NYOTA ZIPOTEAZO.

by Admin | 26 September 2019 08:46 pm09

Kila mtu anayemwongoza mwenzake katika kutenda haki biblia inamfananisha na nyota..
 
Danieli 12:3 “Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.”
 
Unaona? Na ndio maana mtume Paulo aliandika kuna tofauti ya fahari kati ya nyota na nyota. (1Wakorintho 15:41), akiwa na maana kuwa zipo nyota zinazong’aa sana, vile vile zipo zisizong’aa sana, vile vile zipo zinazoonekana kubwa kuliko nyingine na zipo zinazoonekana ndogo..Na tunajua kuwa Bwana wetu Yesu Kristo ndio ile nyota ing’aayo sana kuliko zote, Iliyoonekana na mamajusi, tokea mbali, sio kana kwamba kulikuwa hakuna nyota nyingine hapana , bali ile ndio iliyoonekana yenye fahari na utukufu mkubwa kuliko zote, iliyozidi zote, yeye ndio nyota yenye nguvu kuliko zote, ile nyota ya Asubuhi (Ufunuo 22:16)wakati Jua linakaribia kuchomoza nyingine zote zitazama lakini yenyewe bado itaendelea kuangaza, na nyota hii hata mchana huwa inaonekana kama anga lisipokuwa na mawingu.
 
Lakini bado biblia inatuambia pia katikati ya hizo nyota zipo pia nyota zipoteazo na leo tutaziangazia hizi nyota ni zipi tunalisoma hilo katika
 
Yuda 1:12 “Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa;
 
13 ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; NI NYOTA ZIPOTEAZO, AMBAO WEUSI WA GIZA NDIO AKIBA YAO WALIOWEKEWA MILELE”.
 
Hizi nyota ni zipi katika anga?.
 
Zamani nyota zote ambazo zilikuwa hazitulii au hazina mzunguko maalumu zilijulikana kama nyota zipoteazo, ni nyota ambazo hazikutegemewa na mabaharia katika safari zao za majini, na kuonyesha dira..Ni nyota ambazo unaweza ukaziona leo, na usikae uzione tena mpaka mwisho wa dunia, Kwa mfano hata leo hii ukitazama angani utaona kuna nyota zinakatiza anga kwa mwendo kasi, dakika mbili tatu huzioni tena..huo ni mfano wa nyota zipoteazo, tofauti na baadhi ya nyota ambazo unaweza kuziona mara kwa mara kwamfano mimi tangu nilipokuwa mdogo kuna nyota nilikuwa ninazionaga angani wakati wa usiku, na kama wewe pia nimtazamaji juu, utangundua kuna nyota ambazo zinakuwa zimejikusanya nyingi nyingi ndogo kama kifungu, sasa hizo kwa lugha ya kisayansi zinaitwa KILIMIA, na nyingine utaziona zipo tatu tu kwenye mstari mnyoofu nazo kwa lugha ya kisayansi zinaitwa ORIONI, kama huzijui unaweza ukatoka nje usiku mmoja wenye nyota ukatazama juu hazihitaji elimu au hadubini kuziona, zipo angani na zinaonekana wazi kabisa..Sasa hizi ni nyota sio tu utaziona leo, bali zilikuwa zikionekana tangu vizazi na vizazi huko nyuma, hadi kwenye maandiko zimeandikwa soma..
 
Amosi 5: 8 “mtafuteni YEYE AFANYAYE KILIMIA NA ORIONI, NA KUKIGEUZA KIVULI CHA MAUTI KUWA ASUBUHI, NA KUUFANYA MCHANA KUWA giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake;”
 
Ayubu 9:7 “Aliamuruye jua, nalo halichomozi; Nazo nyota huzipiga muhuri.
8 Ambaye peke yake ni mwenye kuzitandika mbingu, Na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.
9 Yeye afanyaye hizo NYOTA ZA DUBU, na ORIONI, na hicho KILIMIA, Na makundi ya nyota ya kusini”.
 
