TAFUTA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KWA HUDUMA MUNGU ALIYOIWEKA NDANI YAKO.

by Admin | 21 September 2020 08:46 pm09

Tunamtumikia Mungu kwa karama tulizopewa, na karama ndizo zinazozaa Huduma..Na Karama za Roho Mtakatifu zimefananishwa na viungo katika miili yetu. Maana yake tukijifunza kwa kina jinsi viungo vya miili yetu vinavyofanya  kazi basi tutakuwa tumeelewa vyema pia jinsi karama za Roho zinavyotenda kazi.

Warumi 12:4  “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja.

5  Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake”

Tabia moja ya kipekee ya viungo vya mwili ni kwamba kila kiungo kipo kwaajili ya kuvisaidia viungo vingine…Kwamfano Miguu utaona ipo kwa kazi ya kuubeba mwili, haipo kwa kazi ya kujibeba yenyewe..Mikono ni hivyo hivyo, ipo kwa kazi ya kuhudumia mwili sehemu mbalimbali kama kupeleka chakula mdomoni, kuosha mwili, kuchana nywele n.k..

Vile vile macho yapo si kwaajili ya kujiangalia yenyewe, bali kwaajili ya kutazama mambo yanayoendelea katika mwili na nje ya mwili na hivyo kupeleka taarifa kwenye ubongo. Masikio hayapo kwaajili ya kujisikia yenyewe, wala ngozi haipo kwaajili ya kujifunika yenyewe, bali kuufunika mwili na viungo vya ndani.

Moyo haudundi kujifurahisha, au kujipa burudani, bali unafanya vile kuhakikisha unasukuma damu katika viungo vyote vya mwili. Na viungo vingine vyote ni hivyo hivyo, vipo kwaajili ya kusaidia viungo vyenzake.

Na karama za rohoni zinatenda kazi kwa namna hiyo hiyo. Ukiona mahali hakuna kusaidiana basi hapo kuna kasoro, Roho wa Mungu hayupo hapo, lakini mahali ambapo Roho Mtakatifu yupo ni lazima viungo vyote visaidiane.

Ukiona ndani yako huna msaada wowote katika mwili wa Kristo, au huhitaji msaada wowote basi huo ni uthibitisho kwamba wewe ni kiungo kilichokufa na tena kimezikwa.. Kwasababua hata mkono uliokufa haufanyi chochote, na kama umekufa muda mrefu basi maana yake ni kwamba umeshaoza na kilichobakia ni mifupa tu..

Vivyo hivyo kama huna msaada wowote katika Mwili wa Kristo wewe ni mifupa katika roho, na usifurahie kuwa katika hiyo hali, ni afadhali ukafufuka leo!.

Utasema mimi siijui karama yangu! Hivyo nasubiri Mungu anifunulie kwanza.

Ndugu hakuna kitu kinakuja kwa kukaa tu na kukisubiri…Wengi wanakaa tu wakisubiri Mungu awafunulie karama zao, (Wengine wanafanya hivyo kwasababu hawajui na wengine ni wavivu). Nataka nikuambie mtu wa Mungu kama ulikuwa unakaa kusubiri kwasababu hujui basi nataka nikuambie usiendelee kusubiri kwasababu utakaa sana, na wala hutaona chochote…kila siku utabaki ukikisia tu labda ni hii, au ile.. utabaki ukihuzunika unapoona wengine wanafanya kazi ya Mungu na wewe hufanyi chochote..Hivyo usibaki kusubiri!. (Kasome hichi kisa 2Wafalme 7:1-15 )

Kuifahamu karama yako hakuji kwa namna hiyo (ya kusubiri), kunakuja kwa wewe kujiingiza kwenye kazi yoyote au huduma yoyote ya Mungu ambayo inaona inafunguka mbele yako, na huko huko utaona kuna mahali umefit vizuri!..utaona kuna mahali unafanya vizuri na  kwa furaha zaidi ya wengine na tena unafanya kwa ubora na pasipo kusukumwa..Utaona Mungu anaanza kukufungulia milango na kukupa akili na uwezo wa kutumika katika hilo eneo siku baada ya siku. Ukiona umefikia hiyo hatua, basi hapo huenda ndio mahali huduma yako ilipo, usianze kunia Makuu na kutamani makubwa, anza na hicho hicho chako kwasababu ni muhimu sana katika Mwili wa Kristo kwaajili ya kuwahudumia watu wake, na siku zinavyozidi kwenda Kristo atazidi kukistawisha.

Usisubiri maono wala kuoteshwa ndoto wala kutokewa na Bwana au malaika!..Je siku ulipokwenda kutafuta kazi ulisubiri maono au ndoto?. Vivyo hivyo katika kuifanya kazi ya Mungu hatuenendi kwa kuona bali kwa IMANI. (2Wakorintho 5:7).

