MATENDO YETU YANAPIMWA KATIKA MIZANI.

by Admin | 5 July 2020 08:46 pm07

Ukisoma katika biblia utakuta kuna mahali Bwana alikuwa anasema maneno haya…

1Wafalme 16: 25 “Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia”

1Wafalme 16: 30 “Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana kuliko wote waliomtangulia”.

Utaona hapo huyo Mfalme aliyeitwa Omri alifanya machukizo makubwa kuliko baba zake waliomtangulia…na anakuja kupata mtoto anayeitwa Ahabu na huyo mtoto anafanya naye mabaya kuliko yeye na wote waliomtangulia…Maana yake ni kwamba hali ya mtoto inakuwa ni mbaya kuliko ya mzazi, na ya mjukuu ni mbaya kuliko ya Baba na babu.

Sasa unaweza kujiuliza ni kwanini Bwana aweke hilo neno “ naye akafanya mabaya kuliko wote waliomtangulia”?..Jibu ni kwasababu matendo yetu yanapimwa yakilinganishwa na ya waliotutangulia..

Kama baba kaua mtu mmoja, na mtoto wake akaua wawili…basi maasi ya mtoto yamezidi yale ya Baba mara mbili…yaani kama yangewekwa katika mizani basi mzigo wa mtoto ni mkubwa kuliko wa Baba.

Kadhalika kama mtoto kafanya mema kuliko baba yake basi matendo yake kama yakiwekwa katika mizani yataonekana yamezidi ya Baba yake…na kama Baba yake amefanya mema kuliko yeye basi matendo ya Baba yake katika mizani ya kimbinguni ni mazito kuliko ya mtoto, na hivyo ya mtoto yataonekana yamepunguka…

Ndicho kilichomtokea Mfalme Belshaza wa Babeli…Mfalme huyu ijapokuwa alikuwa anayajua matendo ambayo Mungu wa Israeli alimfanyia Baba yake…lakini bado matendo yake yalikuwa maovu kuliko baba yake…Na mema yake yalionekana ni pungufu kuliko mema ya Baba yake katika mizani ya kimbinguni. Kwani Baba yake alimheshimu Mungu lakini yeye hakumweshimu na kwenda kuvichukua vyombo vitakatifu na kuvitumia kwa karamu zake za kiasherati.

Na Bwana akamwambia maneno haya..

Danieli 5:27 “TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka”.

Maana yake ni kwamba matendo mema aliyoyafanya baba yake yamezidi ya kwake…Bwana Mungu alitegemea matendo ambayo angeyafanya yazidi ya baba yake lakini kinyume chake yamepungua, na hivyo akamhukumu.

Biblia inasema….

2 Samweli 2:3 “Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, NA MATENDO HUPIMWA NA YEYE KWA MIZANI”.

Ndugu matendo yetu yanapimwa katika mizani kila siku yakilinganishwa na ya wengine kama sisi…kizazi chetu kinapimwa katika mizani kikilinganishwa na vizaza vilivyotangulia..

Mathayo 12:41 “Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona”.

Mahali tunapoishi, tunapofanyia kazi tunapimwa…kila tunalolifanya linapimwa linalinganishwa na la wengine. Hata maisha tunayoishi sisi kama wakristo yanapimwa ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5:20 “Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”.

Unapovaa suruali binti wa Mungu ambaye umezaliwa katika mazingira ya kikristo, pengine hata baba yako ni mchungaji…na unasema unakwenda mbinguni…ukumbuke kuna mwingine kama wewe mwenye umri kama wa kwako mahali fulani ambaye ni mzuri kuliko wewe na mwenye umbo zuri kuliko lako lakini havai hizo suruali wala vimini, ingawa mazingira yote yanamruhusu kufanya hivyo…yeye ameshinda katika mazingira magumu ya vishawishi vingi lakini wewe umeshindwa katika mazingira marahisi..Jua upendo wako kwa Mungu unapimwa!.

Unaposhindwa kumtafuta Mungu kwa kazi yako unayofanya masaa 8 tu kwa siku, na kusema upo bize sana…kumbuka kuna mwingine aliye bize kuliko wewe mwenye kufanya kazi masaa 10 mahali pengine lakini hakosi ibada, wala hakosi muda wa kusali na kuomba na kusoma Neno…ingawa anachoka kulko wewe…Fahamu kuwa upendo wako unapimwa!

Hivyo ndugu huu ni wakati wa kujipima kabla ya kupimwa!…na kujitathimini upya…

Kumbuka siku zote, usilisahau hili Neno utembeapo, uishipo…matendo yako yanapimwa katika mizani.

Ayubu 31: 5 “Kwamba nimetembea katika ubatili, Na mguu wangu umeukimbilia udanganyifu;

6 (Na nipimwe katika mizani iliyo sawasawa, Ili Mungu aujue uelekevu wangu);

Bwana atubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! Mwanamke anapaswa afunikwe kichwa anapokuwa ibadani?

KISIMA CHA MAJI YA UZIMA NI KILE KILE CHA ZAMANI.

NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/05/matendo-yetu-yanapimwa-katika-mizani/