OLE WA NCHI NA BAHARI.

by Admin | 1 April 2020 08:46 pm04

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.

13 Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.

15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.

16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.

17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama JUU YA MCHANGA WA BAHARI”.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, kama ukisoma mistari iliyotangulia kabla ya hiyo, utaona kuwa shetani kuna majira alijaribu kufanya vita katika mbingu, lakini alishindwa kama biblia inavyotuambia akatupwa chini na mahali pake hapakuonekana tena mbinguni kuanzia huo wakati.

Lakini biblia inatuambia pia alipotupwa, hakukaa katika eneo la nchi peke yake, au hakwenda baharini moja kwa moja , hapana, bali alikwenda kusimama juu ya mchanga wa bahari….Kwa namna nyingine alikwenda kusimama ufukweni mahali ambapo nchi na bahari vinakutana.

Shetani alifahamu kuwa, hivyo ndivyo vitu viwili vinavyoikamilisha dunia, hakuegemea tu upande mmoja afanye makao yake huo hapana..badala yake alisimama pale ufukweni ili aweze kuyaona na kuyatawala yale yanayotoka katika nchi na yale yanayotoka katika bahari. Na ndio maana baada ya pale biblia inasema “Ole wa nchi na bahari”, Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu..

Unaona? haituambii nchi tu peke yake, au bahari peke yake, hapana bali vyote viwili, kwasababu ndipo alipopania kuwanasa wanadamu.

SASA NCHI NA BAHARI KIBIBLIA VINAWAKILISHA NINI?

BAHARI: au sehemu yenye maji mengi, biblia imeshatupa majibu yake,.Tusome.

Ufunuo 17:15 “Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”.

Kumbe maji yanawakilisha jamaa, na makutano na mataifa na lugha…Yaani kwa ufupi watu wengi.

Vilevile, tunaweza kuona jambo lingine, pale Bwana Yesu alipochagua mitume wake, wengi wao aliwachagua kutoka katikakati ya wavuvi, akifunua kuwa watakuja kufanya kazi ya uvuvi wa watu wengi, yaani jamaa, na mataifa la Lugha, kama alivyomwambia Petro na Andrea katika (Mathayo 4:19)..

Hivyo Bahari inawakalisha watu wengi, kwahiyo shetani tangu alipoona ameshindwa hawezi tena kupigana yeye kama yeye aliamua sasa kuelekeza macho yake katikati ya watu ili apate nguvu, na chombo kikubwa anachokitumia ili kupata ufuasi mkubwa wa watu ni kupitia kitu kinachoitwa DINI, penye dini ndipo palipo na watu wengi, sio katika siasa au makabila..

Hivyo mpaka sasa yupo katika kilele cha kuzikutanisha dini zote na madhehebu yake yote ambayo tangu zamani yalishautupilia mbali uongozo wa Roho Mtakatifu na kufuata mapokeo yao ya kibinadamu, ili zikubaliane katika kitu kimoja.

Na ndio maana ukisoma ile sura inayofuata ya 13, utaona Yule joka aliposimama tu pale kwenye mchanga wa bahari, wakati huo huo wanyama wawili walitokea, mmoja alitokea baharini, na mwingine akatokea nchi kavu (Soma ufunuo sura ya 13 yote utaona)..Sasa Yule aliyetokea habarini ndiyo huyu atakayepata nguvu ya kuwa na wafuasi wengi sana duniani kwa kupitia dini…

NCHI: NI Hifadhi ya kimwili, tangu mwanzo, Mungu alipomuumba Adamu alimpa ardhi ailime na kuitunza kwasababu huko ndipo alipomchipulia chakula chake kitakachomfanya aishi hapa duniani.

Ayubu 28:5 “Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula;…”..

Hata sasa chakula na utajiri vipo katika ardhi..Hivyo kwa lugha ya sasa nchi tunaweza kusema inawakilisha Uchumi,..Fedha, biashara, hazina, vitu vinavyoweza kumpatia mwanadamu Rizki ili aishi hapa duniani n.k…

Kwahiyo shetani kuona hivyo, alisimama pia katika eneo hilo.. tangu huo wakati akajikita kudhibiti mihimili hiyo miwili mikuu, Watu, na uchumi.. nchi na bahari..

