JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

by Devis Julius | 17 September 2020 08:46 pm09

Katika biblia shetani amepewa majina tofauti tofauti na hiyo ni kutokana na aina ya kazi anazozifanya hapa duniani, kwamfano biblia inapomwita shetani/ibilisi ni kwasababu ni mpinzani na mshitaki wa roho zetu kwa Mungu ndio tafsiri ya jina hilo,.

Vilevile sehemu nyingine inapomwita Joka (Ufunuo 12), ni kwasababu ni mwongo kama alivyokuwa nyoka, na anameza roho za watu kama majoka yafanyavyo kumeza wanyama,..

Bado sehemu nyingine inamwita, mkuu wa ulimwengu huu, (Yohana 12:31,2Wakorintho 4:4), kwasababu mambo yote yaliyotukuka ulimwenguni sasa yanashikiliwa na yeye, yeye ndiye kiongozi wa hayo ..

Pia inamwita mfalme wa uweza wa anga (Waefeso 2:2) kwasababu nguvu zote za giza katika ulimwengu wa roho anazishikilia yeye, baba wa mapepo na wachawi duniani.

Vilevile sehemu nyingine inamwita mjaribu (Mathayo 4:3,1Wathesalonike 3:5), kwasababu, yeye ndio chanzo cha majaribu yote kwa mkristo..Na ndio maana Bwana Yesu alituambia kesheni mwombe msije ingia majaribuni..Kwasababu tusipoomba huyu atapata nafasi kubwa ya kutuletea majaribu ili kutuangusha.

Lakini zaidi ya yote biblia inatuonyesha kuwa atakuja kuwa na jina lingine, lijulikanalo kama Abadoni au Apolioni,.. Tafsiri ya jina hili ni MHARIBIFU…Ikiwa na maana atakuja kuwa na kazi ya kufanya uharibifu tu.

Kama leo hii unamwona shetani ni mharibifu, basi bado haujajua vizuri uharibifu wake upoje.

Tukisoma kitabu cha ufunuo, kama tunavyojua mara baada ya unyakuo wa kanisa kupita, kutafuata matukio ambayo hayaelezeki kwa namna ya kawaida. Tukiachana na yale mapigo ya vile vitasa 7 na ile siku ya Bwana mwenyewe ambayo jua hili litaondolewa, kutatangulia kwanza mapigo ya baragumu 7,..Sasa hatuwezi kuyachambua yote hapa, ikiwa utahitaji somo lake utuambia inbox tukutumie..

Lakini leo tutatazama, baragumu la tano, ambalo ndio kiini cha somo letu la Leo. Baragumu hilo litakapopigwa, biblia inatuambia, Shimo la kuzimu litafunguliwa na humo watatoka nzige wabaya sana..tusome;

Ufunuo 9:1 “Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu.

2 Akalifungua shimo la kuzimu; moshi ukapanda kutoka mle shimoni kama moshi wa tanuru kubwa; jua na anga vikatiwa giza kwa sababu ya ule moshi wa shimoni.

3 Nzige wakatoka katika ule moshi, wakaenda juu ya nchi, wakapewa nguvu kama nguvu waliyo nayo nge wa nchi.

4 Wakaambiwa wasiyadhuru majani ya nchi, wala kitu cho chote kilicho kibichi, wala mti wo wote, ila wale watu wasio na muhuri ya Mungu katika vipaji vya nyuso zao.

5 Wakapewa amri kwamba wasiwaue, bali wateswe miezi mitano. Na maumivu yao yalikuwa kama kuumwa na nge, aumapo mwanadamu.

6 Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia.

7 Na maumbo ya hao nzige yalikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita, na juu ya vichwa vyao kama taji, mfano wa dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama nyuso za wanadamu.

8 Nao walikuwa na nywele kama nywele za wanawake. Na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9 Nao walikuwa na dirii kifuani kama dirii za chuma. Na sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya magari, ya farasi wengi waendao kasi vitani.

10 Nao wana mikia kama ya nge, na miiba; na nguvu yao ya kuwadhuru wanadamu miezi mitano ilikuwa katika mikia yao.

11 Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni ABADONI, na kwa Kiyunani analo jina lake APOLIONI.

Sasa hapa biblia imetumia tu lugha ya mfano ili upate halisi ya jinsi mambo yatakavyokuwa.. Hapo anasema wakatoka nzige..Sasa hao sio nzige halisi bali hayo ni Mapepo (maroho) ambayo kwasasa yapo kifunguni..Kumbuka si idadi yote ya mapepo yafayanyayo kazi sasa, yapo mengine mengine yapo kifungoni, biblia inasema hivyo katika kitabu cha Yuda.

