KUMBUKA, VIVUKO VYA YORDANI VINAKUNGOJA MBELENI.

by Admin | 18 April 2020 08:46 pm04

Ni jambo la kawaida, kuona tabia za watu zinabadilika hususani pale wanapoona wanakaribia kwenda kuangamizwa wote,..Utaona wengi wao wanajigeuza na kujifanya kama vile wao ni kama wale wengine, ili wafanikiwe kijipenyeza kisirisiri katikati yao wasalimishe roho zao..

Hiyo ilitokea wakati wa kipindi cha Esta, pale ambapo maadui wa Wayahudi walipokusudia kuwaua wayahudi wote kwa kibali cha mfalme Ahasuero, lakini kibao kilipowageukia na kuona mfalme ndio amewapa heshima mara dufu,na ziadi ya yote amewapa mamlaka ya kuwatafuta wale maadui zao wawaue, biblia inatuambia jamii kubwa ya watu wakajigeuza na wenyewe kujifanya ni wayahudi ..

Esta 8:16 “Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi.

17 Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia”.

Unaona hapo?..

Tunasoma tena habari nyingine, kuna wakati jamii mbili za wana wa Israeli zilipigana, ambazo ni Ni jamii ya watu wa Efraimu, na watu wa Gileadi… Sababu ya vita yenyewe ilikuwa ni wale watu wa Gileadi walikwenda kupigana na maadui zao, bila kuwashirikisha watu wa Efraimu kwenda kuwasaidia, hivyo watu wa Efraimu wakakasirika kuona uamuzi ule waliouchukua ndugu zao hivyo wakapanga vita wawapige na Wagileadi, Lakini mambo yalikuwa ni tofuati, kinyume chake wao ndio waliopigwa..

Sasa baada ya kuona wanazidiwa na hali ndio inakuwa mbaya, ikawabidi, watoroke watu wengi, wajaribu kuvuka kujichanganya na jamii ya wagileadi. Sasa ilikuwa ili kufika ng’ambo ni sharti uvuke mto wa Yordani..Lakini wao walidhani ni rahisi rahisi tu kama siku zote, unavuka tu na kuingia bila kuulizwa chochote..wengine wakadhani hata wakiulizwa wewe ni nani, je ni mwenyeji wa huku watasema tu ndio, halafu basi wataruhusiwa kuvuka..

Hawakujua kuwa wale wagileadi walipata taarifa juu ya njama zao, Hivyo walichokifanya ni kwenda kusimama pale kwenye vivuko vya Yordani, pale mpakani, na watu wote, waliochanganyikana nao walipofika wavuke wasijue kuwa huyu ni nani na huyu ni nani, walitumia njama moja ya kuwakamata waefraimu katikati ya wagileadi, waliwaambia watamke Neno “shibolethi” tusome..

Waamuzi 12:5 “Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La;

6 ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu”.

Unaona, walitumia kigezo cha Lugha, kuwashika, vinginevyo wasingewatambua kwa namna yoyote, kwasababu walijua lugha ya asili ni kitu kinachoshikamana na mtu kuliko kitu kingine chochote, walijua lugha ya asili inaweza kweli kuigwa lakini haiwezi kuigwa kwa ufasaha wake wote, haijalishi mgeni atajifunza kwa miaka mingapi, ile lugha ambayo hajazaliwa nayo hawezi kuiiga kwa ufasaha wote..Hata leo hii mzungu aishi uswahilini hata miaka 50 na akakijua Kiswahili chote, bado kuna vimelea vya lugha hatoweza kuvitamka ipasavyo kama Yule mzawa..

Sasa Biblia inatuambia agano la kale ni kivule cha mambo yatakayotokea katika kipindi cha agano jipya..Na habari hizo hazijaandikwa ili kutusisimua tu, hapana bali zina ujumbe mkubwa sana kwetu katika roho.

Inamaana kuwa utafika wakati mambo ya wokovu hayatakuwa kama yalivyo leo hii, kuna wakati wale waovu watatamani sana kwa nguvu kujiingiza katika ufalme, watajigueza kwa kila namna ili tu wapate nafasi, lakini safari hii, haitakuwa ni kwa njia rahisi kwa wanavyodhani, bali watakuwa na mtihani mkubwa wa kufanya..

Luka 16:16 “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu”.

Utapimwa wokovu wako, sio kwa kusema tu mimi nimeokoka, mimi nilibatizwa, mimi ninakwenda kanisani bali vitazingatiwa vigezo vya ndani zaidi, utaulizwa je! Huo wokovu unauzoefu nao kiasi gani, Je, ni wa kujifunza tu, au ulikuwa ni sehemu ya maisha yako tangu zamani..

Hili ndio lile kundi ambalo Bwana alilitolea mfano wake, wa mtu Yule aliyekutwa ndani ya harusi lakini hana vazi la harusi mpaka watu wakawa wanashangaa ameingiaje ingiaje mule ndani na wakati hana vazi la harusi..Kumbuka wakati huu kule nje kulikuwa kunaendelea machinjo.. Akatoroka akaingia ndani, lakini alionekana kwasababu hakuwa na vazi (hakuwa na kadi ya mwaliko tangu zamani) Kilichofuata ni kwamba alikamatwa na kufungwa na kwenda kutupwa nje..

Ndipo Bwana akamalizia kwa kusema maneno haya.. “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”. Soma (Mathayo 22:1-14)

Hivyo ndugu anza kuujenga uhusiano wako na Mungu kuanzia sasa, usisubiri wakati Fulani, kubali kuzaliwa mara ya pili leo uikulie wokovu ujifunze lugha ya kimbinguni, kama bado hujaokoka.. kwasababu unafika wakati hapo mbele hakutakuwa tena na mlango wa neema ya yule atakayetaka kuingia.. kwa maana hizi ni nyakati za mwisho jambo ambalo hakuna mtu asiyelijua hilo.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!

 

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

Yeshuruni ni nani katika biblia?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/04/18/kumbuka-vivuko-vya-yordani-vinakungoja-mbeleni/