NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.

by Admin | 26 December 2019 08:46 pm12

Kuchagua mwenza wa Maisha si jambo la kulichukulia kiwepesi wepesi tu kama vile kuchagua Rafiki, ambaye hata mkigombana mnaweza mkaachana na kurudiana muda wowote.

Tena ikiwa wewe ni mtu uliyeokoka ndio unapaswa uwe makini mara dufu, kwasababu ukifanya maamuzi yasiyosahihi utajikuta sio tu kuupoteza wokovu wako bali pia kufanyika chombo cha kuwapoteza na wengine.

Ipo mifano mingi katika biblia ya watu ambao waliingia katika mikono ya wenza ambao sio sahihi. Kwamfano tunamwona mtu mmoja aliyeitwa Ahabu yeye alimwoa Yezebeli, hakuna asiyejua mke wake huyu jinsi alivyokuwa mwiba kwake na kwa Israeli nzima.. Na hiyo yote ni kwasababu alifanya uamuzi usiosahihi katika kuchagua mwenza wa maisha wa kuoa.

1Wafalme 21:25 “(Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa Bwana ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. 

26 Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)”

Tunamwona tena mtu mwingine aliyeitwa Samsoni, jinsi alivyoanguka katika mikono ya mwanamke Delila, binti wa kifilisti, Tunamwona tena Sulemani alivyoanguka kwa wanawake wa mataifa mengine jinsi walivyomgeuza moyo na kumfanya aabudu miungu mingine ikiwa kikwazo kwake kwa Mungu hadi ikafikia hatua ya Mungu kumuundokeshea maadui ….

Vilevile tunaomwona mwanamke Abigaili jinsi alivyoanguka mikononi kwa mume  mpumbavu  mlevi aliyeitwa Nabali..Ambaye ilikuwa ni nusura tu amsababishie mauti yeye pamoja na familia yake yote na wafanyakazi wake wote (soma 1Samweli 25).

Tunaomwona Herode naye, ambaye alijiingiza katika uuaji wa damu isiyokuwa na hatia ya Yohana Mbatizaji  kwa wivu tu wa mke wake, ambaye kiuhalisia hata hakuwa mke wake bali mke wa kaka yake alimuua Yohana kwa shinikizo la mke wake katili.

Matatizo kama hayo vilevile yanaweza kumpata mtu yeyote kama asipojua njia ipasayo ya kumpata mwenza wa maisha sahihi.

Leo hii tutajifunza kanuni chache za kibiblia ambazo ukizifuata utakuwa na uhakika wa kuwa huyu uliyempata asilimia mia ni mwenza Mungu aliyekupangia.

Sasa kabla hatujaenda mbali hapa natazamia kuwa naongea na mtu ambaye ameshaokoka. Kama hujaokoka basi mwisho wa somo hili fanya hivyo, ndio ujumbe huu utakuwa na manufaa kwako.

HATUA YA KWANZA:

Usiwe na haraka ya kuoa au kuolewa: Biblia inatuambia wazi kuwa mapenzi huwa yanachochewa na huwa yanaamshwa..na kama yanaamshwa inamaanisha kuwa kumbe huwa yanapoa  pia soma:

Wimbo uliobora 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Hizi ni hekimu tunafundishwa.. mambo ya kuingia katika ndoa si ya kuyakurupukia. Kisa umemwona Fulani ameolewa au Fulani kaolewa, au umempenda binti yule au kijana yule hivyo na wewe ukaamua moja kwa moja ukaanze mahusiano naye ili mfunge ndoa..Biblia inatuasa tusiyachochee mapenzi kabla ya wakati wake..Mapenzi yana wakati wake..

Ikiwa wewe bado ni binti/kijana mdogo unatafuta mpenzi wa nini wakati unajua kabisa hamna mpango wa kuoana?. Hali kama hiyo ikikujia au vishawishi kama hivyo vikikujia vikatae, kwasababu wakati wake haujafika….Au wewe ni mwanafunzi hujamaliza masomo yako, unataka kuingia katika mahusiano ambayo lengo lake linapaswa liwe ni ndoa, Je utamwoa huyo au yule na huku ukiwa bado masomoni? Huoni kama huo sio wakati wake?..Hivyo ukijikuta unataka kufanya hivyo kataa hiyo hali, toa mawazo yako huko, fanya mambo yako kama vile mtoto mchanga, mpaka wakati wake huko mbeleni utakapofika..

Vilevile wewe bado upo chini ya wazazi wako, au unajijua bado hali yako kiuchumi bado haijaimarika vizuri, unakimbilia wapi kufikiria mambo kama hayo..Simaanishi kuwa mpaka uwe Tajiri ndio uoe, lakini unapaswa ujiandae kisaikolojia, je! Nikifanya hivi, huyo mke wangu nitaweza kumuhudumia hata kwa yale mahitaji ya msingi tu,?  Mambo kama hayo unatakiwa uyafikirie kabla hujaanza kutafuta mwenza wa maisha.