Sasa utaanzaje safari ya kuilelekea huduma yako Mungu aliyoikusudia?

Kwanza kabisa, jichanganye na watakatifu mahali unapoabudu na mahali unapoishi, au popote pale unapoweza kukutana nao (Usijitenge wala usijione bora).. Shiriki nao katika kazi wanazozifanya za kanisa au za kihuduma, popote pale ambapo unaona unaweza kuchangia mawazo yako, au ujuzi wako, au chochote kile, wewe changia!. Utaona pale ulipochangia pengine mawazo yako yamekuwa bora mara nyingi kuliko ya wengine, au pale ulipotumia ujuzi wako au elimu yako pameleta matokeo makubwa sana, na hivyo pakafanya uwepo wako uwe wa muhimu sana..n.k

Kwamfano unaweza kuingia kwenye kundi, katikati huko ukasikia kuna mtu fulani alipatwa na matatizo haya na yale hivyo sasahivi yupo katika masononeko makubwa, wameenda watu kumfariji lakini wapi!..na hata kashafikia hatua ya kukata tamaa na kurudi nyuma, sasa wewe kama karama yako ni faraja, utaona kuna kitu kitakuchoma ndani..na kujisikia huruma mara mbili zaidi ya wenzako, na kutafuta kwenda kumsaidia yule mtu, na utashangaa umemrudisha na amerudia katika hali yake, na watu wote wanashangaa umewezaje! ..ukishaanza kuona hizo hali za kuweza kufanya kitu ambacho ni kigumu kwa wengine kukifanya lakini wewe umeweza tena kwa ufasaha!, basi huo ni uthibitisho kuwa haupo mbali na huduma yako. Ukifikia hiyo hatua utaona Bwana ataanza kukusafishia njia zaidi ya kuliendea kusudi alilokuitia utaona hekima inazidi kuongezeka juu yako siku baada ya siku, na utaona majukumu ya wewe kuifanya hiyo kazi ya Mungu yanazidi kuongezeka, utaona mzigo unazidi kuongezeka ndani yako..Na mwisho wa siku Mungu ataweka ndani yako UZIO.

Uzio ni hali fulani ambayo inawatokea watumishi wa Mungu, ambao ikipita siku au masaa hawajafanya kazi ya Mungu, wanasikia hali moja mbaya sana, hata kufikia KUUMWA! au kuishiwa nguvu za Mwili. Ndio kama ile hali ya Bwana aliyosema katika Yohana 4:34  “Yesu akawaambia, Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake”.

Kazi ya Mungu inakuwa kama ni chakula kwao!. Hivyo hiyo hali ni kama ishara ya kumsaidia mtu wa Mungu asitoke nje ya mstari. Hivyo ikitokea amemaliza siku moja au mbili hajatumika kabisa katika kazi yake hiyo, hali ya mwili wake inaanza kumbadilikia na hivyo inamfanya siku zote aifanye kazi ya Mungu kama vile ni chakula chake.

Sasa kumbuka kama tulivyotangulia kusema..Karama na huduma ni kwaajili ya masaidiano na si kwaajili ya kujisaidia mwenyewe.. Kwahiyo ukiona umeingia kwenye huduma fulani katikati ya watakatifu na moyo wako unaelekea kupata pesa, au kupata umaarufu wako binafsi na si wa Kristo, au kupata jina au cheo, au umaarufu..basi jua hiyo ni roho nyingine ya Adui ipo ndani yako, ambayo shetani kakupandikizia, na lengo la roho hiyo ni kwenda kuliharibu kundi la Mungu

Lakini ukiona ni kwenda kusaidia watakatifu na watu wengine, basi zidi kufanya mbele ya safari Bwana atakufungulia milango zaidi.

Ndugu kama ulikuwa unasubiria maono ndipo uanze kuifanya kazi ya Mungu, leo umejua…usisubiri, jiunganishe na wanaofanya kazi za Mungu na huko huko Bwana atakusafishia njia..Lakini pia kabla ya kwenda huko kama hujaokoka! Ni vyema ukafanya hivyo leo, kwasababu huwezi kwenda kufanya kazi ya mtu ambaye hampatani. Hivyo ni lazima umkubali ndipo ukafanya kazi zake, hivyo mpokee leo Kristo moyoni mwako, na kisha katafute kubatizwa na Roho Mtakatifu atakuongoza katika njia unayoiendea.

Tafuta kwa bidii kuifanya kazi ya Mungu, na Mungu atakuheshimu.

Bwana akubariki!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

MTU ASIYE PAMOJA NAMI YU KINYUME CHANGU.

Je Mungu anawapenda watu wote au ana chuki?

JE NI LAZIMA MKRISTO AOE/AOLEWE?

LOLOTE ATAKALOWAAMBIA FANYENI.

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/09/21/tafuta-kuifanya-kazi-ya-mungu-kwa-huduma-mungu-aliyoiweka-ndani-yako/