by Admin | 20 January 2020 08:46 pm01
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.
Leo tutaona kimaandiko ni jinsi gani Roho wa Mungu anavyowasaidia watu kuyaelewa maandiko. Watu wengi, wanaposoma biblia na kuona kama ni ngumu haieleweki hususani vile vitabu vya manabii, kama vile Danieli, Isaya, Ezekieli, Yeremia, Zekaria, Ufunuo na vinginevyo, basi wanakata tamaa kabisa ya kuvimaliza, wanaona ni afadhali tu waache, au wanaona pengine hawastahili kufahamu habari zile kwasasa ni za watumishi Fulani tu, au viongozi Fulani wa dini waliokomaa ndio wanaouwezo wa kuelewa.
Lakini nataka nikuambie kutolielewa Neno la Mungu, sio ujinga, bali Mungu mwenyewe ndio karuhusu sehemu nyingine kulifunga kwa makusudi maalumu ili awafunulie wale waliotayari kujifunza (Danieli 12:4, Mathayo 13:11-14). Hivyo leo tutaangazia mfano mmoja wa kwenye biblia ili na wewe kwa kupitia habari hii, upate motisha ya kupenda kujifunza Neno la Mungu peke yako ukiongozwa na Roho Mtakatifu mwenyewe.
Sasa tukisoma kile kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona habari ya mtu mmoja aliyetoka Kushi kwenda kuhiji Yerusalemu, Mtu huyu hakuwa myahudi, wala hakuwa chini ya viongozi wa kidini wa kiyahudi kama Gamalieli na wenzake, bali alikuwa ni kiongozi tu mkuu wa nchi hiyo ya Kushi (ambayo kwasasa ni nchi ya Ethiopia), lakini mtu huyu alimpenda Mungu wa Israeli, na hiyo ikawa inamfanya kila wakati wa sikukuu za kiyahudi na yeye awe anapanda Yerusalemu kuungana na wayahudi wengine kumwabudu Yehova.
Lakini pia alikuwa ni mtu aliyependa kujifunza maandiko. Tunasoma alipokuwa anarudi kutoka Yerusalemu akiwa kwenye gari lake, safarini kurejea nyumbani, biblia inatuambia mule ndani ya gari lake alikuwa akisoma vitabu vya manabii vya agano la kale..Kitabu cha Isaya sura ile ya 53, Mtu huyu alikuwa hayaelewi haya maandiko hata kidogo, pengine alikuwa anayasoma kwa kuyarudia tena na tena,labda pengine atapata tafsiri yake, au ufunuo..akifikiria habari ile ilikuwa inamzungumzia nani, anawaza moyoni mwake, mistari ile inamaanisha nini,..
Sasa kwa kitendo tu kama kile cha kutia nia kutaka kujua maana ya maneno yale..Hapo hapo Roho Mtakatifu akaanza kufanya kazi, akaanza kumwandalia mwalimu wa kumfundisha tokea mbali sana na yeye alipokuwepo.. Roho Mtakatifu akamtafutia mtu, akampata Filipo.. Filipo akiwa huko Samaria akihubiri na kubatiza watu, Roho Mtakatifu akamkatisha kazi yake, na kumwambia anza safari kuelekea mahali pasipo kuwa na watu, Kusini Njia ya jangwa la Gaza, Wakati anaondoka pengine Filipo anawaza kichwani kwake mbona Mungu anafanya niache maelfu ya watu huku Samaria na kuniambia niende huku mahali pasipokuwa na watu..Lakini yeye alitii kwasababu alijua Mungu anamakusudio yake, pengine alidhani huko anapokwenda atakutana na watu wengi zaidi ya wale aliowaacha Samaria,..Akasafiri kupita jangwa lile mpaka akafika mahali akaliona gari Fulani kwa mbali njiani, Roho Mtakatifu akamwambia lisogelee karibu kabisa..Na yeye akalisogelea, alipolisogelea akamwona mtu ndani yake yupo bize akisoma kwa sauti kitabu cha Isaya sura ile ya 53…
Ndipo kuanzia hapo Filipo akaanza kuzungumza naye tusome..
Matendo 8:26 “Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.
27 Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,
28 akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.
29 Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.
30 Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?
31 Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.
32 Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.
33 Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.
34 Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?
35 Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.
36 Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?
37 Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]
38 Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.
39 Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.
Unaweza kuona hapo, Mkushi Yule sio tu aliishia kuyaelewa maandiko yale bali maandiko yale bali pia yalimpelekea kupata mpaka na ubatizo. Lakini hiyo yote ni kwasababu alitia nia moyoni mwake ya kutaka kuyatafakari maandiko kufahamu maana ya yale yaliyoandikwa. Na ndipo akafunuliwa mambo ambayo, hata kuhani mkuu kule Yerusalemu alikuwa hayajui, viongozi wote wa dini na waandishi wanayasoma kila siku lakini hawayaelewi..anakuja kufunuliwa mkushi ambaye hana ujuzi wowote na torati.
Vivyo hivyo na wewe na mimi, Kama umeokoka na unaye Roho Mtakatifu ndani yako, sio wakati wa wewe kukaa kungojea fundisho Fulani uletewe na mhubiri Fulani, au mchungaji Fulani tu peke yake,..Anza kwa kujijengea utaratibu wa wewe mwenyewe kuyatafakari maandiko binafsi kwa bidii na kumwomba Mungu akufunulie, ndipo hapo Mungu atakapotumia njia zake yeye mwenyewe alizozipanga kukufunulia, aidha kwa ufunuo au kwa muhubiri, hapo ndipo utakapopata uhakika kuwa Roho Mtakatifu amesema na wewe.. Wapo wengine wanasema nilikuwa ninautafakari sana mstari Fulani jana usiku, lakini sikuelewa, ghafla kesho yake nikasikia mhubiri Fulani anauhubiri mstari ule ule au nikakutana na mafundisho yale yale,.Hiyo ni ishara kuwa Mungu amemfunulia maana ya mstari ule. Sasa zipo njia nyingine nyingi ambazo Mungu anaweza kumfunulia mtu ikiwa tu atataka yeye mwenyewe kufahamu.
Lakini usikae tu bila kujishughulisha, kusubiria tu kufundishwa wakati wote, ujue kuwa yapo mambo ambayo Roho Mtakatifu anataka kukufundisha wewe kama wewe, vile vile anataka kukujengea uwezo wa wewe kuisikia sauti yake. Hivyo kama wewe umeshaokoka anza kuchukua hatua ya kuyatafakari maandiko bila kuogopa hichi ni kitabu cha manabii kisichoeleweka, au sio, suala la kutafsiri sio lako bali ni la Mungu, yeye mwenyewe ndiye atakayekufungulia njia zake za kuliewa.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312
Mada Nyinginezo:
SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOFICHWA.
KITABU CHA UZIMA
WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.
Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?
Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?
KUOTA UNAKULA CHAKULA.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/20/jinsi-roho-mtakatifu-anavyowafunulia-watu-maandiko/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.