Wimbo uliobora 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”.

Usiogope labda umri umeenda au vipi, Isaka na Yakobo walipata wake zao wakiwa katika umri mkubwa tu, lakini tunaona wake waliowapata walikuwa ni bora Zaidi ya wake wa watu wengine..Vivyo hivyo usikimbilie tu kuoa au kuoelewa kwasababu Fulani Fulani bali uvumilivu pia ni muhimu katika kupata mwenza sahihi na ndoa iliyo bora.

Lakini sawa ikiwe umeyazingatia hayo vizuri na sasa upo tayari kuwa mwenza, basi zingatia mambo yafuatayo:

  1. NI LAZIMA AWE NI MKRISTO.

Nikisema ni lazima awe ni mkristo simaanishi awe amezaliwa katika dini ya ki-kristo, anaweza akawa amezaliwa lakini matendo yake yapo mbali na ukristo, bali namaanisha ni lazima awe ameokoka, na yupo katika mstari ulionyooka wa wokovu wake, Maisha yake yakimshuhudia kuwa ameokoka, kama wewe ulivyo.

Ukiangalia watu wote tulioona kwenye biblia kuanzia Ahabu mpaka Sulemani wote hao waliingia katika matatizo makubwa kwasababu waliyakaidi maagizo ya Mungu..Pale walipoambiwa wasioe wala wasioelewe na watu walio nje ya taifa la Israeli.

Soma

Kumbukumbu 7:3 “binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 

4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi”.

Mungu alikuwa na sababu kuwaambia vile, kwasababu alijua watawageuza moyo na kuandamana nao na miungu yao.

Nehemia 13:25 “Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang’oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe. 

26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye”.

Hivyo jambo la kwanza kabisa la kumtambua kuwa huyu ni mwenza wa maisha sahihi au sio sahihi usikimbilie kumtazama sura, au maumbile yake, au upendo wake kwako..Hilo jambo liondoe akilini kabisa..Usiangalie elimu yake au fedha zake, au ukarimu wake..wala usikimbilie kusema nimeoteshwa kwenye ndoto au nimeonyeshwa kwenye maono kuwa huyu ndio mpenzi wangu…Nataka nikumbie Neno la Mungu ni Zaidi ya ndoto au maono yoyote..Ndoto yoyote  au unabii unaokinzana  na Neno la Mungu unapaswa uukatae hata kama utaonekana unao uhalisia kiasi gani, Neno ndio linatuambia hivyo soma Kumbukumbu 13 utalithibitisha hilo.

Hivyo mwanamke yeyote au mvulana yeyote, anayekujia anataka kukuoa au unataka  kumuoa, mwangalie kwanza Je! yeye ni mkristo aliyesimama katika Imani?…Na kama sio mkristo Je! Yupo tayari kuamini na kumfuata YESU..Ikiwa yupo tayari aanze kwa  kugeuka kwanza ndipo hatua nyingine za kumtathimini sifuate.

2.USIWE NA HARAKA KUFUNGA NAYE NDOA:

Jambo lingine watu wasilolijua ni hili, pindi imetokea tu amemwona kuwa huyu ni mzuri, au anafaa, au ni mtakatifu, anaenda kanisani, bila kutuliza akili zao, moja kwa moja wanakimbilia kwenda kuoa au kuolewa naye..Na baadaye akishagundua kumbe yupo hivi au vile  hiki anaishia kujuta..

Sikuzote tendo la haraka haraka mara nyingi huwa halitokani na Mungu. Ukiona mtu Fulani anakushurutisha haraka haraka ufanye kitu Fulani, au mfanye biashara Fulani bila hata kuwa na nafasi ya kuitafakari vizuri basi ikatae moja kwa moja, ukiona mtu anakulazimisha ununue hiki au kile harakaraka bila hata ya kukiangalia vizuri basi usikinunue kwanza hata kama kwa macho kinaonekana ni kizuri.. Shetani naye huwa ndio anawashurutisha watu hivyo kuingia katika dhambi, atakuambia fanya hichi chapchap hakina shida, lakini baadaye ndio utakuja kujutia milele kwanini ulifanya vile.

Hivyo ukishamthibitisha kuwa huyu au yule ni mkristo, mtakatifu anampenda Mungu, chukua nafasi kumtathimini, pata muda wa kutosha hata miezi kadhaa, ikiwezekana hata mwaka kumwangalia Maisha yake, ..hiyo itakusaidia kuondoa kule kukurupuka ndani yako, na utapata nafasi ya kujua vile ambavyo mwanzoni alikuwa huvijui kuhusu yeye au vile ambavyo amevificha mbele yako. Yusufu hakuwa na haraka ya kumfanya Mariamu kuwa mke wake, bali alingoja kwa kipindi Fulani na ndio maana alipogundua kuwa ana mimba, kumbuka mpaka mimba ionekane labda ni kuanzia miezi 3 na kuendelea, hivyo wakati huo wote hakuwahi kumkaribia wala kumjua, isipokuwa alikuwa amemposa tu, na baadaye alipogundua kuwa ana mimba, akawa radhi kumuacha..Ndipo Mungu akasema usimuache.. Hivyo na wewe chukua nafasi ya kumtathimini huyo anayetaka kuwa mpenzi wako.

