USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

Usipokuwa mwaminifu sasa, nafasi yako itachukuliwa na mtu mwingine.


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Mkuu wa Uzima libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia Neno la Mungu..Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Leo tutajifunza madhara ya kutokuwa mwaminifu katika kazi ya Mungu… Kuna tofauti ya utendaji kazi kati ya mtu na mtu…Mtu anatenda kazi ya Mungu kulingana na karama aliyopewa. Hivyo kama mtu kapewa karama Fulani halafu karama ile haitumii au anaitumia isivyopaswa basi kuna madhara makubwa sana…Na moja ya dhara hilo ni nafasi yake kunyang’anywa na kupewa mwingine.

Na kitu cha kuogopesha ambacho watu wengi hawakifahamu ni kwamba Mungu kamwe hamnyang’anyi mtu karama…bali anamnyang’anya ile huduma…Yaani ile Neema ambayo Mungu angetembea naye kwa karama aliyompa..Neema hiyo anapewa mwingine ambaye atazaa Zaidi lakini yule mtu ataendelea kukaa na karama yake ile ile lakini hatatumika katika viwango ambavyo Mungu alikuwa amemkusudia atumike. Kama alikuwa na karama ya kinabii..ataendelea kuona maono..Lakini lile kusudi kuu ambalo Mungu alilikusudia kumtumia kwa karama ile linahamishiwa kwa mtu mwingine.

Katika Biblia tunamwona mtu mmoja aliyeitwa SAULI ambaye alipakwa mafuta na Mungu mwenyewe, na Roho wa Mungu akamshukia juu yake kwa nguvu ile awe mtawala juu ya Israeli. Lakini pamoja na kuwa alitiwa mafuta na Mungu mwenyewe na Mungu alimnyanyua kutoka chini, na kupewa uweza na nguvu nyingi..lakini mtu yule hakuitumia vyema nafasi yake, aliacha kumheshimu Mungu na kumtii…Mungu akimwambia afanye hivi..yeye anafanya vile..na kile asichopaswa kukifanya ndicho alichokuwa anakifanya, na alikuwa anafanya vile kwa makusudi. Jambo ambalo lilimhuzunisha Mungu na kufikia hatua ya kuondoa nafasi yake na kumpa mtu mwingine.

1Samweli 15:24 “Ndipo Sauli akamwambia Samweli, Nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya Bwana, pia na maneno yako; kwa sababu naliwaogopa wale watu, nikaitii sauti yao.

25 Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu; rudi pamoja nami, nipate kumwabudu Bwana.

26 Samweli akasema, Sitarudi pamoja nawe; kwa sababu umelikataa neno la Bwana, Bwana naye amekukataa wewe, usiwe mfalme wa Israeli.

27 Naye Samweli alipogeuka, aende zake, Sauli akaushika upindo wa vazi lake, nalo likararuka.

28 Basi Samweli akamwambia, Leo Bwana amekurarulia ufalme wa Israeli, naye amempa jirani yako, aliye mwema kuliko wewe.

29 Tena Yeye aliye Nguvu za Israeli hatanena uongo, wala hataona majuto; maana siye mwanadamu, hata ajute”.

Wakati Sauli anaidharau hiyo nafasi aliyowekwa..Tayari Mungu alikuwa ameshamwandaa Daudi kuichukua nafasi yake.

Sulemani naye baada ya kutumika kwa muda mrefu..ilifika kipindi akakengeuka na kuitumikia miungu migeni jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya Mungu..Nafasi yake naye ikachukuliwa na mtumishi wake.

1Wafalme 11:11 “Kwa hiyo Bwana akamwambia Sulemani, Kwa kuwa umefanya hayo, wala hukuyashika maagano yangu, na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako”.

Na ipo mifano mingine mingi katika biblia..lakini wa mwisho tunausoma ni wa Yuda aliyekuwa mwanafunzi wa Yesu. Huyu naye alipewa nafasi katika huduma ya Kristo..lakini aliichezea na kuidharau nafasi ile..na mwishowe kufungua mlango wa roho ya shetani kumwingia ili kumsaliti Bwana..Na siku zote kazi ya Mungu haipwayi..

Wala hakuna mtu maalum kwa Mungu..ukikataa kumtumikia Mungu sasa..basi Mungu anao watu wengi, nafasi yako inachukuliwa na mtu mwingine…Yeye hana mtu mmoja tu au watu Fulani kadhaa anaowategemea kwamba wakikosekana hao basi kazi yake haiendi mbele. Nataka nikuambie hata Paulo angeukataa wito wa Mungu angenyanyuka mtu mwingine kuifanya kazi kama ile ile ya Paulo kwa wakati ule ule..Lakini Paulo na wengine wamekuwa vile walivyo kwasababu waliutii utumishi wa Mungu na kuuheshimu.

Matendo 1:15 “Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,

16 Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;

17 kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.

18 (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka………20 Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi, Kikao chake na kiwe ukiwa, Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo;

21 Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,

22 kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.

23 Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya.

24 Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,

25 ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. 26 Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.”