Kwanza Ili awapate Watu anatumia kivuli cha dini, ambapo hivi karibu anaenda kutimiza adhma yake ya kuzileta dini zote zilizopoteza uongozo wa Roho Mtakatifu pamoja, zikiongozwa na ile dini mama ya Rumi, na cha ajabu biblia inatuambia watu wote na mataifa yote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwanakondoo tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu wataufurahia huo utawala na mfumo mzima wa ibilisi ..

Na sasa ili kuwalazimisha watu wote waufuate huo mfumo wa mpinga-Kristo, shetani atamnyanyua mnyama mwingine ambaye atakuwa na nguvu ya kiuchumi sana,(taifa kubwa) ambalo hilo litayahimiza mataifa mengine yote yapokee maagizo kutoka kwa huo umoja wa dini duniani, na mtu yoyote atakayekataa kuupokea hataruhusiwa kununua wala kuuza, wala kufanya biashara yoyote, wala kuajiriwa mahali popote.. Unaona Jinsi hali itakavyokuwa mbaya.. Ni nani atapona hapo.

Haya ni mambo ambayo tunaweza kuyashuhudia siku za hivi karibuni wala tusidhani bado miaka mingi, jaribu kufikiria jinsi ugonjwa huu wa Corona ulivyozuka tu ghafla, na athari yake ndogo tu inawafanya watu wasiweze kutembea hata nje katika baadhi ya nchi, na imetokea tu ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu tu, hakuna ambaye angeamini kuwa dunia ingeweza kuwa namna hii, dunia ambayo inashamra shamra za kila namna..Lakini mambo yamekuwa hivyo barabara zipo wazi..Hata matajiri na wana wa wafalme, na watu mashuhuri na fedha zao haziwasaidii wakati huu. Ndivyo mambo yatakavyobadilika ghafla tu wakati huo ukifika.

Shetani ameshajidhatiti vya kutosha, na ghafla tu, dini zote zitafikia muafaka mmoja zikiongozwa na dini ile mama ya Rumi, watafikia muafaka mmoja, watapata sapoti kutoka katika kila pembe ya dunia, watakuwa na kiongozi wao mmoja ambaye ndio atakuwa mpinga-Kristo..Huyo ataishawishi dunia iwe na ustaarabu mpya, Lakini lengo lake ni kuihimiza ile chapa ya mnyama ili awanase wanadamu wote.. Sasa kwa kuwa yeye amejikita katika masuala ya kiimani sana, kama tulivyosema atapata msaada mwingine kutoka katika taifa lenye nguvu ya kiuchumi duniani, ili kuyalazimisha mataifa mengine yote yamtii yeye kwa shuruti.

Mpaka wakati huo umefika ujue unyakuo tayari umeshapita ndugu yangu, sijui utakula nini wewe unayemkataa Yesu leo, wewe ambaye utakuwepo ulimwenguni wakati huo, pona yako itakuwa ni kufia njaa ndani, kama utakuwa hujakamatwa na kuuliwa kwa mateso yasiyokuwa ya kawaida.. Hakuna mtu yoyote atayevumiliwa na mtu au chombo chochote cha dola ambaye ataonekana hajapokea chapa hiyo ya mnyama.. usifikiri utapona..Ni ngumu sana ndugu, usidhani akaunti yako ya benki itakusaidia wakati huo, hilo jambo halitakuwepo, usidhani utakimbilia mafichoni, ondoa hayo mawazo, usidhani elimu yako itakusaidia kupata ajira wakati huo, acha kufikiria hivyo..Chapa utaipokea tu.

Hizi ni nyakati za hatari tunazoishi, ole wa nchi na bahari!…Kimbilio pekee ni Kristo tu saa hii..Ikiwa upo bado nje ya Kristo, basi fanya uamuzi wa Busara leo hii, tubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, omba toba kwa Mungu, nenda kabatizwe ikiwa bado hujafanya hivyo. huu ni wakati sasa wa kuamka usingizini.

Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 13

UCHAWI WA BALAAMU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

DANIELI: Mlango wa 7

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko miaka elfu”?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/01/ole-wa-nchi-na-bahari/