by Admin | 31 March 2020 08:46 pm03
Nakusalimu katika jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima..
Kwanini mara nyingine tunakuwa ni wepesi kufanya dhambi, ni wepesi kuwasengenya majirani zetu, ni wepesi kwenda kuzini, licha ya kwamba tunasema tumeokoka, au tupo karibu na Mungu, lakini bado ni wepesi kutazama picha chafu mitandaoni na kufanya masturbation….
Ni kwasababu tunamdhania Mungu yeye ni kama sisi, kwamba anaelewa tu! Ni madhaifu ya kawaida ya mwili..Na kibaya Zaidi pale tunapoona Mungu hachukui hatua yoyote ya adhabu katika ouvu tulioufanya, pengine pale tulipoenda kutazama picha chafu mitandaoni halafu Mungu akakaa kimya, halafu kesho yake tena tukarudia jambo hilo hilo na bado akawa yupo vilevile, hakuna lolote baya amelifanya katika Maisha yetu, kesho kutwa tena tukaenda kuzini, jambo likawa vilevile, kanisani tunahudhuria, kwaya tunaimba, maombi tunafanya, wala hakuna shida yoyote, wiki ijayo tukaanza kuwazungumizia vibaya majirani zetu, tulikuwa hatuli rushwa wala hututoi rushwa lakini tulipoanza kula rushwa na tukaona hakuna jambo lolote baya lililotukuta basi ndio ikawa desturi yetu kufanya hivyo, licha ya kuwa unasema ni mkristo.
Imekuwa hivyo hivyo miaka nenda miaka rudi, unawaza moyoni na kusema “hata Mungu anaelewa mambo haya”, ndio maana haniadhibu kwa lolote, Unadhani yeye ni kama wewe, Unadhani anavyowaza juu ya maovu ni kama wewe unavyowaza, unamchukulia kama mtu mwenzako asiyeweza kujali mambo madogo madogo kama hayo, unadhani kuwa hawezi kukuacha, wala kukuadhibu kwa vitu kama hivyo..
Lakini leo sikiliza Neno la Mungu linavyosema..
Zaburi 50:16 “Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.
18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.
19 Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.
20 Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.
21 NDIVYO ULIVYOFANYA, NAMI NIKANYAMAZA; UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.
22 Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya”
Angalia tena ule mstari wa 21 anasema.. “Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; ukadhani ya kuwa mimi ni kama wewe”…Unaona, Mungu anapokaa kimya kutokana na dhambi zako unazozifanya kwa siri, usidhani yeye anakufurahia tu!.. Unasema umeokoka na huku unayo mambo yako ya siri ambayo unajua kabisa ni machukizo kwa Mungu, lakini Mungu hakusemeshi kwa lolote na wewe umestarehe tu, unadhani Mungu ni kama wewe, ataendelea na wewe hivyo siku zote..La! Anasema atakurarua na asipatikane mtu wa kukuponya..
Hasemi atakupiga tu, halafu basi au atakuadhibu, hapana anasema atakurarua..Na unajua anayerarua ni mnyama mkali kama vile simba, maana yake ni kuwa atakuharibu vibaya sana, kiasi cha kwamba hutaweza kusimama tena baada ya hapo, hata uombeweje, au uhubiriweje, hutaweza tena kusimama…Ndio maana anasema hapo “asipatikane mtu wa kukuponya”
Na ujumbe huo Mungu anausema kwa wale wote wanaomsahau..Inamaanisha kuwa hapo mwanzo walishawahi kuwa wake, lakini wakamzoelea wakamwona kama yeye ni kama wao, wakawa hawaogopi tena kufanya dhambi mbele zake..
Ndugu ikiwa wewe ni mmojawapo, Basi wakati wako wa kutubu kwa kumaanisha ndio huu, pengine umebakisha kipindi kifupi sana kukumbana na makucha hayo ya Mungu (Usitafute kuujua upande wa pili wa ghadhabu ya Mungu, kwasababu inatisha sana).. Ikiwa unafanya dhambi kisirisiri za kujirudia rudia ambazo hazimpendezi Mungu, na umekuwa ukizifanya kwa muda mrefu sasa na Mungu amekaa kimya tu, ni heri usiendelee kuzifanya, kwasababu kwa kukaa kwake kimya hivyo usidhani yeye ni kama wewe..
Hivyo chukua hatua sasa ya kuuimarisha wokovu wako, na Mungu atakusamehe na kuiahirisha ghadhabu yake kwako.
Kumbuka hizi ni nyakati za mwisho, hakuna haja ya kuthibitishiwa tena kuwa tunaishi katika majira ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hali halisi yenyewe inaonekana kwa mambo yanayoendelea sasa hivi duniani, hivyo huu si wakati wa kuweka mguu mmoja kwa Kristo na mwingine nje, huu ni wakati wa kuzama moja kwa moja kwa Bwana, kwasababu UNYAKUO sasa ni wakati wowote.
2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.
MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!
KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.
KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.
KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?
Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/03/31/ukadhani-ya-kuwa-mimi-ni-kama-wewe/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.