Umeona?..Mungu hakufanya kazi ya hasara…kumbe wakati Yuda anaanza kufikiria kumsaliti Bwana..Tayari Mungu alikuwa ameshaandaa mtu wa kuichukua nafasi yake tangu wakati ule ule…Huyu Mathiya alikuwa na Yesu tangu ubatizo wa Yohana mpaka kupaa kwake…alikuwa ameshawekwa tayari kuichukua nafasi ya Yuda.

Hata sisi leo hii, wapo watu waliowekwa tayari kuzichukua nafasi zetu, tangu siku ile tulipookoka..Tunapozichezea hizi nafasi tulizopewa sasa katika kumtumikia Mungu, katika kuhubiri injili, katika kuihudumia Injili..Siku inafika kinara kitaondolewa na kupewa mwingine ambaye tayari alikuwa ameshaandaliwa.

Mifano hiyo tuliyojifunza ni ya kwenye biblia..lakini tunaweza kujifunza mfano mwingine katika mtu wa nyakati zetu..Na huyu si mwingine ya Mhubiri wa Mungu mashuhuri Reinhard Bonnke…ambaye wengi wetu tunamfahamu, ambaye wiki kadhaa nyuma tulisikia habari za kufariki kwake. Huyu mwanzoni mwa huduma yake kabla hajaingia kwenye kazi ya kuwavuna mamilioni ya watu kwa Kristo, alikuwa anasua sua kidogo. Mungu anamwita kufanya kazi ya kupeleka injili kwa mataifa ya Afrika ili mamilioni waokolewe..lakini yeye akawa anakawia kawia na kujishauri shauri kana kwamba yeye ni mtu maalumu sana.

Wakati bado yupo anajifikiria fikiria, siku moja alisikia sauti inamwambia “nafasi hiyo nimekupa kwasababu kuna mwingine alipewa akaikataa, na wewe ukiikataa atapewa mtu mwingine”. Baada ya kusikia hivyo aliogopa sana..Ndipo akaamua kwa gharama zote kuifanya kazi ya Mungu ili nafasi yake isichukuliwe na mwingine..Na matokeo ya kutii kwake ndiyo tunayoyaona leo,..Mungu alimtumia kuvuna mamilioni ya watu Afrika waliokuwa wanakwenda kuzimu.

Hivyo na sisi tunajifunza..Kamwe tusijione ni watu maalum mbele za Mungu. Kamwe tusijidhanie ni sisi tu ndio Mungu anao..Mungu anao watu wake wengi, ambao wapo tayari kwa utumishi wake..Eliya Mtishbi kuna kipindi alikwenda kusimama mbele za Mungu na kumwambia.. “Ni mimi tu peke yangu nimebaki nabii wako” ..lakini Mungu alimwambiaje?

Warumi 11: 3 “Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.

4 Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali”.

Leo hii unajiona una kipawa cha kuimba..Wewe ukiimba watu wanatubu, lakini unavaa vimini, unapiga make-up, unavaa nusu uchi, ni mwasherati kwa sirisiri..umeonywa mara kadhaa lakini hutaki kusikia…Nataka nikuambie kamwe usijifikirie upo peke yako..Nafasi yako atapewa mtu mwingine.

Wewe ni Mchungaji, au Mwalimu, au Nabii au Mtume au Mhubiri…lakini chini kwa chini ni mwasherati, chini kwa chini ni unalivuruga kundi, chini kwa chini ni mtu wa kupenda anasa na mapato ya udhalimu, chini kwa chini ni mzinzi..unadhani Mungu hakuoni..Utamficha mwanadamu lakini si Mungu…Nafasi yako itachukuliwa na mwingine na pengine hata imeshachukuliwa hujui tu!..Unaweza ukawa bado unaendelea kuota ndoto, unaendelea kuona maono, unaendelea kuimba vizuri hiyo siyo hoja!…

Hata Sulemani aliponyang’anywa ufalme wake hakuondolewa kila kitu alibakishiwa hekima yake…hata Sauli aliponyang’anywa ufalme wake hakupokonywa siku hiyo hiyo alikufa akiwa mfalme, lakini kumbe tayari utukufu wa Mungu ulikuwa umeshamwondokea…Hata Yuda nia ya kumsaliti ilipoingia ndani yake Bwana hakumfukuza aliendelea kutembea naye lakini, utukufu ulikuwa tayari umeshamwondoka na siku ya mwisho alipasuka matumbo.

Hivyo sikia maonyo ya Mungu leo mtu wa Mungu, na Bwana azidi kutusaidia tudumu katika Neema yake kithabiti. Tukikumbuka kuwa muda tuliona nao ni mchache..Kristo yu malangoni kurudi.

Bwana akubariki.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

NI KIPI MUNGU ANACHOKITAZAMA ZAIDI, MOYO AU MWILI?

JUMA LA SABINI (70) LA DANIELI

MPINGA-KRISTO

UNYAKUO.

JE! UNA MASIKIO YANAYOSIKIA?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Pius matumla
Pius matumla
1 year ago

I real enjoyed the word of God be blessed May have more teaching in my email

Anonymous
Anonymous
3 years ago

Naomba nitumie mafundisho zaidii kwenye email yangu