VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

by Admin | 8 June 2020 08:46 pm06

Maadamu tunaishi hapa duniani, kila siku tupo mapambanoni….Unapomwamini Yesu Kristo tu na kuamua kumfuata kwa moyo wote, kwa kitendo hicho tu tayari umeshatangaza vita na ufalme wa giza..Na vita hivyo huna budi kuvikabili mpaka siku unaondoka hapa duniani. Hakuna siku hivi vita vya imani vitaisha..utapitia hiki, utatulia kidogo ghafla kitanyanyuka kingine, lakini Bwana atakuwa upande wako kukupa ushindi. Lakini shetani huwa hakati tamaa kama sisi wanadamu…Kuanzia mwanzo wa safari yako mpaka mwisho utakuwa vitani tu!…kwahiyo jiandae kwa hilo…Kama alikupa shamba wakati ukiwa wake, leo umemsaliti atalidai shamba lake, kama alikupa heshima hiyo heshima atakunyang’anya na atawatumia watumishi wake.

Tunaweza kujifunza kwa ufupi kwa Bwana wetu Yesu, jinsi shetani alivyoanzana naye kwenye huduma yake na alivyomaliza naye. Inadhaniwa na wengi kuwa siku ile shetani alipomjaribu Bwana kule jangwani ndio ilikuwa mwisho wa majaribu.. Lakini nataka nikuambie sivyo!…Ndio ilikuwa ni mwanzo tu wa majaribu…ingekuwa ndio ilikuwa mwisho sidhani kama Bwana angesulubiwa…Hebu tusome.

Luka 4:12 “Yesu akajibu akamwambia, Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.

13 Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha AKAENDA ZAKE KWA MUDA”.

Nataka uone hicho kipengele cha mwisho kinachosema “akaenda zake kwa muda!”…Maana yake ni kwamba atarudi tena baadaye!. Anakwenda kuandaa vita vingine vipya..hivyo kakubali kashindwa lakini hiyo haimpi sababu ya kukata tamaa…Na utaona aliporudi tena alirudi kwa nguvu nyingi akishindana na Bwana kupitia watu na wakuu…Aliwavaa mpaka viongozi wa dini wakubwa, na wakuu wa nchi kupambana na Yesu…Mpaka ilifikia wakati mfalme Herode anatafuta kumuua Bwana Yesu. Hebu jiweke kwenye nafasi kama hiyo,!..viongozi wa dini wanakupinga! Na bado mkuu wa nchi anatafuta kukuua?..Bila shaka hivyo ni vita vikali sana..

Na haikutosha hapo, kuonyesha jinsi gani shetani hakati tamaa…japokuwa alimshindwa, lakini bado hata wakati yupo pale msalabani anamjia tena na kumwambia maneno yale yale kama aliyomwambia kule jangwani… “ikiwa kweli wewe ni mwana wa Mungu jishushe msalabani!”…bado anaamini anaouwezo wa kumwangusha Bwana hata akiwa bado amebakisha dakika moja ya pumzi ya uhai wake…Mpaka sekunde ya mwisho Bwana yupo vitani.. Na ndio maana Bwana aliwaambia hivi wanafunzi..

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.

Sasa dhiki inayozungumziwa hapo ndio hayo majaribu…Na mfano wa dhiki hizo sio kuvunjiwa bar yako iliyokuwa inakupatia kipato, au kuibiwa fedha zako na mfanyakazi wako wa Bar!…au kupigwa baada ya kufumaniwa, au kuingizwa jela baada ya kushikwa unaiba!… Hapana hizo sio dhiki(sio vita vya imani) bali ni majibu ya dhambi zako!…Dhiki hasa ni zile unazozipitia baada ya wewe kuukataa ubaya!..mfano unafukuzwa kazi kwasababu umekataa kufanya uasherati, unasingiziwa kitu Fulani kwasababu umekataa kwenda katika njia zao, unachukiwa na kutengwa kwasababu umebadilisha njia zako na umeacha kuwa wa kidunia au kuabudu sanamu, au mizimu au kufanya matambiko…Mfano wa dhiki hizo ndio majaribu..

Kwasababu majaribu haya yataendelea mpaka mwisho wa maisha yetu!..biblia inatuonya TUVUMILIE! Na TUSTAHIMILI na pia tusiogope!…kwasababu Bwana atakuwa upande wetu kutusaidia tukijua kuwa lipo taji la uzima linatungojea huko mbeleni.

Yakobo 1:12 “Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea TAJI YA UZIMA, Bwana aliyowaahidia wampendao”.

Ufunuo 2:9 “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

10 USIOGOPE MAMBO YATAKAYOKUPATA; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa TAJI YA UZIMA”.

Bwana akubariki.

Kama hujaokoka, mlango wa neema upo wazi..lakini hautakuwa hivi siku zote…nyakati hizi muda unaenda kwa kasi sana…kufumba na kufumba dunia itaisha..na utaanza utawala mpya wa Bwana wetu Yesu Kristo..ambapo Huko atawalipa watakatifu wake kwa kadri ya Uvumilivu wao…Waliostahimili zaidi watapewa thawabu kubwa zaidi..Bwana atusaidie tufike huko.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE UNAMTHAMINI BWANA?

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

JE! KUBET NI DHAMBI?

Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/06/08/vita-vya-imani-ni-vita-endelevu/