Ayubu 38: 31 “Je! Waweza kuufunga mnyororo wa KILIMIA, Au kuvilegeza vifungo vya ORIONI?
32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake?….”
 
Unaona, na nyingine nyingi, nyota ya asubuhi unaifahamu ni moja ya nyota zilizo rasmi, wakati wote ipo, lakini embu fikiria juu ya kitu kinachoitwa KIMONDO kama unakifahamu, chenyewe hata hakipiti angani bali utaona sekunde mbili au tatu kina’ngaa sana angani hata kuliko nyota zote halafu baada ya hapo ukioni tena milele hujui kimepotelea wapi..
Ndivyo ilivyo kwa wahubiri wengi wa siku hizi za mwisho, kigezo cha wao kushika biblia au kuwa viongozi wa makundi ya watu, hakiwafanyi kuwa nyota bora, ni kweli anaweza akawa amekidhi vigezo vya kuwa nyota lakini ni nyota ipoteayo..Nyota isiyodumu, ambayo Mtume Yuda ameandika weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele…ukisoma mistari michache ya juu utaona anawafananisha na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa;…
 
Hawa ni viongozi wasiotoa matunda ambayo Mungu anataka ayaone wakiyatoa yaani kuwafanya watu waokolewe na wamjue yeye, hawa ni viongozi wasiodumu katika mzunguko waliowekewa wa injili, yaani hawadumu katika mafundisho ya msingi ya Neno la Mungu, na dalili kubwa inayowatambulisha utaona watu wanaowafuata hawaoni dira yoyote ya kuwafanya wafikie hatma njema ya maisha yao ya milele, wanaangaza kidogo tu, halafu muda mfupi hawapo, wanatafuta mambo yao wenyewe, na katika kipindi hichi cha mwisho wapo wengi.
 
Ndugu, wakati tuliopo sasa, si wakati wa kukaa bila ufahamu, kwasababu upotevu ni mwingi, na njia ni nyembamba sana ielekeayo uzimani…Hivi unajua kuwa kuongezeka kwa waalimu wa Uongo na wahubiri wa uongo ndivyo inavyozidi kuifanya ile njie izidi kuwa nyembamba zaidi?..Njia ya uzima kila siku inazidi kuwa nyembamba….soma biblia jifunze Neno la Mungu tafuta kwanza kuweka uhusiano wako na Mungu sawa, Nyota kweli ni NYINGI, Lakini zipoteazo pia ni NYINGI ZAIDI, hivyo kuwa makini na ile nyota inayokuongoza. Bwana Yupo mlangoni kurudi.
 
Je! Unahabari kuwa hili ndio kanisa la mwisho la saba tuishilo lijulikanalo kama Laodikia na hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hili?. Je! Unahabari kuwa taifa la Israeli sasa linazidi kupata nguvu, na moja ya hizi siku neema itahamia kwao na kwa wakati huo UNYAKUO utakuwa umeshapita?, Na je unahabari kuwa kama huna Roho Mtakatifu huwezi kunyakuliwa?.
 
Unasubiri nini, Ulimwengu ukutese na bado mbingu uikose?..Tafakari tena ufanye maamuzi yenye akili, Kristo anakuita alikufa kwa ajili yako, ukimaanisha kumgeukia atakupokea na kukufanya uwe wake, hivyo TUBU TU, kisha tafuta mahali ukabatizwe ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la YESU KRISTO kama hujafanya hivyo, upate ondoleo la dhambi zako, kisha Bwana atakupa kipawa chake cha Roho Mtakatifu bure.
 
Ubarikiwe sana.
 

Mada Nyinginezo:

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

INJILI KULINGANA NA TEKNOLOJIA.

HUDUMA YA (ELIFAZI, BILDADI, NA SOFARI).

UTEKA ULIOGEUZWA.

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

SIRI YA KUASI KATIKA KANISA LA MUNGU.


Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/26/nyota-zipoteazo/