Mlima sinai upo nchi gani? Na Je unaijua Sinai yako ya rohoni?

by Admin | 18 August 2020 08:46 pm08

Mlima sinai upo nchi gani? Na Je unaijua Sinai yako rohoni?


Mlima Sinai, au kwa jina lingine unajulikana kama Mlima Horebu, upo katika Rasi ya Sinai, Nchi ya Misri..Tazama katika picha.

sinai

Mlima huu, ni mlima ambao Mungu aliutumia kuwapa wana wa Israeli Torati na zile Amri 10. Ni mlima ambao wana wa Israeli waliutazama kwa muda mrefu kama mlima ambao unamtambulisha Mungu yupoje pale anapotaka kuzungumza na watu wake. Kufuatana na mstari huu;

Kutoka 19:16 “Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka.

17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. 18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.

19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti.

20 Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu”.

Unaona, wana wa Israeli walijiundia picha kuwa siku zote Mungu akishuka mahali kuzungumza na mtu/watu ni lazima kuwe na moto, na matetemeko, na upepo mkali n.k. .

Eliya naye alidhani vivyo hivyo, wakati mmoja alipokuwa anamkimbia Yezebeli, alienda kwenye mlima huu wa Musa, mlima Sinai (Horebu) kwa ajili ya kukutana na Mungu, Na yeye akidhani kuwa ili Mungu ashuke mahali Fulani ni lazima uwepo moto, na matetemeko ya ardhi. Lakini siku hiyo alipokwenda kwenye mlima huo ndio alijua ukweli wote wa Mungu.

Ni kweli kama ilivyo ada, Mungu alijifunua kwake kama alivyojifunua kwa Musa na Wana wa Israeli kwa radi, mingurumo n.k. Lakini Eliya aligundua mbona bado simwona MUNGU?

1Wafalme 19:8 “Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.

9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya?

10 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.

11 Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;

12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.

13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya”?

Unaona Eliya alipoisia tu ile sauti ya utulivu na upole. Hapo ndipo alipousikia uwepo wa Mungu ukibubujika ndani yake akajua sasa Mungu ameshuka kuzungumza na mimi.. Hapo ndipo alipofahamu  kuwa Mungu hakai katika milima, hakai katika tufani, hakai katika upepo wa kisulisuli, bali katika utulivu na upole.

Vivyo hivyo na wewe leo hii unahitaji kumwona Mungu, unahitaji kukutana na Mungu katika Sinai, yako..Basi jifunze kujinyenyekeza mbele zake, kaa katika utulivu mkubwa wa Roho, huku ukijifunza kanuni za Mungu katika maandiko, na hakika atajifunua kwako zaidi hata ya alivyojifunua kwa wana wa Israeli. Mungu ni mnyenyekevu na hivyo anajifunua kwa wanyenyekevu kwake, wanaolitii Neno lake.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Israeli ipo bara gani?

Neno Korbani linamaanisha nini? (Marko 7:11)

SAYUNI ni nini?

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/08/18/mlima-sinai-upo-nchi-gani-na-je-unaijua-sinai-yako-rohoni/