SI KILA KIPENDEZACHO KINATOKA KWA BWANA.

by Admin | 12 January 2020 08:46 pm01

Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.


Shalom. Ni siku nyingine tena tumepewa na Bwana. Karibu tujifunze Biblia. Leo tutajifunza njia mojawapo shetani anayotumia kuwaangusha watu.

Kama wengi wetu tunavyojua..historia ya shetani ni ndefu kidogo, ilianzia mbinguni…Huko biblia inasema alikuwa ni malaika wa sifa, Alikuwa ni kerubi wa sifa. Lakini alifanya aliyoyafanya akaiacha enzi yake na nafasi yake akatamani kuwa kama Mungu…baadhi walishawishika kumfuata, kama leo hii tu watu wanavyoshawishika kuwaabudu wanadamu wenzao…Lakini kundi lingine la malaika lililoongozwa na Mikaeli malaika mkuu walimpinga (ambalo hao walikuwa ni wengi kuliko wale walioungana naye) na ikasababisha vita mbinguni..theluthi moja (1/3) ikawa upande wa lusifa na ndio iliyoshindwa vita na theluthi (2/3) iliyokuwa upande wa Mikaeli.

Kumbuka Mungu hakuhusika kwenye hiyo vita, bali Malaika watakatifu, Mungu kamwe hapigani na viumbe vyake..yeye anakuwa tu upande wa wenye haki kuwafanikisha na waovu kuwafadhaisha..Kama alivyokuwa na Daudi vitani dhidi ya majeshi ya maadui zake wafilisti. Hivyo Mungu hata mbingni alikuwa upande wa Mikaeli na malaika zake (kasome Ufunuo 12:7-12).

Sasa leo hatutaingia kuzungumzia kwa undani hiyo vita..Lakini tutaangalia njia moja wapo lusifa aliyoitumia kuwaangusha Malaika walioasi mbinguni.

Tunasoma katika ufunuo..

Ufunuo 12:3 “Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.

4 NA MKIA WAKE WAKOKOTA THELUTHI YA NYOTA ZA MBINGUNI, NA KUZIANGUSHA KATIKA NCHI”.

Nataka tuuzingatie huo mstari wa 4 unaosema …Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.”

Tunaweza kujiuliza kwanini hajasema mkono wake, au uso wake, au pembe zake..bali anasema mkia wake..Ikiwa na maana kuwa Ushawishi wa shetani haupo katika uso wake, wala pembe zake bali katika mkia wake…

Adui shetani anapotaka kumwangusha mtu, atakuja na uso mzuri, atamletea vitu vizuri usoni, vinavyovutia vyenye ahadi nyingi nzuri, na vyenye matumaini na kutia moyo, lakini nyuma yake anauzungusha mkia wake kumwangusha huyo mtu. Atakuonyesha fursa zote za kuiba, na kufanya ufisadi lakini mbeleni ameshakuandalia watu wa kukuchoma moto na kukufunga.

Atakuhubiria leo hii mafundisho mazuri ya kukufariji na dhambi, na atatumia maandiko kukushawishi kwamba ulevi sio dhambi, kwamba Mungu hawezi kuwahukumu watenda dhambi, Mungu siku zote ni Mungu wa rehema..Kwa uso atakuwa na mwonekano mzuri mbele yako na wa faraja lakini nyuma yake kwa mkia wake anakukokotea kuzimu. Atakuhubiria kuvaa vimini, na nguo zinazochora maungo yako hakuna shida, biblia inaruhusu, lakini yeye anajua ni wangapi unawapeleka kuzima kwa uzinzi wako, na kwamba Mungu naye hataweza kukuacha kwa kosa la kuwakosha wengine.. Ndivyo alivyowadanganya na malaika zake na kumwamini Hakuwafuata kwa ukali, bali kwa uzuri aliokuwa nao, na kwa ahadi nyingi, ingekuwa ni hivyo ni nani angemfuata..

..na hatimaye wakajikuta wote wametupwa chini..

Ndivyo shetani alivyo, pale ambapo anataka kumwangusha mtu hatakuja na mapembe, wala kwato…atajigeuza na kuwa malaika wa Nuru.

Hivyo kwa ufupi tu..Biblia inatuonya tujihadhari…Vitu vya ulimwengu huu vinavyoonekana ni vizuri kwa mwonekano, starehe, anasa, michezo, n.k. lakini vingi ni miradi ya shetani…Hivyo tuwe macho kila siku, sio kila kinachoonekana kwa macho au kinachoonekana kizuri kinatoka kwa Mungu, vingi vinatoka kwa Yule adui..Fashion zinatoka kwa Yule Adui, mitindo mitindo inatoka kwa Yule Adui, burudani nyingi na michezo mingi inayovutia na yenye ushawishi inatoka kwa yule adui. Hivyo Bwana atupe macho ya kuona. Maana hatukosi kuzijua fikra za shetani.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali share na wengine ujumbe huu.

Mada Nyinginezo:

ANGUKO LA UFALME WA SHETANI:

UKWELI UNAOPOTOSHA.

VIFUNGO VYA GIZA VYA MILELE.

UFUNUO: Mlango wa 12

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

MPINGA-KRISTO

HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/12/si-kila-kipendezacho-kinatoka-kwa-bwana/