Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

by Admin | 17 October 2020 08:46 pm10

SWALI:  Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati” (1 Wakorinto:15:56)?.

JIBU: Pale Adamu alipoasi katika bustani ya Edeni, alipewa mapigo mawili makubwa…la kwanza Ardhi imelaaniwa kwa ajili yake, la pili ATAKUFA. Maana yake ni kwamba, Matokeo ya ardhi kulaaniwa ndio yale Bwana Mungu aliyoyataja pale kwamba atakula kwa jasho, maana yake ni kwamba ataishi lakini katika hali ya kuishi huko atakuwa katika mateso ya kuhangaika siku zote za Maisha yake, hatapumzika!.

Lakini pigo la pili aliloambiwa kwamba Atakufa, biblia haijataja matokeo yake…Maana yake ni kwamba nalo pia sio zuri, maana yake ni kwamba katika kufa huko pia sio kwamba atakwenda kustarehe na kupumzika. Hapana!.. Baada ya kufa atakwenda sehemu ya wafu nako huko sio sehemu ya kwenda kupumzika, bali pia kuna kutaabika baada ya kifo, kwasababu kifo ni pigo!.

Hivyo kabla ya Bwana Yesu mtu yeyote awe mkamilifu au mwovu baada ya kufa alikuwa anashuka sehemu ya wafu ambayo haikuwa salama sana, bado anaendelea kuitumikia laana, na shetani alikuwa anao uwezo wa kufika mahali wafu walipo, na baadhi yao kuwafanya anavyotaka..Sasa ili kuelewa vizuri kasome Habari za Samweli, jinsi shetani alivyomtaabisha kwa kumpandisha kutoka kwa wafu (kasome 1Samweli 28:15). Hivyo mauti ilikuwa ni sehemu chungu, kwasababu shetani alikuwa na mamlaka nako.

Mpaka Bwana Yesu alipokuja na kwenda kuzitwaa funguo za mauti na kuzimu, Ndipo ukatokea wokovu kwa wale watakaokufa katika haki, kwa kuhamishwa na kuwekwa sehemu salama inayoitwa Paradiso. Huko watapumzika bila kufikiwa na adui shetani, (kwasababu funguo anazo Kristo na si shetani tena, hivyo shetani hawezi kuwafikia wala hajui walipo), watakaa huko wakingoja ufufuo wa kwenda mbinguni, siku ile parapanda ya mwisho itakapolia, ambapo watafufuliwa na kuvaa miili yao ya asili kwanza, kisha ya utukufu itavikwa juu ya ile ya asili (ili ule unaoharibika uvae kutokuharibika, na mauti imezwe na uzima 1Wakorintho 15:54) na kisha wataungana na watakatifu walio hai, wote wakiwa na miili yao ya utukufu isiyoweza kuharibika wala kufa na kwa Pamoja watakwenda mbinguni.

Lakini wafu waliokufa katika dhambi (yaani ambao hawajamwamini Yesu), wanapokufa hawaendi paradiso bali kuzimu sehemu ya mateso ya muda, wakingojea kusimamishwa  siku ile katika kiti cha hukumu na kuhukumiwa kulingana na matendo yao, na kutupwa katika lile ziwa la moto Pamoja na shetani na malaiika zake.

Hivyo Mauti ina UCHUNGU kwa wale waliokufa nje ya Kristo, na kwa wale watakaokufa wakiwa hawajampokea Kristo. Kwasababu hata baada ya kufa wataendelea kuteseka.. Na uchungu huo unakuja ni kwasababu ya Maisha ya Dhambi waliyokuwa wanayaishi, hivyo baada ya kufa, watapata uchungu, Lakini kama wangeishi Maisha ya utakatifu ambayo yanakuja kwa kumpokea Bwana Yesu na kujazwa Roho Mtakatifu, basi wasingepata uchungu baada ya kifo, badala yake baada ya kifo wangepumzishwa mahali pa raha panapoitwa peponi/paradiso…sawasawa na andiko hili ….

“Ufunuo 14:12  Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.

13  Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, HERI WAFU WAFAO KATIKA BWANA TANGU SASA. NAAM, ASEMA ROHO, WAPATE KUPUMZIKA BAADA YA TAABU ZAO; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao”

Hiyo ndiyo sababu biblia inasema hapo katika 1Wakorintho 15:56 kuwa “UCHUNGU WA MAUTI NI DHAMBI”.. Maana yake tukifa katika dhambi, tutapata uchungu baada ya kifo.

Hapo ndipo utakapojua umuhimu wa Yesu Kristo upi?, na jinsi gani kama sio Baba kumleta ulimwenguni, shughuli yetu ilikuwa imekwisha!..tungekuwa hatuko salama hata baada ya kifo..Uchungu tungeendelea nao, baada ya kufa, na hiyo ingekuwa ni milele.

Kama utataka kujua mistari inayozungumzia Habari za Yesu kuzitwaa funguo za Mauti na kuzimu, na jinsi yeye mwenyewe alivyoshinda uchungu wa Mauti,.unaweza kusoma binafsi mistari ifuatayo.. (Matendo 2:23-27, Ufunuo 1:17-18, Warumi 14:8-9).

