaza sauti yake, akasema, Ukateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yapukusieni mbali majani yake, na kuyatawanya matunda yake, wanyama na waondoke hapo chini yake, na ndege katika matawi yake.
15 Walakini kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikapate maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama katika majani ya nchi;
16 moyo wake ubadilike, usiwe moyo wa binadamu, na apewe moyo wa mnyama; nyakati saba zikapite juu yake.
17 Hukumu hii imekuja kwa AGIZO LA WALINZI, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge. “
Baada ya Mfalme Nebukadreza kumsimulia Danieli ndoto hii, ndipo tunasoma Danieli mkuu wa waganga alimpa tafsiri yake na kumwambia ule mti mkubwa wenye nguvu ambao wanyama wote wa kondeni walipata uvuli chini yake, unamwakilisha yeye, na kwamba ulionekana umekatwa kwa agizo la WALINZI, ikiwa na maana kuwa ataondolewa katika enzi yake ya kifalme, naye atakaa mwituni na kula majani kama ng’ombe mpaka nyakati saba zitakapotimia ( yaani miaka 7), hadi hapo atakapofahamu kuwa aliye juu ndiye anayetawala falme zote za dunia.
Lakini tunaona pamoja na kupewa ISHARA hii na Danieli kumshauri ATUBU aache njia zake mbaya kwa kuwahurumia MASKINI, Hakutubu aliendelea kuwa na kiburi, kuwanyanyasa maskini na kutokuwa na huruma kwa watu, mpaka kiwango cha maovu yake kilipofikia kilele, tunasoma baada ya miezi 12 jambo hilo lilimtokea kama lilivyo.
Danieli 4:28-30″
28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.
29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.
30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?
31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.
32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.
33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.
AGIZO LA WALINZI:
Kama tunavyosoma habari hii kuwa kulikuwa na WALINZI mbinguni waliokuwa wanatazama mienendo yote Ufalme wa Nebukadreza, mema yake yote na mabaya yake yote aliyoyafanya, Kumbuka Hawa ni MALAIKA WATAKATIFU walioko mbinguni, wanaotazama kila cheo, nafasi au mamlaka mtu aliyonayo, je! anavitumiaje?. Kama mtu anatenda mema Mungu kwa mkono wa hao walinzi anakulipa, lakini kama unatenda maovu au unaitumia vibaya nafasi yako uliyopewa, Mungu kwa mkono wa hao walinzi utapokea HUKUMU. Na mambo hayo ni hapa hapa duniani kabla ya hukumu kuu ya siku ya mwisho.
Kama wewe ni Raisi fahamu tu kuna WALINZI mbinguni wanakutazama kama vile wale waliokuwa wanamtazama Mfalme Nebukadreza, kama wewe ni waziri,mbunge, mkuu wa mkoa, balozi, diwani, m/kijiji, mjumbe, n.k. fahamu tu wapo walinzi juu wanakutazama mienendo yako kama je unaenenda katika haki au la!..Kama wewe ni mchungaji, mwinjilisti, Nabii, mwalimu, shemasi, mwimba kwaya, mfanya usafi kanisani, mwandishi, n.k. fahamu tu wapo walinzi mbinguni wanakutazama kama je! unasimama katika njia ya haki au la!, Kama wewe ni baba, au mama, au mlezi au boss, jua tu kuna walinzi watakatifu mbinguni wakifuatilia nyendo zako kama kweli hao unaowalea unawatendea haki au la!….n.k.
Kwahiyo katika nafasi yoyote uliyopewa na Mungu ni muhimu kuendana nayo kwa umakini ukijua kuwa, hakuna mamlaka iliyojiweka yenyewe (Warumi 1:1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana HAKUNA MAMLAKA ISIYOTOKA KWA MUNGU; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.). Mfalme Nebukadreza alipuuzia hilo na kusahau kuwa anatazamwa juu na kwamba Bwana ndiye anayetoa mamlaka yote, matokeo yake thamani yake ikashushwa kuliko hata mnyama wa porini kwa muda wa miaka 7, lakini alipogundua kosa lake, alitubu na kuwa mnyenyekevu hivyo Mungu akamrehemu na kumrejeshea vyote na enzi kupita kiasi. Sasa huyu alifanyika kama mfano,neema hiyo inaweza isiwepo kwako, kama utatumia vibaya nafasi uliyopewa.
Ndipo Mfalme Nebukadreza alimalizia na kusema:
Danieli 4:34 Hata mwisho wa siku hizo, mimi, Nebukadreza, nikainua macho yangu kuelekea mbingu, fahamu zangu zikanirudia; nikamhimidi Yeye aliye juu, nikamsifu na kumheshimu Yeye aishiye milele; kwa maana mamlaka yake ni mamlaka ya milele, na ufalme wake hudumu toka kizazi hata kizazi;
35 na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?
36 Basi wakati uo huo fahamu zangu zikanirudia, na kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu, enzi yangu na fahari yangu zikanirudia; na mawaziri wangu, na madiwani wangu, wakaja kunitafuta; nami nikathibitika katika ufalme wangu, nikaongezewa enzi kupita kiasi.
37 Basi mimi, Nebukadreza, namhimidi Mfalme wa mbinguni, namtukuza na kumheshimu; maana matendo yake yote ni kweli, na njia zake ni za adili; na wale waendao kwa kutakabari, yeye aweza kuwadhili.
Kwahiyo ndugu kumbuka ishara na maajabu(ndoto, Maono, mafanikio, uponyaji, kuepushwa na mabaya, kutendewa miujiza Mungu anayokuonyesha ni kukutaka ufikie toba, utubie uasherati wako, ulevi wako, sanamu zako, vimini vyako, makeup zako na usengenyaji wako n.k. Pia usisahau katika nafasi uliyopewa wapo walinzi juu wanakutazama.
Ubarikiwe na Bwana Yesu.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Kwa Mwendelezo >>> MLANGO WA TANO:
Mada Nyinginezo:
ACHENI MJUE YA KUWA MIMI NI MUNGU.
MTI UANGUKAPO, PAPO HAPO UTALALA.
UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?
MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2018/07/10/danieli-mlango-wa-4/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.