Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za Mfalme Sauli kupata majibu kwa mwanamke mchawi?

by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09

JIBU:Shalom!. Ni vizuri tuifahamu sifa ya Mungu, ili tusiishie tu kumchukulia yeye yupo mbinguni kaketi kwenye kiti cha Enzi, mahali pengine popote palipo pachafu hawezi kuingia wala kukanyaga, wala kujua kinachoendelea huko.

Zaburi 139:7 “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. 9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. 11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; 12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”

Na ndio maana ukisoma ule mstari ule mstari wa 6 juu yake kidogo unasema hivi.. “Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.” Hii Ikiwa na maana kuwa uweza wa Mungu hautambulikani, na njia zake hazitafutikani hata tukijaribu kumtafakari Mungu vipi, hatuwezi kumpima kwa akili zetu hizi za kibinadamu kwa jinsi alivyoenea kila mahali.   Hiyo Inatuthibitishia kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kuwepo kila mahali, na ndio pekee mwenye funguo za makao ya viumbe vyote ulimwenguni,..hakuna mwingine yeyote mwenye uwezo huo.Kama tunavyofahamu..

Zipo falme Kuu tatu zinazotembea katika duara lote la uumbaji wa Mungu, Ufalme wa kwanza ni ufalme wa Mungu mwenyewe ambao huo upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme wa pili ni ufalme wa giza nao pia upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme ya tatu ni ufalme ya wanadamu ambao ndio huu tunaouona katika mwili na ndio huu tunaoishi mimi mimi na wewe.   Na falme hizi zote kila mmoja inayo utendaji kazi wake wenyewe, na nguvu zake, na mamlaka yake yenyewe, na kama zilivyojipanga ile Falme ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi mbali na nyingine zote ndiyo ya Mungu wetu, kisha hapo chini unafuata ufalme wa giza ambao ndio shetani anaumiliki, na wa mwisho ndio huu wa kwetu sisi wanadamu.   Sasa Yule mwenye nguvu zaidi ndiye mwenye uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ufalme wa chini yake.

Kwa mfano ufalme wa mbinguni ambao ndio wa Mungu wetu, unaouwezo wa kuamua lolote juu hizi falme mbili za chini, unaouwezo wa kuzitumia au kuziamurisha lolote la kufanya, zinaweza kutumiwa pia kutimiza kusudi Fulani la Mungu kwa muda kwa kipindi fulani. Vivyo hivyo na ufalme wa pili ambao ni wa giza unao nguvu wa kuumurisha ufalme wa chini yake (yaani sisi tunaouishi), kamwe mwanadamu hata afanyaje hawezi kuushinda ufalme wa ibilisi kama hana Mungu, atatawaliwa tu na falme hizo mbili, na ndio maana shetani naye alikuwa na ujasiri wa kujigamba mbele ya Yesu na kumwambia hivi vyote ni vyangu nami humpa yeyote nimtakaye na huku sisi tunajua kuwa dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Unadhani shetani alikuwa anajisifia bure?, hapana kwasababu ufalme wake ni kweli una nguvu zaidi ya ufalme wa wanadamu..

Hivyo alikuwa na haki ya kusema vile. Hali kadhalika ule ufalme ulio dhaifu hauwezi kuelewa mambo yanayoendelea katika ufalme ulio juu yake wenye nguvu hata uwe na bidii kiasi gani.   Hivyo ufalme wa ibilisi hauwezi kujua lolote linaloendelea katika ufalme wa Mungu, hata atafute kiasi gani hawezi kujua chochote.   Sasa Tukirudi kwenye swali lililoulizwa Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za mfalme Sauli .kupata majibu kwa mwanamke .mwenye pepo.nisaidie hapo.   Jibu ni Ndio Mungu anaoweza kuleta majibu sio tu kupitia ufalme wa giza, bali pia kupitia ufalme wa kibinadamu, Kwasababu yeye yupo mahali popote,.kama hapo juu anavyosema

Zaburi 139:8 “Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. ”  

Lakini yeye kuwa uwezo huo wa kupitisha ujumbe wake kupitia falme hizo zote mbili haimaanishi kuwa unampendeza au umemfikia Mungu kinyume chake ni hukumu inafuata…Pia hiyo haimaanishi kuwa mtu anapokwenda kwa mganga kumtafuta Mungu atamwona, kumbuka wote wanaokwenda kwa waganga hawana lengo la kumtafuta Mungu, hakuna hata mmoja, huwa wanakwenda kutafuta njia za kutatuliwa matatizo yao na wala sio kumtafuta Mungu,kama wangekuwa na lengo la kumtafuta Mungu wasingedhubutu kutumia njia hizo ambazo wanajua kabisa Mungu amezikataa. Hata Sauli mwenyewe hakwenda kumtafuta Mungu kule kwa mganga,bali samweli amsaidie kutatua ufumbuzi wa shida iliyo mbele yake..  

Na ndio huko huko Mungu wakati mwingine anatokea kuzungumza na watu, na ikishafika hatua kama hiyo basi ujue kuwa kinachofuata ni hukumu tu kwa kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.   Hata wachawi wenyewe huwa wanakutana na sauti ya Mungu huko huko katika shughuli zao zikiwaonya matendo yao, lakini hawawezi kusema siri hizo wanazo wao wenyewe, wale ambao wanakuja kuokolewa ukiwauliza watakuthibitishia hilo kwamba kuna wakati Fulani ambao Mungu alishawahi kuwaonya.  

Sio tu Sauli alikwenda kwa waganga..Yupo ambaye alikuwa ni mchawi kabisa biblia inamtaja naye ni Balaamu, nabii wa uongo, huyu naye Mungu alikuwa anazungumza naye akimwonya asiwalaani Israeli, lakini yeye hakusikia sauti ile ya Mungu akatia ukwazo kwa wana wa Israeli, Mungu baadaye akaja kumuua.   Hivyo huo uwezo Mungu anao,lakini sio njia Mungu anayoitumia kuleta majibu ya maombi wa watu. Njia yoyote nje ya Yesu Kristo, yaani njia ya sanamu, njia ya uganga, njia ya sayansi, hakuna hata moja yenyewe uwezo wa kufikisha maombi kwa Mungu, wala usijaribu kufanya hivyo utaangukia hukumu, isiyoponyeka. japo Mungu anaweza kuzitumia hizo kuleta majibu kwa watu tena majibu yaambatanayo na hukumu wala sio jambo jema.

Ubarikiwe.


Mada Nyinginezo:

JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.

JE! NI KWELI KUNA VIUMBE VINAVYOISHI SAYARI NYINGINE (ALIENS)?

BWANA YESU ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA; MAFARISAYO HUPANUA HIRIZI ZAO, NA KUONGEZA MATAMVUA YAO?

HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?

EPUKA KUTOA UDHURU.

MSTARI HUU UNA MAANA GANI? “TUPA CHAKULA CHAKO USONI PA MAJI; MAANA UTAKIONA BAADA YA SIKU NYINGI”. (MHUBIRI 11:1)


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/jemungu-anaweza-kuleta-majibu-kupitia-nguvu-za-giza-maana-nashindwa-kuelewa-ninaposoma-habari-za-mfalme-sauli-kupata-majibu-kwa-mwanamke-mchawi/