USITUPE LULU ZAKO MBELE YA NGURUWE.

by Admin | 5 April 2020 08:46 pm04

Mathayo 7:6 “Msiwape mbwa kilicho kitakatifu, wala msitupe lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua”.

Maneno hayo yalizungumzwa na Bwana wetu Yesu. Akifunua kuwa sio kila neno/kitukinawafaa baadhi ya watu. Hivyo tuwe na hekima tunapotoa au tunaposema vitu vyetu vilivyo vya thamani mbele za watu, kwasababu unaweza ukasema kitu ukadhani kitakuwa na manufaa kwa yule unayemwambia badala yake kitu kile kikageuka kuwa matatizo kwako.

Tutajifunza mfano mmoja muhimu katika biblia kisha kupitia huo tutapata kuelewa Zaidi kiini cha somo letu.

Wakati Mungu anamtokea Musa na kuzungumza naye kwa mara ya kwanza katika kile kijiti kilichokuwa kinawaka moto lakini hakiteketei…Alimwambia maneno haya..

Kutoka 3:6 “Mimi ni Mungu wa baba yako Ibrahimu, Isaka na Yakobo….

7 Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;

8 nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

9 Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.

10 Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.”

Baada ya Mungu kumwambia maneno haya ya ahadi na ya Faraja..alimwambia akawaambie habari hizo wana wa Israeli…Kwamba wamejiliwa na wanakwenda kutolewa katika nchi ya Misri ya utumwa na kupelekwa nchi ya Ahadi. Hivyo Musa akaenda kuwaambia wana wa Israeli habari hizo nao wakafurahi.

Lakini jambo la kipekee ni kwamba Mungu alipomwambia Musa aende kwa Farao…alimwambia amwambie Farao maneno mengine tofauti na hayo…Tusome..

Kutoka 3:16 “Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri;

17 Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali.

18 Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, BWANA MUNGU WA WAEBRANIA, AMEKUTANA NASI; BASI SASA TWAKUOMBA, TUPE RUHUSA TWENDE MWENDO SIKU TATU JANGWANI, ILI TUMTOLEE DHABIHU BWANA MUNGU WETU.

19 Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu”.

Sasa unaweza kujiuliza kwanini Mungu hakumwambia Musa amwambie Farao kwamba “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo nimeona mateso ya watu wangu jinsi gani unavyowatumikisha hivyo wape ruhusa waondoke waende nchi ya ahadi niliyowaahidia?”…Badala yake Mungu hakumruhusu Musa kumwambia Farao habari zozote kuhusu Ibrahimu, wala kuhusu mahali wanapokwenda..badala yake ni kama Mungu alimdanganya Farao kwamba wanakwenda tu kumtolea Mungu dhabihu jangwani kisha watarudi…kumbe ndio walikuwa wanakweda kutokomea huko.

Hivyo Farao akadanganyika akajua kuwa wana wa Israeli wanataka tu kwenda kumtolea Mungu wao dhabihu jangwani siku tatu na kisha watarudi kumbe nyuma yake kulikuwa na mpango mwingine wa wana wa Israeli kutokomea huko huko na kutokurudi tena…

Sasa japokuwa Farao alikuwa anajua ni kitendo tu cha kwenda na kurudi lakini alikuwa mgumu vile hebu tafakari laiti angejua kuwa wale watu ndio wamepanga wanaondoka kabisa kabisa hali ingekuwaje?..bila shaka vingeamka tena vita vingine visivyokuwa na maana.

Sasa Kwanini Mungu alifanya vile?, Ni kwasababu aliwazuilia wana wa Israeli wasitupe lulu zao mbele za nguruwe wasije wakazikanyaga mbele ya miguu yao na kugeuka na kuwararua.

Hivyo wana wa Israeli mpaka wanaondoka Misri…Farao alikuwa anajua kuwa ni wanakwenda tu na kurudi.. Hebu tusome mistari kadhaa kulithibitisha hilo..

Kutoka 5:2 “Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.

3 Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu Bwana, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga”.

Soma tena..

Kutoka 8:25 “Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.

26 Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka Bwana, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?

27 La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu Bwana, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.

28 Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni”.

Umeona hapo Farao anawaambia “lakini hamtakwenda mbali sana”…maana yake alikuwa anafikiri kwamba watarudi baada ya kutoka kule…na sehemu nyingine utaona Farao anawaambia waende tu huko jangwani watu walio wazee lakini Watoto wabaki na mifugo (soma kutoka 10:24)…Hivyo ikabakia kuwa siri ya Musa na wana wa Israeli kwamba siku yao ya kutoka Misri kikabisa kabisa imefika…Farao na waMisri hawakuijua hiyo siri, walidhani wanakwenda tu jangwani watarudi baada ya siku chache watakapomaliza kutoa sadaka zao hizo, watarudi na kuendelea kuwatumikisha.

Farao alikuja kushtuka kuwa kalaghaiwa na wale watu, wamekimbia na hawana mpango wa kurudi tena siku alipokuja kupata taarifa kuwa wale watu hawaelekea ile njia ya jangwa bali waligeuka na kurudi kuikabili bahari…Ndipo alipoelewa kuwa wamefanya makosa makubwa kuwaachilia waondoke.. Tusome

Kutoka 14:5 “Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu WAMEKWISHA KIMBIA; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena?”

