BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

by Admin | 3 April 2020 08:46 pm04

Basi tuendelee kumjua mungu, naye atatujilia kama mvua ya vuli.


Ndugu, mmoja aliniuliza, akasema, Ni faida gani unapata katika kumtumikia Mungu?..Nikamwambia ni nyingi tu, akasema mimi niliokoka tangu zamani, na niliamua kweli kumfuata Mungu, mpaka ikafika hatua ya mke wangu kunikimbia kutokana na hali yangu, nikawa ninamwomba Mungu sana, ninafunga, ninahudhuria semina mbalimbali, ninahudhuria maombi ya mikesha sana tena sana, nikawa ninamwomba Mungu anikumbuke katika hali yangu ya kiuchumi, lakini kwa jinsi nilivyozidi kuendelea ndivyo mambo yangu yalivyozidi kuwa mabaya,..

Ndugu huyu Kwa jinsi alivyokuwa anaongea na mimi alikuwa anaonyesha kuwa tayari ameshakata tama na ameshaachana na wokovu..Mwisho kabisa akaniambia “Huoni kuwa kuna tatizo fulani na huyu Mungu tunayemtumikia”?

Neno hilo lilinishtua kidogo, nikamwambia kwangu mimi sijaona tatizo lolote katika kumtumikia, sijajua uhusiano wako na Mungu upoje kwa upande wako, Nikamwambia Daudi alisema katika biblia kuwa yeye tangu ujana wake mpaka amekuwa mzee hajawahi kuona mwenye haki ameachwa na Mungu…

Nilipomwambia vile nikisubiri anijibu, Yule mtu hakunijibu tena akaondoka..

Ndugu yangu, lipo jambo ambalo sisi kama wakristo tulioamaaisha kweli kumfuata Mungu tunapaswa tulijue Daudi japokuwa alizungumza maneno hayo, lakini haikumaanisha kuwa ni muda wote na wakati wote mambo yalikuwa yanakwenda kama alivyotaka.. Zipo nyakati nyingi alimwona Mungu kama amemwacha, Kama alikuwa hamsikii, au haoni shida zake anazozipitia dhidi ya hali yake na maadui zake lakini alijipa moyo akisema, Bwana yupo pamoja nami,gongo lake na fimbo yake vyanifariji na alizidi kujipa moyo kumshukuru na kumsifu Mungu..akijua kuwa hata katika mateso yake Mungu hawezi kumwacha.

Sikiliza maneno haya ya Daudi..

Zaburi 13:1 “Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako?

2 Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?

3 Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti.

4 Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa.

5 Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako.

6 Naam, nimwimbie Bwana, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu”.

 

Zaburi 42:9 “Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

10 Watesi wangu hunitukana mithili ya kuniponda mifupa yangu, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako?”

Unaona, upo wakati aliomba lakini haoni majibu, alitamani lakini hakupata, alikuwa akihuzunika akikumbuka kuna wakati alimpiga Goliathi, na wafilisti wote wakawa wanamuogopa lakini wakati mwingine haoni msaada wowote mpaka anaenda kuomba hifadhi kwa hao hao wafilisti ambao walikuwa adui zake, walau wampe eneo la kuipumzisha nafsi yake..mpaka unafika wakati tena wafilisti wanakwenda kupigana na ndugu zake Wayahudi na yeye pia anataka kujumuika nao ili tu awaridhishe wafilisti wasimwone kuwa ni msaliti..Wengi wetu hatujui kuwa Daudi tunayemsoma kuna wakati alilikimbia taifa lake na kwenda kutafuta msaada kwa wafilisti (maadui wa Israeli)..

Sasa kwa namna ya kawaida ungeweza kusema Daudi alishaachwa na Mungu tangu zamani, kuna tatizo na huyo Mungu anayemtukia,..Lakini pamoja na mateso hayo yote alizidi kuzishilia ahadi za Mungu, akimshukuru yeye, na kumwimbia siku zote..Mpaka wakati ulipofika wa yeye kustareheshwa ulipofika, na kufanywa mfalme wa Israeli nzima, mpaka leo hii tunamsoma Daudi kama mtu aliyeupendezesha moyo wa Mungu, haikuwa safari rahisi, ya kudhani kuwa kila alichokiomba kilikuwa kinakuja kwa ghafla tu..

Baadaye Daudi anakuja kusema..

Zaburi 66:19 “Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu.

20 Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake”.

Hata na sisi wakati huu, Bwana Yesu alituambia, ombeni nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa, hakumaanisha kuwa tuombapo yatakuja wakati huo huo kwa ghafla, inaweza pia ikawa hivyo lakini si wakati wote,..Ni kuamini, na kungoja na kuwa na saburi…Na ndio maana Bwana wetu huyo huyo sehemu nyingine alisema maneno haya..

Luka Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa.

2 Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu.

3 Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu.

4 Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu,

5 lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.

6 Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu.

7 Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?

8 Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?”

Unaona, maandiko hayo yanatuonyesha kabisa, kuombwa kwetu kunapaswa kusiwe kwa kukata tamaa kama vile kulivyokuwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Daudi. Kwasababu ni uhakika kwamba mwisho wa siku tutajibiwa, iwe isiwe, majibu yatakuja tu kama tulivyomwomba, kwasababu Mungu ni mvumilivu kwetu. Na anatuhurumia na anapendezwa na dua zetu.

Hivyo wewe uliyemfuata Kristo kwa moyo wako wote, nataka nikuambie usikatishwe tamaa, kuona hakuna dalili yoyote leo, majira yako yatafika, nawe utasema kama Daudi “Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu”.

Zidi tu kuonyesha bidii kumtafuta yeye leo ,wacha kuangalia hali yako ya sasa..Wakati wa kukujilia kama mvua ya vuli utafika kama hautautupa utakatifu wako na wokovu wako.

Hosea 6:3 “Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini [HAKIKA] kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

https://wingulamashahidi.org/mafundisho-ya-ndoa/

SAA YA KUHARIBIWA IIJIAYO ULIMWENGU WOTE.

KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.

KWA HIYO NDUGU, VUMILIENI, HATA KUJA KWAKE BWANA.

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/03/basi-tuendelee-kumjua-mungunaye-atatujilia-kama-mvua-ya-vuli/