Sasa sehemu ya pili, inasema “NGUVU YA TORATI NI DHAMBI”..Maana yake ni Nini?

Ili tuelewe ni kwa namna gani, Torati au sheria ndiyo nguvu ya dhambi…Hebu tutafakari mifano ifuatayo..

Kama umewahi kuchunguza, mahali ambapo pamewekwa sheria kali, ndipo panapovuta umakini wa watu zaidi..Ukimwambia mtu usipite mahali hapa usiku, ndio kama umemtangazia apite..kwasababu kila siku atajiuliza kwanini yule anikataze nisipite pale usiku, kwani kuna nini…siku moja nitajaribu nipite kwa siri ili nijue ni nini kinaendelea pale. Umeona?..Hapo hiyo sheria uliyompa kwamba asipite mahali hapo usiku, tayari imemfungulia mlango wa kuivunja…Lakini kama usingemwambia hata asingehangaika kutafuta kupita mahali hapo usiku.

Vivyo hivyo, ukimwacha mtoto nyumbani na kumwambia ni marufuku kufungua kile chumba, ukikufungua ni utakuwa umefanya makosa!…Sasa kwa kumwambia vile ndio kama umemjulisha kuwa akatafute kukifungua hata kwa siri ili aangalie kuna nini ndani ambacho kinakatazwa kisiangaliwe, hivyo atajizuia siku ya kwanza, ya pili lakini siku moja atakuwa anajiuliza ni nini kipo kule, hivyo atatafuta hata kuchungulia tu.. “tayari kashaivunja ile sheria”.

Kadhalika sheria inaposema “Usizini” tayari imefungua mlango wa yule anayeambiwa usizini akazini…Ni hivyo hivyo na dhambi nyingine zozote..zinapata nguvu katika SHERIA au AMRI. Ndio maana Mtume Paulo kwa uongozo wa Roho alisema..

Warumi 7:8 “ Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. KWA MAANA DHAMBI BILA SHERIA IMEKUFA.

9 Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa”.

Warumi 7: 5 “ Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao”.

10  Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti”.

Hiyo ndio sababu Neno la Mungu linasema hapo.. “Nguvu ya dhambi ni Torati”. Lakini Bwana Yesu alipokuja na kutoa uhai wake pale Kalvari, na kufufuka na kupaa mbinguni..alituachia ahadi ya Baba, ambayo ni Roho Mtakatifu.. Kwa huyo hatuishi kwa Sheria. Na hatuwi chini ya sheria..Huyo anatusaidia kushinda dhambi pasipo sheria…Maana yake ni kwamba sheria isema kwamba usizini, au isiseme bado Dhambi haina nguvu juu yetu. Hiyo ni nguvu ya kipekee sana  na zawadi isiyoelezeka. Na hapa pia ndio utaona umuhimu wa Yesu Kristo. Kama sio kuja, ahadi hii tusingeipata…Ingekuwa kwa jinsi sheria zinavyoongezeka ndivyo na dhambi ingetulemea sana. Lakini wote waliompokea Kristo na kupokea Roho wake mtakatifu, wanapewa uwezo wa kipekee kushinda ndambi.

Hivyo kama hujampokea Kristo ndugu yangu..tumaini lako lipo kwa nani?..Unafikiri utaweza kushinda zinaa kwa nguvu zako?, unafikiri utaweza kuushinda ulevi? Au usengenyaji?..Hutaweza..na kwa jinsi utakavyozidi kujiwekea sheria kwamba sitafanya hivi au sitafanya vile, ndivyo unavyozidi kujimaliza..kwasababu nguvu ya dhambi ipo katika hizo sheria unazojiwekea…kwasababu utakapojiwekea sheria ya kwamba kesho sijakunywa pombe na humtaki Yesu, hiyo sheria uliyojiwekea utavumilia siku ya kwanza, pengine na ya pili.. lakini zitakapopita siku kadhaa utapata kiu ambayo hujawahi kuipata.. na utalewa mara mbili Zaidi ya ulivyokuwa unalewa. Kwasababu hiyo basi..mpokee Kristo leo, wokovu ni bure ili upate uwezo wa kushinda dhambi, na pia uepukane na UCHUNGU WA MAUTI.. ambao utawapata wale wote ambao hawajampokea Yesu baada ya kumaliza maisha haya. Baada ya kutubu, tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu Kristo, ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu (Matendo 2:38, Matendo 8:16). Na Roho Mtakatifu atakutia muhuri..

Bwana akubariki

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kuume, maana yake nini?

TAFUTA KUJUA MAMBO YAJAYO

KATIKA SIKU HIYO WATASEMA,HUYU NDIYE BWANA TULIYEMNGOJA.

UBATIZO NI NINI NA ULIO SAHIHI NI UPI?

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/10/17/nini-maana-ya-uchungu-wa-mauti-ni-dhambi-na-nguvu-za-dhambi-ni-torati/