HUYU SI YULE SEREMALA, MWANA WA MARIAMU?

by Admin | 16 July 2020 08:46 pm07

Shalom.

Kulikuwa na sababu kwanini Yusufu awe seremala, vilevile kulikuwa na sababu pia kwanini Bwana wetu Yesu Kristo naye pia awe seremala, na sio kazi nyingine, kabla ya yeye kuanza huduma.

Tunayasoma hayo katika..

Marko 6:3 “HUYU SI YULE SEREMALA, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake”.

Soma tena..

Mathayo 13:55 “HUYU SI MWANA WA SEREMALA? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?”

Unaona Yesu na baba yake wote walijulikana sana mpaka kupata umaarufu kutokana na hiyo kazi yao ya Useremala, bila shaka walikuwa ni wabunifu wazuri sana, uundaji wao ulikuwa wa kipekee. Kama tunavyofahamu kazi hii, inakuwa ni pale mteja anakuja na mchoro wake na kutaka atengenezewa kitu Fulani, labda meza ya muundo fulani, au kiti au kabati zuri lenye shelfu 6 la nguo na vyombo..Sasa yeye akishamaliza kutoa maelezo yake, au mchoro wake, kwa upande wa pili anapigiwa gharama zote za material kisha anaacha pesa ya awali(advance), Halafu anaambiwa arudi labda baada ya wiki 2..

Huo muda ukishapita anarudi na kukuta kabati lake lipo tayari,safi kabisa limekamilika, anamalizia kiwango cha pesa alichobakisha, kisha analichukua kabati lake, anaondoka analipeleka nyumbani au ofisini.. Lakini ni rahisi kuliangalia ukaona kama ni kazi nyepesi, hajui taabu walisumbuka nayo wale maseremala.

Sasa Mungu kumpitisha Bwana Yesu katika ujenzi tena wa kazi ambayo ilikuwa tayari ni ya baba yake, Ni kumuonyesha kuwa upo ujenzi atakaopaswa aufanye wa kanisa ambalo kwanza lilikuwa ni la baba yake mbinguni..

Yesu kama seramala alijua ili kabati liundike, sio kusimamisha tu gogo,.. bali ilihitajika misumeno ipite, lilihitaji kufanyike vipimo vya hali ya juu, kama pa kuongezwa paongezwe na kama pa kupungwa papunguzwe,..Vilevile ilihitajika Nyundo, na misumari ya kutosha ihusike,…Na hiyo yote ni kufatana na kile alichokiona kikifanywa na baba yake au maagizo ya baba yake, na sio yake mwenyewe.

Na ndio maana alisema..

Yohana 5:19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.

20 Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu”.

Hivyo hata Kristo alipoanza kuijenga nyumba ya Mungu(Kanisa), alilijenga kwa maagizo ya baba yake, aliposema mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane nafsi yake, ajitwike msalaba wake anifuate, alimaanisha, maagizo hayo hakujitungia mwenyewe bali aliyapokea hayo kutoka kwa Baba yake.

Aliposema aaminiye na kubatizwa ataokoka, hakujitungia mwenyewe, bali vipimo hivyo alivitoa kwa Baba yake. Kwamba ili mtu astahili uzima ni sharti amwaminiye yeye, na vilevile akabatizwe kihalili kama ipasavyo.

Aliposema duniani mna dhiki, lakini jipeni moyo,mimi nimeushinda ulimwengu, mambo hayo alionyeshwa na Baba yake kwamba kuna wakati watu wake watapaswa wapitie nyundo, na misumari mikali, na misimeno, kama yeye alivyopitia, ili wakamilishwe.

Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake”

Hivyo ndugu yangu, hata mimi na wewe leo, hatuna budi kumruhusu Kristo ambaye ndiye seremala mkuu na mwaminifu wa maisha yetu atuunde tuwe kama Mungu apendavyo, tunapopitishwa na yeye katika moto, tustahimili, tunapopitishwa na yeye wakati mwingine katika dhiki, vilevile tustahimili, kwasababu tutakapokamilishwa, tutakuwa vyombo vyenye thamani nyingi sana..

Mambo hayo tutayajua vizuri tutakapofika ng’ambo kwa yale mema mazuri Mungu aliyotuandalia. Kwasababu huo ujenzi wake hauishii tu kwenye maisha yetu, bali pia kwenye Makazi yetu ya milele, aliyokwenda kutuandalia..

Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.

4 Nami niendako mwaijua njia”.

Bwana akubariki.

Je! Umeyakabidhi maisha yako kwake?. Kama bado basi wakati wako ndio huu. Usisibiri wakati mwingine, kwasababu huo hautafika. Fanya uamuzi sasa wa kumgeukia yeye aliye mkuu wa uzima, ambaye aliyatoa maisha yake kwa ajili yako, ili upokee maisha ya milele. Natumai leo haitapita bila kumkaribisha Kristo ndani yako.

Waebrania 12:3 “Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

WAKATI WA BWANA KUKUVUSHA, NI LAZIMA ARUHUSU JESHI LA ADUI KUNYANYUKA.

HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

TUNAMHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUYAELEWA MAANDIKO.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/07/16/huyu-si-yule-seremala-mwana-wa-mariamu/