Ndugu katika safari ya wokovu… si kila kitu kizuri Bwana anachokuambia ni cha kwenda kuwaambia watu kama kilivyo…Bwana amekuahidia au amekupa ufunuo fulani wa jambo lako zuri linalokuja mbele usikurupuke na kwenda kusimulia simulia huku na huko…kwa kufanya hivyo utakuwa umempa adui nafasi na mlango mzuri wa kuyaharibu maono yako uliyopewa..

Hali kadhalika Bwana anapokutoa leo katika ulimwengu(yaani katika dhambi)…ambao inafananishwa na Misri yetu…sio kila kitu ambacho Mungu kakufunulia ni cha kukieleza mbele za watu wa kidunia…Unatakiwa uondoke katika dhambi kwa njama kama hizo za wana wa Israeli..

Kwamfano Ulikuwa unauza Bar…na majirani zako wanauza bar kama wewe, sasa umempokea Yesu na Roho Mtakatifu amekushuhudia ndani yako kwamba, biashara hiyo ni ya utumwa wa dhambi na itakupeleka kuzimu…sasa wewe anza kuifunga hiyo haraka sio lazima uwaambie wale wanaokuzunguka sababu ya kuifunga, wewe jiponye nafsi yako kwanza huo sio wakati wa kuanza kuwahubiria….baada ya kuifunga na kuhakikisha marago yako yote umeyatoa Misri, ndipo uwaambie mimi nimeokoka na hiyo kazi siirudii tena….lakini ukiwahi kuwaambia kwamba nimeokoka na Kesho au Kesho kutwa nitaifunga hiyo Bar, au nitaacha hii kazi ya kujiuza, au nitaacha haya madili haramu tunayoyafanya, au nitaacha uvaaji wa nguo hizi na vimini hivi, au nitaacha dansi..ukianza kumwambia huyo mpenzi wako unayefanya naye uasherati kwamba sasa umeokoka hivyo kuanzia Kesho nakuacha…nataka nikuambie kwamba utakuwa umejiweka kupitia vita visivyokuwa na lazima…mwache kwanza huyo unayefanya naye uzinzi, ikiwezekana mtoroke baadaye akikuuliza kwanini umeondoka bila kuniambia mwambie ni kwasababu nimeokoka na siwezi tena kuishi Maisha ya uasherati…lakini ukimwambia huku bado upo naye nyumba moja….nakwambia shetani atakupelekesha kweli kweli na unaweza kujikuta huwezi kumwacha wala kuuacha ulimwengu….Utapitia vita visivyokuwa na sababu..

Vita vinatakiwa vianze baada ya wewe kuondoka katika ulimwengu..Ulimwengu unatakiwa ujue kwamba wewe umeokoka baada ya kuondoa marago yako yote ulimwenguni na sio wakati ambao wewe bado upo katika ulimwengu…kama vile wana wa Israeli walivyoondoa majeshi yao ndipo Farao akabutuka na kujua kuwa wale watu hawakwenda safari ya kwenda na kurudi..bali walipanga kupotelea moja kwa moja..ndipo akapanga majeshi kumfuatilia.

Hivyo kama hujaokoka leo? Huu ndio wakati wako sasa..Tubu mpokee Yesu, kutubu maana yake ni kugeuka na kuacha yale uliyokuwa unafanya mwanzo…na njia ni hiyo hiyo, fungasha marago yako yote na kimbia kimya kimpya!…usitoe taarifa kamili kwanini utatoka mpaka utakapotoka Misri…Toka Misri leo kwa njama zozote zile uwezazo…Toka kwenye ulevi, toka kwenye ulimwengu wa starehe za kidunia,miziki, toka kwenye huo mtandao wa wala rushwa, wizi, , utapeli, usengenyaji, uasherati, ulawiti,ufisadi…

Kwa mwazo igiza hata unaumwa ili wakupe ruhusa utoke katika kampuni yao hiyo ya bia..na baadaye wakikuuliza mbona hurudi waambie mimi nimeokoka na huko sirudi tena..Igiza hata unakwenda kusalimia nyumbani ili tu huyo mtu unayeishi naye ambaye mnafanya naye uasherati akupe ruhusa uondoke na huko akiona hurudi akikuuliza vipi mwambie nimeokoka huku huku na Maisha hayo siyaishi tena. Jiponye nafsi yako kwa gharama zozote…

Dunia inapita na mambo yake yote..Bwana Yesu alisema itakufaidia nini upate ulimwengu mzima na upate hasara ya nafsi yako?…Ikimaanisha kuwa nafsi ni kitu cha kulinda kuliko kitu kingine chochote…hivyo kwa gharama zozote na njama zozote jiokoe nafsi yako na huu ulimwengu.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 5

JINA LA MUNGU NI LIPI?

UJIO WA BWANA YESU.

JE ADAMU ALIKUWA NA KITOVU?

JIHADHARI NA DHAMBI YA WIVU/HUSUDA.

UPEPO WA ROHO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/05/usitupe-lulu-zako-mbele-ya-nguruwe/