Sasa mapepo hayo Yamefananishwa na wale Nzige waharibifu wa mazao, na ulimwengu umefananishwa na shamba lenye mazao (Mathayo 13:38) Na kama unavyojua nzige wakipita mahali kwenye mazao ya kijani, kitendo cha masaa machache tu, hilo shamba linageuka na kuwa vijiti tu.. Ni tishio kubwa sana duniani hata sasa, fuatilia tu habari ya nzige wa jangwani walipopita Afrika Mashariki kipindi cha hivi karibu uone uharibifu wao ulivyokuwa tishio.

Sasa tunajuaje kama haya ni mapepo na si nzige halisi, ni kwasababu hayajapewa kudhuru nchi, bali wanadamu ambao hawana muhuri wa Mungu duniani. Kazi hiyo huwa inafanywa na shetani mwenyewe na malaika zake, Soma Ufunuo 7 utaona hao ambao watakuwa wameitiwa muhuri ni wakina nani. Lakini kama ikitokea unyakuo leo hii umekupita, ujue kuwa mambo hayo yatakukuta tu..

Mapepo haya yatakayoachiliwa kutoka kuzimu na moja kwa moja yatapokea oda kutoka kwa kiongozi wao mkuu shetani/Apolioni/Abadoni, kwa lengo la KUWAHARIBU wanadamu tu. Kama jinsi atakavyojulikana kwa jina hilo.

Mapepo haya yatawaingia watu, bila kizuizi chochote, mengine yatawafanya watu kuwa vichaa, na kuwatesa tu kama yalivyomtesa Yule bwana aliyekutana na Yesu kule makaburini, mengine yatawafanya watu wawe wakatili kupita kiasi, kuchukiana kitaongezeka mara nyingi zaidi, kugombana, kuumizana, na kuuana n.k. mengine yatawafanya watu wapate ajali lakini si za kuwaua, bali za kuwaumiza tu vibaya..

Mengine yatawaletea watu magonjwa yasiyo ya kawaida lakini hakuna kifo, kama vile wakati wa Ayubu, siku hiyo kama hukwenda kwenye unyakuo utakaa kwenye majivu ya kila namna kujipoza lakini wapi, utatamani kufa lakini kifo kitakukimbia, yaani kwa ufupi duniani kutakuwa na watu ambao si watu, maroho hayo yatafanya uharibifu usio kuwa wakawaida.

Mioyo ya wanadamu itaharibiwa kwa kiwango cha juu sana, na kama vile yanavyofananishwa na nzige maana yake ni kuwa mpaka hicho kipindi chao kiishe, watu watakuwa kama makapi tu, wamechoka sana..

Huo wakati ndugu yangu, si wa kuwepo, ukisikia hizi ni siku za mwisho, usidhani unyakuo ukishapita mambo yatakuwa kama unavyoyaona leo.. Ni Roho Mtakatifu ndani ya kanisa lake ndiye anayezuia hayo mambo kwasasa. Lakini kuna wakati utafika, ataondolewa, na akiondolewa anaondoka na kanisa lake takatifu (Ndio unyakuo wenyewe).Kitakachosalia duniani ni vilio tu na kusaga meno (Mathayo 25:30).

2Wathesalonike 2:5 “Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; LAKINI YUKO AZUIAYE SASA, HATA ATAKAPOONDOLEWA”.

Swali la kujiuliza, Je! Bado tunaudharau wokovu wa Yesu?.

Je! Bado tunaishi maisha ya kutokujali, mpaka haya mambo yote yatukute? Kama ndivyo ni heri tuyakabidhi maisha yetu kwa Bwana leo, ayaokoe. Vilevile tukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na Kwa jina la YESU KRISTO tupate ondoleo la dhambi zetu. Bwana wetu ni mwingi wa huruma, anatuonya mbele kabla ya mambo hayajatokea kwa ghafla. Hivyo mpokee Kristo leo na atakufanya kiumbe kipya, ulimwengu unapita na mambo yake yote, lakini Kristo na Neno lake wanadumu milele. Na yeye anatuambia itatufaidia nini kuupata ulimwengu mzima na kupata hasara za nafsi zetu?

Bwana atusaidie, Bwana atubariki sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

AMELAANIWA AANGIKWAYE MSALABANI.

UFUNUO: Mlango wa 10.

Nini maana ya maneno haya ya Bwana? “Nami nikiinuliwa juu ya nchi,NITAWAVUTA WOTE KWANGU”(Yohana12:32).

Areopago ni nini? Kwanini mtume Paulo walimpeleka huko?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 8 (Kitabu cha Ezekieli)

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/17/jina-lake-kwa-kiebrania-ni-abadoni-na-kwa-kiyunani-ni-apolioni/