by Admin | 4 June 2020 08:46 pm06
Biblia inapozungumzia mioyo..haimaanishi hii mioyo iliyomo ndani ya vifua vyetu inayosukuma damu…hapana bali inazungumzia utu wa ndani ambao ni roho zetu.
Biblia inasema katika…
Waefeso 1:18 “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo”
Umeona hapo inasema “macho ya mioyo”..sasa moyo wa nyama hauwezi kuwa na macho…maana yake ikimaanisha kuwa ni kitu kingine ndio kinachozungumziwa hapo…na hicho si kingine Zaidi ya ROHO ZETU.
Roho zetu ni mfano wa miili yetu, zina macho, zina masikio, zina miguu, zina mikono, zina kila kitu ambacho kinaweza kunaweza kuonekana kwenye hii miili ya damu na nyama…Roho zetu na zenyewe zinakula na zinaishi na zinaweza kufa pia endapo zikiwekwa katika mazingira fulani yasiyoruhusu uhai.
Mtu ambaye ni kipofu rohoni ni yule ambaye macho ya roho yake hayaoni…Na kumbuka sio yule ambaye haoni vitu vya ulimwengu wa roho kama wachawi, au malaika, au maono…Hapana bali ni yule ambaye halielewi Neno. Na mtu asiyelielewa neno kwake huyo haliwezi kumsaidia chochote, na ni rahisi kulipuuzia. Hata wewe ukisoma kitabu ambacho hukielewi ni rahisi kukipuuzia hata kama kitabu hicho kitakuwa kinasifiwa na wangapi..Na ndivyo hivyo biblia nayo, kama haieleweki kwa mtu inageuka na kuwa kitabu kisicho na maana yoyote kwa anayekisoma….Na kuelewa maana yake ni kutambua matumizi ya kile unachokisoma katika Maisha uliyopo sasa.
Sasa hebu turudi kwenye biblia tusome kisa kimoja tutajifunza Zaidi maana ya “kufumbuliwa macho ya kiroho”.
Kama wewe ni msomi mzuri wa biblia utakumbuka kisa kimoja cha vijana wawili waliokuwa wanaelekea Kijiji kimoja kilichoitwa Emau, siku ile Bwana Yesu alipofufuka, na njiani Yesu mwenyewe aliwatokea na kuungana nao na wao pasipo kujua kuwa ni Yesu walidhani kuwa ni mtu tu wa kawaida…Hebu tusome…
Luka 24: 13 “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.
14 Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.
15 Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.
16 Macho yao yakafumbwa wasimtambue.
17 Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.
18 Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?
19 Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;
20 tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.
21 Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;
22 tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,
23 wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai.
24 Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.
25 Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!
26 JE! HAIKUMPASA KRISTO KUPATA MATESO HAYA NA KUINGIA KATIKA UTUKUFU WAKE?
27 AKAANZA KUTOKA MUSA NA MANABII WOTE, AKAWAELEZA KATIKA MAANDIKO YOTE MAMBO YALIYOMHUSU YEYE MWENYEWE.
28 Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.
29 Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.
30 Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
31 Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. 32 WAKAAMBIANA, JE! MIOYO YETU HAIKUWAKA NDANI YETU HAPO ALIPOKUWA AKISEMA NASI NJIANI, NA KUTUFUNULIA MAANDIKO?”
Sasa kama utagundua kitu…hawa hata wakati Yesu anazungumza nao kule barabarani na kuwafafanulia maandiko, bado walikuwa hata hawaelewi vizuri kile Bwana alichokua anakisema…Lakini baada tu ya kuula ule mkate…ghafla ufahamu ukawaingia wa yale maandiko Bwana aliyokuwa anazungumza nao kule njiani…uelewa wa ajabu wa kile Bwana alichokuwa anawaambia kule njiani ukawaingia, akili ya kuchambua maandiko ikawaingia, na mwisho wakaona mbona kama yale maandiko ndio yanayomhusu mtu fulani aliyekuwa na sauti kama ya huyu tunayezungumza naye hapa?…
Je huyu siye yule Yesu kweli ama ndugu yake??..hebu ngoja tumwangalie vizuri!..walipomtazama vizuri wakagundua ni yeye…kisha akatoweka mbele yao…lakini walianza kumgundua kwanza kwa andiko ndipo uso baadaye…Maana yake ni kwamba hata kama Yesu angewatokea kwa sura nyingine au hata kama angekuwa amejifunika uso wasimwone…kwa ufunuo wa maandiko bado wangemuhisi tu, …Hebu wasikie wanavyosema hapa katika ule mstari wa mwisho.. “WAKAAMBIANA, JE! MIOYO YETU HAIKUWAKA NDANI YETU HAPO ALIPOKUWA AKISEMA NASI NJIANI, NA KUTUFUNULIA MAANDIKO?”…Yaani maana yake ni kwamba imekuwaje kuwaje hatujamtambua tangu pale mwanzo alipoanza kutufunulia haya maandiko?..
Kwahiyo kilichofunuliwa cha kwanza ni macho ya mioyo yao (yaani uelewa wa maandiko) ndipo vitu vingine vikafuata… Kama wasingeyaelewa maandiko wasingemtambua Bwana kwa namna yoyote ile hata kama angejitambulisha wazi mbele yao kwamba yeye ndiye Kristo, bado wasingemwamini.
Kama sehemu fulani maandiko yanavyosema….
Yohana 12:37 “Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;
38 ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
39 Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,
40 Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya”
Kwahiyo ni muhimu sana kutafuta kufumbuliwa macho ya rohoni, wengi wanatafuta kuona wachawi!, huko sio kufumbuliwa macho, wengine wanatafuta kuona maono..huko nako sio kufumbuliwa macho ya rohoni! Wala kuota ndoto za kimiujiza sio kufumbuliwa macho……kupata kuelewa Kwanini Yesu alikuja duniani, anataka nini sasa, na yupo wapi sasa, na kuyaelewa mapenzi yake na kuyafanya huko ndio kufumbuliwa macho ya rohoni…Na hapo utamwona Yesu kila siku katika Maisha yako..huhitaji macho ya damu na nyama kuhakiki, tayari macho yako ya ndani yanamwona kila siku katika Maisha yako.
Luka 24: 44 “Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.
45 Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.
46 Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu”
Na mtu muuaji bado hajambuliwa macho, mtu anayevaa vimini hajafumbuliwa macho, mtu anayezini na anayefanya uasherati, na anayefanya mambo mengine ya kidunia bado ni kipofu wa rohoni, haijalishi anaona maono au anatabiri..bado ni kipofu! Kulingana na biblia.
Na tunafunguliwaje macho ya rohoni?..kwanza kwa kukubali kwamba sisi ni wakosaji, na kisha kwenda chini yake kwa unyenyekevu na kuomba rehema na toba…baada ya hapo kumtii maagizo yake ya kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi na kwa jina lake..kisha kupokea Roho wake mtakatifu..Huyo ndiye aliye na jukumu la kufumbua macho yetu ya rohoni na kutufanya kuyaelewa maandiko..lakini pasipo huyo kamwe hatuwezi kumwelewa Mungu wala kumjua…tutakuwa tu kama Wanyama ambao wana macho lakini hawaoni.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.
WAKAKAA KWAKE SIKU ILE. NAYO ILIKUWA YAPATA SAA KUMI.
WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.
WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.
IKIMBIE DHAMBI KWA GHARAMA ZOZOTE ZILE!
USIMZIMISHE ROHO.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/04/umefumbuliwa-macho-yako-ya-kiroho/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.