Kisha ukiwa katika hali hiyo ya kumtazama sasa ndipo umwombe Mungu..Hapo unajinyenyekeza mbele za Mungu unamwambia nimemwona dada huyu au kaka huyu, ikiwa ni sawasawa na mapenzi yako Ee Mungu naomba unifanikishe na ikiwa sio sawa na mapenzi yako uniepushe naye..

Ukishamaliza kuomba hivyo kwa muda wa kutosha, ikiwezekana kufunga kwa kipindi Fulani..Basi anza harakati za kwenda kutoa mahari kama wewe ni mume, na kama wewe ni mwanamke himiza tendo hilo kwa huyo mwanaume, kwasababu Mungu yupo pamoja na wewe katika kila hatua, kama huyo siye yeye Mungu mwenyewe atamwondoa kwako, au atakuepusha naye, hivyo uwe na amani kuanzia huo wakati kwasababu ulishazitanguliza kwanza kanuni zake, hivyo ni wajibu wa Mungu kukulinda baada ya hapo..

Hakikisha unakwenda kujitambulisha kwao, na yeye kwenu, unatoa mahari, mnafuata hatua zote za ndoa ya kikristo.Kisha baada ya hapo mnafungishwa ndoa kanisani…Hapo ndipo huyu anakuwa mwenza Mungu aliyemkusudia kwa ajili yako.

Ikiwa utazingatia kufuata hatua hizo zote, ondoa wasiwasi kuwa ndoa yako itakuwa na miiba ndani yake, kinyume chake ndio utaimarika hata katika Imani yako kwasababu mke atakuwa msaidizi kwa mume, na mume atakuwa ulinzi kwa mke..Wote wawili wakisimama katika imani mafanikio tele ya rohoni na mwilini yataambatana  nao, na Watoto wao pia watabarikiwa.

IKIWA HAUJAOKOKA:

Lakini kama wewe hujaokoka. Fahamu kuwa upo katika hatari kubwa sana, kwanza kwa kuukosa uzima wa milele, Na pili kwa kutokuwa na ndoa yenye baraka za Mungu..Kwasababu unataka kuoa au kuolewa lakini hujui kuwa anayeifungisha ndoa yenye heri na baraka ni Mungu..Sasa ikiwa umekosana na Mungu wako unatazamia vipi uwe heri katika ndoa yako unayoitazamia..Au upate wapi mwenza wa maisha aliye sahihi..Kwasababu wewe hapo ulipo tayari sio sahihi..utaishia kuoa asiyesahihi mwenzako na mwisho wake ni mlipuko.

Ni vizuri ukafanya uamuzi sahihi leo. Hizi ni siku za mwisho. Yesu yupo mlangoni kurudi..Dalili zote zinaonyesha kuwa unyakuo ni wakati wowote, Parapanda itakapolia wewe utakuwa wapi, wakati wenzako wapo mbinguni wewe utakuwa hapa chini katika dhiki kuu ya mpinga-kristo. Na baada ya hapo unaishia katika ziwa lile la moto. Kama ulikuwa hujui hili ndio kanisa la mwisho, lijulikanalo kama Laodikia, soma Ufunuo 3, Na kwanza hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili,.Na kanisa hili ndio lililokemewa sana na Bwana Yesu kuliko makanisa mengine yaliyotangulia nyuma,.kwamba lipo vuguvugu,..Ni heri tungekuwa baridi au moto, kwasababu hiyo tumeambiwa tutatapikwa.Na tunajua matapishi huwa hayarudiwi tena. Hivyo ikifikia hatua ya wewe ndugu yangu kutapikwa, basi ujue hutakaa urudiwe tena, sehemu yako itakuwa ni katika lile ziwa la moto.

Unasubiri nini kwanini usimpe Yesu Kristo Maisha yako leo ayaokoe, Kesho inaweza ikawa isiwe yako. Nazungumza na wewe unayejiita mkristo, lakini huishi kama KRISTO, ndio maana Bwana anasema wewe ni vuguvugu…

Kama upo tayari kufanya hivyo kumpa Bwana Maisha yako…

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Na Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Zingatia hayo na Bwana atakuwa pamoja nawe. Vilevile Usiacha kutembelea Website hii  https://wingulamashahidi.org mara kwa mara ili ujifunze maneno ya uzima..

Ubarikiwe sana.

Mada Nyinginezo:

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

Je! ni halali kutoa cheti kwa wakristo wanaooa?

Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/12/26/njia-sahihi-ya-kumpata-mwenza-wa-maisha-kibiblia/