Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

by Admin | 10 October 2020 08:46 pm10

SWALI: Biblia ina maana gani kusema “Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni” Je! si sahihi kutafuta hekima?

Mhubiri1:17 “Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.

18 Yaani, Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni, Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko”.

JIBU: Ukisoma Sura hiyo ya kwanza yote, na zinazofuata utaona Sulemani alikuwa anaeleza jinsi alivyojibidiisha katika kutafuta mambo ya ulimwenguni, na hekima yake na kazi zote “zinazofanywa chini ya mbingu (Mhubiri 1:13)”.

Lakini hasemi alikuwa anayatafuta  mambo ya ki-mbinguni, hapana, na ndio maana utaona kila mahali anaishia kusema ni ubatili mtupu, sehemu zote, yaani maudhui ya kitabu cha mhubiri kinaeleza hatma ya kazi zote na shughuli zote zinazofanywa na wanadamu chini ya jua, na ndio maana mwishoni kabisa  mwa kitabu hicho utaona sasa Sulemani anatoa jibu la jambo la muhimu ambalo mwanadamu anapaswa alitafute siku zote za maisha yake..Anasema na hilo si lingine zaidi ya kumcha Mungu basi. (Soma Mhubiri 12:13).

Sasa tukirudi kwenye mstari huo anaposema “Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni,Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko” Hamaanishi Hekima ya kimbinguni au maarifa ya kimbinguni,..Hapana!, kinyume chake hekima ya kimbinguni na maarifa ya kimbinguni ndio yanayomfanya mtu awe na amani na furaha na utulivu wa nafsi..Kumjua Yesu ambaye ndio hekima ya Mungu (sawasawa na 1Wakorintho 1:24), ni mwisho wa masumbuko yote, unakuwa umefunguliwa milele, hakuna huzuni yoyote wala masikitiko.. Unapolisoma gombo( ambalo ni Neno la Mungu), ndipo unapopata maarifa sahihi ya kuishi hapa duniani, na unafungua milango yote iliyofungwa.

Hivyo maarifa yanayozungumziwa hapo ni haya maarifa ya kiduniani tuliyonayo, kwasababu, pale mtu anapokuwa na elimu kubwa sana, inadhaniwa kuwa ndio itampa furaha ya kweli katika moyo wake, lakini matokeo yanaonyesha kuwa hilo sio kweli, Sulemani alilipata hilo akadhani ndio lingempa furaha aliyokuwa anaitazamia, lakini akagundua kuwa ni ubatili.

Ni jambo la kawaida, wanasayansi wanaokesha maabara usiku kucha, kutafiti na kugundua, asilimia kubwa huwa maisha yao sio ya furaha, kwasababu wanakuwa na hofu ya vitu vingi, hilo likitokea, au lile likizuka itakuwaje, maadui zetu wakitengeneza bomu la atomiki kama hili tunalotengeneza sisi itakuwaje? Dawa au kemikali hii madhara yake yatakuwaje miaka 10 mbele? N.k.n.k.. Maarifa yao na hekima zao zinapozidi kuongezeka huzuni nazo zinazidi kuongezeka…

Hivyo mwisho wa siku inakuwa ni huzuni juu ya huzuni tu na masikitiko juu ya masikitiko na ndio maana biblia inatuasa, tupende kuongeza maarifa kwa Mungu wetu zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote kwasababu huko ndiko tutapata furaha ya kweli idumuyo na utulivu na amani isiyoisha.

Bwana Yesu (ambaye ndio hekima ya Mungu) anasema;

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Kwa Bwana Yesu ndipo penye pumziko la kweli.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

WOSIA WA BWANA YESU KWA WANAFUNZI WAKE.

Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema; Mafarisayo Hupanua HIRIZI zao, na kuongeza MATAMVUA yao?

SIKUKUU YA VIBANDA.

BWANA alimaanisha nini kwenye mstari huu Marko 2:21″ Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kukuu;?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/10/nini-maana-ya-katika-wingi-wa-hekima-mna-wingi-wa-huzuni/